MWILI WA MWANAFUNZI ALIYEZAMA BWAWANI MKOANI NJOMBE KWA SIKU 5 WAPATIKANA

  Picha ya Bwawa toka Maktaba.
Hatimaye Mwili wa Mwanafunzi wa Darasa la Saba wa Shule ya Msingi Matembwe Filbert Luwanja Umepatikana Katika Bwawa la maji Kijijini Hapo,Ikiwa ni Zaidi ya Siku Tano Tangu Alipozama.

Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Itundu Bw Justin Mfugale Amesema Mwili Huo Umepatikana Jana Majira ya Saa Moja Jioni Baada ya Wakazi Wawili wa Kijiji Hicho Kuuona Ukielea Ikiwa ni Baada ya Jitihada za Muda Mrefu za Kuutafuta Mwili Huo.

Amesema Mazishi ya Mtoto Huyo Yanatarajiwa Kufanyika Leo Saa Saba Mchana Kijijini Hapo na Kuwaomba Wananchi Kuendelea Kushirikiana Katika Kukabiliana na Majanga Yanayojitokeza Kijijini Hapo.

Kwa Upande Wao Baadhi ya Mashuhuda na Wananchi Kijijini Hapo Wameiomba Serikali Kuongeza Nguvu Katika Uimarishaji wa Vitengo Vya Uokozi na Majanga na Ili Kuweza Kuokoa Maisha ya Watu Wakati Ajali Kama Hizo Zinazopotokea.

Mtoto Filbert Luwanja Alizama July 24 Mwaka Huu Majira ya Saa Nane Mchana Wakati Akiongelea na Wenzake Wawili Huku Wataalam wa Kuongelea na Kuzama Majini Wakionekana Kuwa Tatizo Sugu Mkoani Njombe .

Siku chache zilizopita mwaka huu wananchi wa mitaa ya Kibena  walipatwa na simanzi ya kuzama kwa kijana mmoja Mexon Nyekelela Chota ambaye alizama kwenye bwawa la maji la kampuni ya Tanwat na hatimaye alipatikana baada ya siku Sita. 

credit matukio na Ngilangwablog


LORI LA MAGOGO LAUA MAFINGA MKOANI IRINGA


Hii ndiyo hali halisi ya tukio
Mkazi mmoja (Jina halijafahamika) wa kijiji cha Itimbo amefariki papo hapo maeneo ya kinyambo katika mji mdogo wa Mafinga. 
Ajali hiyo iliyotokea majira ya mchana wakati marehemu akiwa pembeni mwa barabara alijikuta kavamiwa na tela la gari la magogo,

Imesemekana kuwa gari la magogo lilipofika kwenye bamsi tela lake lilichomoka na kusababisha ajali hiyo mbaya sana.
NA Mafingaonline



MWALIMU WA HISABATI ABAMBWA CHINI YA KITANDA CHA MWANAFUNZI WAKE WA KIKE

Mwalimu huyo akiwa amefungwa pingu chini ya ulinzi wa polisi.
Mwalimu wa somo la Hisabati amebambwa akiwa amejificha chini ya kitanda cha mmoja wa wanafunzi wake mwenye umri wa miaka 16.

Mwalimu huyo ambaye hakutajwa jina, mwenye miaka 35, aligundulika pale mama wa binti huyo aliporejea nyumbani kumtazama binti yake katika siku ya mwisho ya muhula.
 
Alikamatwa na Polisi wa Greater Manchester kwa tuhuma za kutumia vibaya nafasi yake ya uaminifu kisha akaachiwa kwa dhamana lakini amesimamishwa kazi.
 
Mama huyo aliwabamba wawili hao katika chumba cha binti yake baada ya kurejea kwenye nyumba ya familia iliyoko Bolton, Manchester, katika siku ya mwisho ya binti huyo ya muhula.
 
Chanzo kimoja kilieleza: "Wawili hao walirejea nyumbani kwa binti huyo sababu walijua hakuna yeyote angeweza kuwapo pale.
 
"Lakini mama huyo alikuja nyumbani mapema kuliko ilivyodhaniwa na kuwabamba.
"Alikwenda chumbani kwa binti yake na kukuta mwalimu huyo akiwa amejificha chini ya kitanda. Ulikuwa mshituko mkubwa. Mama huyo alipagawa."
 
Mwalimu huyo ameachiwa kwa dhamana na polisi hadi Agosti 15. Haikufahamika kama amesimamishwa na shule yake.
 
Msemaji wa Polisi wa Greater Manchester  alisema: "Polisi wa Greater Manchester wanafanya uchunguzi baada ya mwanaume mmoja kuwa amekutwa kwenye chumba cha msichana wa miaka 16.
 
"Ijumaa, Julai 19, polisi waliitwa sehemu fulani katika eneo la Bolton kufuatia kuhusiana na ustawi wa binti wa miaka 16 ambaye anaishi katika sehemu hiyo.
 
"Maofisa walifika na baadaye siku hiyo mwanaume mwenye umri wa miaka 35 alikamatwa kwa tuhuma za kukiuka maadili ya nafasi yake.
 
"Ameachiwa kwa dhamana hadi Agosti 15, mwaka huu akisubiria hatua zaidi.
 
"Maofisa Polisi wa Greater Manchester na taasisi kadhaa katika eneo la Bolton wanachunguza mazingira yaliyochangia tukio hilo. Uchunguzi huu pia utatazama mambo yoyote ya ulinzi ambayo yanahitaji kujadiliwa na kuona kama kuna makosa yoyote yametendeka."
 
Tukio hilo limekuja takribani mwezi mmoja baada ya mwalimu wa shule aliyeoa, Jeremy Forrest kufungwa jela miaka mitano na nusu na Mahakama ya Lewes kwa kuteka mtoto mmoja baada ya kutoroka kutoka Ufaransa na mwanafunzi wa miaka 15.
 
Muathirika wake, sasa miaka 16, ameshikilia msimamo wa kubaki upande wa mtuhumiwa na wawili hao wamepanga kufunga ndoa mara atakapoachiwa kutoka gerezani.
 
chanzo:ziro99 blog


CCM YAIPONGEZA SERIKALI KUKUBALI KUREKEBISHA SHERIA YA TOZO YA LAINI ZA SIMU


NA MWANDISHI WETU
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza serikali, kwa uamuzi wake kurejesha bungeni kwa ajili ya mdajala zaidi, muswada wa sheria ulioanzisha kodi mpya ya tozo ya sh. 1,000 kwa laini ya simu.

Taarifa ya CCM iliyotolewa leo mjini Dodoma, na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye imesema uamuzi huo umedhihirisha kwamba serikali inawasikiliza na kuwajali wananchi wake.


Akiripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari leo, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa amekaririwa akisema kwamba mjadala kuhusu muswada wa sheria ya kodi hiyo ya tozo hiyo utafanyika wakati wa mkutano wa Bunge unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.


Baada ya kupitishwa na bunge Juni mwaka huu, na utekelezwaji wake kuanza rasmi Julai mwaka huu, CCM ilikuwa miongoni mwa wadau waliopinga vikali kuanzishwa kwa kodi ya tozo hiyo, ikieleza kwamba ni mzigo na usumbufu usio wa lazima kwa watumiaji wa simu ambao wengi matumizi yao ni ya kawaida.


Katika taarifa hiyo, CCM imesema kwa kuwa wabunge wengi ni wa chama hicho, watumie fursa hiyo kuhakikisha sheria ya tozo hiyo inaondolewa na wakati huohuo watumie uwezo wao wote kuhakikisha wanaishauri serikali vizuri kupata njia mbadala itakayotumika kuziba nafasi itakayokuwa imeachwa kwa kuondolewa tozo hiyo.


"Kimsingi hatua hii imetupa faraja na hivyo CCM inaipongeza Serikali kwa kuamua kusitisha sheria ya kodi ya tozo hiyo ya sh. 1,000 kwa laini ya simu kwa kuwa ingesababisha usumbufu na adha isiyo ya lazima kwa wananchi", imesema CCM katika sehemu ya taarifa yake.


WAALIMU NCHINI KENYA WATISHIA KUGOMA TENA

Wilson Sossion
Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion. 

CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kimetishia kuitisha mgomo mwingine iwapo walimu hawatalipwa mishahara yao ya Julai.
Viongozi wa chama hicho wamesema tayari wamewasilisha ilani kwa serikali, na watachukua hatua Jumanne ijayo bila kutoa ilani nyingine yoyote.

Kwenye kikao na wanahabari katika afisi za Knut Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho Mudzo Nzili, amesema serikali imedhihirisha haiwezi kuaminika, kwa kuwa imeenda kinyume na makubaliano yao yaliyopelekea kusitishwa kwa mgomo uliodumu kwa siku 24.

“Tuliweka makubaliano ya kurejea kazini na mwajiri, na yalishuhudiwa na waziri wa leba pamoja na wakuu wengine wa serikali. Makubaliano lazima yaheshimiwe na pande zote mbili za mwajiri na mwajiriwa,” alisema.

Kulingana na Bw Nzili, walimu walikubali kuongeza muda wa muhula ili kujaza kipindi kilichopotezwa wakati wa mgomo, huku TSC ikikubali kuwa walimu hawataadhibiwa kwa kuhusika kwenye mgomo.

Uamuzi wa TSC kutolipa walimu waliohusika kwenye mgomo ulitokana na pendekezo lililowasilishwa kwao na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), iliyodai si haki kwa mfanyakazi kulipwa ilhali hakufanya kazi anayolipiwa.

Bw Nzili alisema inashangaza kuwa serikali ilikubali kuwalipa tu marupurupu ya Sh11.5 bilioni kwa awami ya miaka mitatu, ilhali inataka kuchukua Sh13bn ambayo walimu wangelipwa mwezi huu.

Chama hicho pia kilisema TSC imekiuka sheria kwa kuchukua hatua hiyo, kwani makubaliano yao yalisajiliwa katika Mahakama ya Viwanda ambayo sasa ina mamlaka ya kusimamia utekelezaji wake.

Isitoshe, mwenyekiti wa Knut Wilson Sossion, aliongeza tume hiyo imekiuka sera zake za uadilifu kuhusu jinsi ya kuadhibu utovu wa maadili.

Kulingana na Bw Sossion, walimu wanaolengwa kuadhibiwa wangepewa nafasi ya kujitetea kabla hatua yoyote kuchukuliwa dhidi yao.

“Hakuna mwalimu aliyesikizwa, ilhali TSC imechukua hatua ya kukata mishahara yao. Tunashangaa walichukua hatua hii kwa msingi gani,” alisema.

Septemba
Huku shule zikitarajiwa kufungwa Agosti 16, Bw Sossion alisema wanaweza kugoma hadi Septemba ikiwa hilo litahitajika.

“Walimu ni binadamu na hawana mbinu nyingine ya kujipatia riziki, na huku tuko na serikali ambayo ni mbaya zaidi ya ile ya mkoloni na zingine zilizotangulia,” alisema Bw Sossion.

Kamati ya Ushauri ya chama hicho ambayo ndiyo kuu zaidi, inayojumuisha wanachama 500 kutoka kila tawi nchini, inapangiwa kukutana Jumatatu na kuamua hatua itakayochukuliwa.
 
Bw Sossion alisema hawatashtushwa na kufungiwa gerezani, ikiwa hiyo itapelekea walimu kutendewa haki.


WANAKIJIJI WAFANYA MAOMBI KUJITAKASA KUFUATIA TUKIO LA KUBAKWA KWA PUNDA HADI KUFA KIJIJINI HAPO

Punda
WAKAZI wa kijiji kimoja Kaunti ya Murang’a ambapo inashukiwa punda alibakwa hadi kufa walifanya maombi mnamo Jumatano hii ili kujitakasa.
Wakiongozwa na wahubiri kutoka makanisa kadhaa kutoka sehemu hiyo, wakazi wa kijiji cha Nyati, Lokesheni ya Kamahuha katika eneo bunge la Maragua walikashifu kitendo hicho na kumwomba Mungu msamaha.

Mhubiri Joseph Kamande wa dhehebu la Akorino eneo la Kamahuha alilinganisha kitendo hicho na miji ya Sodoma na Gomorrah katika Kitabu cha Mwanzo kwenye Biblia.

“Hili ni jambo la kushangaza na tunafaa kuomba Mungu atusamehe, hatutaki kijiji chetu kiwe kama Sodoma na Gomorah,” alisema Mhubiri Kamande akiwahutubia wakazi katika uwanja wa Nyayo ambapo kulitokea kisa hicho.

Inadaiwa wanamme ambao idadi yao haijulikani walimchafua punda huyo wa kiume hadi akafa wakati wa usiku.

Mnyama huyo wa thamani ya Sh15,000 aliyekuwa anamilikiwa na Bw Peter Murigi alipatikana akiwa amefungiliwa chini ya mti wa mwembe akiwa amekufa katika uwanja wa Nyayo huku mipira 10 ya kondomu ambayo ilikuwa imetumiwa ikiwa imetapakaa mahali hapo.

Kesha
Cha kushangaza ni kuwa kisa hicho kilitokea mita chache tu kutoka kwa kanisa moja ambapo maombi ya kesha yalikuwa yanafanyika.

“Hatujui ni shetani mgani amewashika wanamme wetu na sote tuko hatarini ya kunajisiwa na waliochafua punda huyo,” alisema Bi Esther Muthoni huku majonzi ya huzuni yakimtoka.

“Hizi ni siku za mwisho ambazo zilitabiriwa na manabii wa Biblia na tunaomba Mungu atusaidie,” alilia Bi Muthoni.
Na SAMUEL KARANJA


ZIARA YA WAZIRI MKUU WA THAILAND BI YINGLUCK SHINAWATRA KATIKA HIFADHI YA SERENGETI MKOANI MARA

 Maandalizi ya Mapokezi ya Waziri Mkuu waThailand Yingluck Shinawatra
 Makanda wakiwa tayari kwa Mapambano
 Waziri wa Mali asili na Utalii nchini Baloz Hamis Kagasheki akipokewa na Mkurugenzi wa TANAPA Allan Kijaz
  Waziri wa Mali asili na Utalii nchini Baloz Hamis Kagashek wakikumbatiana kwa furaha na Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw John Tuppa

KUONA ZAIDI BOFYA HAPA


MAJANGA:MWANASHERIA AISHITAKI ISRAEL KWA KIFO CHA YESU KRISTO

Maajabu mengi sana hugundulika duniani kila siku, lakini kuna kila uwezekano kuwa ajabu lililoko kwenye story hii likawa ajabu la kipekee. 

Mwanasheria mmoja ambaye ni raia wa Kenya ameibuka na kuzishitaki serikali za Israel na Italia kwa kosa la kuhusika kwenye kifo cha Yesu Kristo
 
Mwanasheria huyo Dola Indidis amefungua kesi hiyo kwenye mahakama ya dunia The Hague kule kule ambako rais wa taifa Lake (Kenya ) Mh Uhuru Kenyatta na Makamau wake William Ruto nao wana kesi ya kujibu.

Mwanasheria huyo amesema kuwa lazima serikali za mataifa hayo ziwajibike kwa kitendo cha unyama alichofanyiwa mwanzilishi wa dini ya madhehebu ya Kikristo ambaye ni Yesu aliyesulubiwa msalabani pasipo kuwa na hatia yoyote ya kustahili adhabu hiyo. 

Dola Indidis amefungua shitaka hilo dhidi ya Mfalme wa uliokuwa Ufalme wa Roma Tiberio pamoja na watawala waliokuwa chini yake wakati huo wakiwemo Pontio Pilato na Mfalme Herode pamoja na viongozi wa kiyahudi wakiwemo mafarisayo na masadukayo ambayo kwa pamoja walikula njama ya kumuua Bwana Yesu.


Indidis anasema kuwa ushahidi uko kwenye kitabu kitakatifu Cha Biblia ambayo kila mmoja anafahamu kuwa haisemi uongo . Kwa kuwa wafalme na watawala waliohusika na kitendo hicho hawako hai serikali ambazo mipaka yake ndio ile ile ya iliyokuwa falme ya Roma iliyokuwa madarakani kipindi hicho zitawajibika kwa niaba.

Dola Indidis anasema kuwa vitendo alivyofanyiwa Yesu ni vitendo vya kinyama na ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nay eye kama mwanadamu anahisi kuwa ni jukumu lake kulinda na kutetea heshima ya Yesu Kristo.


Hata hivyo msemaji wa mahakama ya Dunia ambaye hakutajwa utambulisho wake amesema kuwa hakuna kipengele cha kisheria ambacho kinaweza kuruhusu kusikilizwa kwa kesi hiyo kwani ICJ (International Court Of Justice) husikiliza kesi zinazohusu nchi dhidi ya nchi nyingine hivyo kesi hiyo haiwezi hata kufikiriwa. 

Indidis kwa upande wake bado ana imani kuwa ana kesi ya kuhoji na anaamini kuwa atashinda kesi hiyo.

Source: MillardAyo


MFANYAKAZI WA KAMPUNI YA MWANANCHI APIGWA RISASI




 Jessica Ngassa akimuhudumia mumewe, Jackson Ngassa ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Idara ya Usambazaji wa Magazeti aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi na majambazi  Jumamosi usiku jijini Dar es Salaam.


Watu ambao wanasadikiwa kuwa ni majambazi wamemjeruhi kwa risasi mfanyakazi wa Idara ya Usambazaji ya Mwananchi Communications Limited,  Jackson Ngassa.
 
Tukio hilo lilitokea juzi Jumamosi saa 4 usiku eneo la Tabata Matumbi baada ya watu hao kumfuatilia Ngassa tangu alipokuwa anatoka ofisi za Mwananchi eneo la Tabata Relini.
 
Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (Moi), Ngassa alisema wakati akitoka ofisini siku hiyo aliona pikipiki tatu zikiwa nyuma yake lakini hakuhisi kama zilikuwa zinamfuata mpaka walipofika taa  za kuongozea magari za Tabata Dampo.
 
“Nilipofika Tabata Dampo nilihisi kufuatiliwa kwa sababu kila nilipopunguza mwendo nao walipunguza mpaka nilipofika Matumbi ndipo nikasikia wakiniambia simama haraka na kisha wakapiga risasi moja ambayo ilitoboa tanki la mafuta la pikikipiki,” alisema Ngassa.
 
Alisema baada ya kuona hivyo akataka kukimbilia Benki ya Access iliyoko eneo hilo la Matumbi lakini kabla hajafanya hivyo pikipiki nyingine ilimzuia kwa mbele na ghafla akasikia risasi ambayo ilipasua sehemu ya goti mguu wake wa kulia.
 
Hata hivyo, Ngassa alisema begi hilo halikuwa na pesa zozote zaidi ya  kadi ya benki na magari ya kuchezea watoto aliyowanunulia watoto wake
 
Kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa kuunganisha mifupa iliyovunjika kwani risasi aliyopigwa iliingia na kutoka upande wa pili.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari alikwishamtembelea majeruhi katika hospitali ya Muhimbili alikolazwa


WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI KITAIFA MWAKA HUU KUFANYIKA JIJINI MWANZA


Mhe Pereira Silima Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa Usalama Barabarani leo amezungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara na kutoa taarifa ya maadhimisho ya Kitaifa ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Mkoani Mwanza 23/09/13 - 27/09/13. 
======  =======  =======


TCRA YATAMBUA RASMI MCHANGO WA MITANDAO YA KIJAMII (BLOGS),WAZINDUA KAMPENI YA KUHAMASISHA MATUMIZI MAZURI YA MITANDAO YA KIJAMII

 Msanii wa muziki wa asili Tanzania ambaye pia ni msanii wa maigizo na filamu, Mrisho Mpoto akizungumza jambo mbele ya waaandishi wa habari na wamiliki wa blogs mbalimbali katika uzinduzi wa matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii. Mrisho alisimama kuzungumza dakika chache baada ya wimbo alioimba na Banana Zoro kuzinduliwa, unaojulikana kama 'Futa, Delete Kabisa'. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),John Nkomo katika uzinduzi huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkomo, akizungumza mbele ya wamiliki wa blogs mbalimbali Tanzania, waandishi wa habari katika warsha ya kampeni ya kuzindua matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuhamasisha suala zima la maendeleo.

Prof.Nkomo amesema kuwa kwa sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya intaneti kwa Watanzania walio wengi kutoka watumiaji laki tatu miaka mitatu iliyopita hadi watumiaji milioni 7.6 kwa takwimu za hivi karibuni.Amesema kuwa wengin wa watumiaji wa Intaneti,matumizi yao ni katika kujifunza na kujielimisha pamoja na matumizi ya mitandano ya kijamii kama vile facebook,Twitter,BBM,Linkedin na Blog mbalimbali zinazotoa habari mbalimbali zikwemo za kimaendeleo,burudani pamoja na michezo.




 Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), waandishi mbalimbali wa habari pamoja na wamiliki wa mitandao ya kijamii, Blogs, wakisikiliza maneno mazuri kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Tanzania, Profesa John Nkomo, hayupo pichani. Hii ni sehemu maalumu ya kuonyesha kuwa TCRA wanatambua mchango wa mitandao ya kijamii, hususan blogs na wamiliki wao kwa ujumla.
Meneja Uhusiano wa TCRA,Innocent Mungi akiwakaribisha wadau mbalimbali wa mambo ya habari za kwenye mitandao,kuhusiana na uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi mazuri ya Mitandao ya Mawasiliano,Warsha hiyo imefanyika leo Makao makuu ya Ofisi hizo,zilizopo barabara ya Sam Nujoma jijini Dar.
 Wadau wa mawasiliano wa mitandao ya kijamii, blogs, wakisikiliza hoja mbalimbali zilizotolewa na viongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA katika uzinduzi wao wa matumizi mazuri ya mitandao kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo ya Taifa.


MWANDISHI WA HABARI ADHALILISHWA UJIO WA WAZIRI MKUU WA THAILAND


Mpigapicha wa New Habari Anthony Siyame akidhalilishwa na askari wa Idara ya Usalama wa Taifa wakati wa mapokezi ya Waziri Mkuu wa Thailand, Yungluck Shinawatra baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam  jana,Julai 30 2013.
(Picha kwa hisani ya Selemani Mpochi) .
 
Cha ajabu ni kwamba wakati mpigapicha huyo akifanyiwa visa na kushindwa kufanya kazi yake kwa utulivu wanahabari wengine wa kigeni walipewa ushirikiano mzuri na kufanya kazi yao bila bughuza  kabisa.


RAIS MUGABE KUKUBALIANA NA MATOKEO ENDAPO ATASHINDWA

Rais Robert Mugabe.

RAIA wa Zimbabwe wanapiga kura katika uchaguzi wa Urais unaotajwa kuwa na ushindani mkali huku kukiwa na madai ya udanganyifu. Rais Robert Mugabe wa miaka 89 amesema atang’atuka ikiwa yeye na chama chake cha Zanu-PF watashindwa.

Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na chama chake cha Movement for Democratic Change (MDC) wamelalamikia Zanu-PF kwa kuhitilafiana na utaratibu wa uchaguzi ili kunyakua ushindi, lakini chama tawala kimekanusha madai hayo.Shughuli za kampeini zimekua ghasia zozote huku kukiwa na visa vichache sana vya kuwatisha wapiga kura.

Vyama vya Zanu-PF na MDC viliunda serikali ya muungano mwaka wa 2008 baada ya muafaka wa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi kufuatia matokeo ya Urais yaliyozua utata. Bw. Tsvangirai alishinda awamu ya kwanza, lakini akajiondoa kwa raundi ya pili akilalamikia mashambulizi yaliyolenga wafuasi wake.

Serikali ya Zimbabwe imewapiga marufuku waangalizi wa magharibi kuchunguza uchaguzi wa leo. Hata hivyo Muungano wa Afrika (AU), Kanda ya Kusini mwa Afrika (SADC) na makundi ya kijamii nchini Zimbabwe yamekubaliwa kufuatilia jinsi uchaguzi utakavyoendeshwa.

Watu milioni 6.4 wamejiandikisha kupiga kura hii, na maelfu walijitokeza kwenye kampeini za uchaguzi. Matokeo yanatarajiwa kutolewa kwa siku tano zijazo. Mwandishi wa BBC aliyeko Harare amesema kuna foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura ikiwa siku ya mapumzoko kuhakikisha raia wanapata nafasi ya kuamua serikali mpya.

Mshindi wa moja kwa moja sharti apate asili mia 50 ya kura zote kutangazwa Rais. Ikiwa hakuna mgombea atapata kura hizo, raundi ya pili imepangwa kufanyika Septemba 11. Uchaguzi huu ndio wa kwanza kufanyika Zimbabwe chini ya katiba mpya iliyopitishwa mnamo mwezi Machi mwaka huu.
-BBC


DIWANI MTEULE WA KATA YA THEMI ARUSHA AANZA KUWATUMIKIA WANANCHI WAKE

 Picha juu na chini Diwani mteule wa kata ya Themi Arusha Ndugu Melance Kinabo(KABURU) kupitia CHADEMA akizungumza na wakina mama ambao ni wakulima wa mbogamboga waliomuita kwa simu kumuomba msaada baada ya mwenyekiti wa Mtaa wa Themi Magharibi Mzee Dions Msele - CCM kukataza matumizi ya mfereji wa kumwagia maji ktk mashamba ya kina mama wa mtaa husika bila sababu za msingi.
----
 Diwani mteule wa kata ya Themi Arusha Ndugu Melance Kinabo(KABURU) kupitia CHADEMA ameanza kazi zake rasmi kama diwani hili hali bado hajaapishwa.Leo tarehe 29 - June 2013 mishale ya saa tisa alasiri Diwani wa Themi Ndugu Kaburu aliwasili mtaa wa Fire maeneo ya magorofa ya polisi kusikiliza kilio cha kina mama ambao ni wakulima wa mbogamboga waliomuita kwa simu kumuomba msaada baada ya mwenyekiti wa Mtaa wa Themi Magharibi Mzee Dions Msele - CCM kukataza matumizi ya mfereji wa kumwagia maji ktk mashamba ya kina mama wa mtaa husika bila sababu za msingi.

Diwani huyu wa Themi kupitia Chadema  aliwahoji kina mama husika na kugundua kuwa Mwenyikiti wa mtaa hakuwa na sababu za msingi za kuwazuiya kina mama hao kuendelea na kilimo cha umwagiliaji kupitia mfereji husika.

Diwani huyu mteule akuchukua hatua ya kuhoji tatizo husika kwa mtendaji wa kata ya Themi na kugundua kuwa kina mama hawa wa Themi Magharibi wananyanyaswa na mwenyekiti wa mtaa Dions Msele - CCM na ndipo akatoa amri kuwa mfereji huo ufunguliwe na kina mama waendelee na kilimo cha mboga bila kusumbuliwa na pia ametoa ahadi ya kusimamia utengenezaji wa kalavat kwenye mfereji husika kuepusha ajali kwa watoto wa polisi wanaoishi maeneo ya Themi Magharibi karibu na chanzo cha mfereji huo ulioleta utata.


SOMA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA UALIMU 2013/2014

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Dr Shukuru kawambwa. 
---
Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.

Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
---

MAELEKEZO MUHIMU:

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Mafunzo ya Ualimu mwaka wa masomo 2013/2014 wanatakiwa kuripoti katika Vyuo walivyopangiwa tarehe 15/08/2013.

Fomu ya maelekezo (joining instruction) itatumwa kwa mhusika kupitia anuani yake. Aidha, fomu hizi zinapatikana pia kwenyetovuti hii  kwa kubofya katika link ya Chuo husika.
Wanafunzi wanatakiwa kufika Vyuoni wakiwa na mahitaji yafuatayo:
  1. Vyeti halisi vya Baraza la Mitihani la Tanzania kidato cha NNE na SITA kulingana na kozi husika;
  2. Ada ya muhula wa kwanza sh.100,000/= au ya mwaka sh. 200,000/=;
  3. Sare ya Chuo kulingana na maelekezo ya Chuo husika; na
  4. Fedha za tahadhari chuoni na matumizi binafsi.

Mkuu wa Chuo anatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosajiliwa Chuoni ni wale waliopo kwenye orodha hii tu na SI vinginevyo.

Usajili wa waliochaguliwa kujiunga na Vyuo utafungwa tarehe 25/08/2013 saa 12.00 jioni.

*Bofya namba 1 au 2 hapa chini ili kupakua nakala yenye orodha ya majina

 
  1.  WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA CHETI 2013/2014 (1.64 MB) 
  2.  WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA STASHAHADA 2013/2014 (997.5 kB)


WATOTO WENGI HUKATISHA MASOMO SABABU YA MIMBA ZA UTOTONI

Na Anna Nkinda- Gaborone,  Botswana.
 
Imeelezwa kwamba ndoa za utotoni ni moja ya sababu inayowafanya watoto wa kike kukatiza masomo yao huku asilimia 24 ya watoto hao  wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 18 wakiolewa katika nchi zilizopo kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kutokana na umri wao watoto hao walitakiwa kuwa wanafunzi wa shule za Sekondari na siyo kuishi na wanaume hivyo basi jitihada za pamoja zinatakiwa ili kuhakikisha kuwa sheria na sera za kumlinda  mtoto wa kike na kumjengea mazingira salama ya kuishi zinatungwa.

Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wajumbe waliohudhulia mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya Lansmore Masa Square iliyopo mjini Gabarone nchini Botswana.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa mkutano huo unafanyika kipindi ambacho jitihada kubwa zinafanywa na nchi wanachama wa EAC na SADC ili kuhakikisha kuwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na mimba za utotoni zinapungua.

“Taarifa ya Kanda inaonyesha kuwa Ugonjwa wa Ukimwi ni changamoto kwa vijana wetu kwani  kati ya maaambukizi mapya 620,000 yanatokea kila mwaka  kuna  vijana wadogo wenye umri wa miaka 15hadi 24 kati ya hao asilimia  60% ni wasichana hii inamaana kuwa kwa  saa moja wasichana 31 na wavulana 21 wanapata maambukizi”, alisema Mama Kikwete

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa kuwa mtoto wa kike anapata elimu  ingawa idadi ya watoto wa kike ni kubwa katika elimu ya msingi lakini wakifika elimu ya sekondari  idadi yao inapungua.

Mama Kikwete alisema, “Ingawa kuna jamii zingine ni mwiko kwa wazazi kuongea na watoto wao kuhusu afya ya uzazi lakini watoto hawa wanatakiwa kufahamu afya ya uzazi na mabadiliko ya miili yao  ili waweze kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi na mimba za utotoni”.
           
Alisema nchini Tanzania kupitia Taasisi ya WAMA kuna kampeni isemayo mtoto wa mwenzio ni wako mkinge dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ambayo inaihamasisha jamii kuwalinda watoto pia taasisi hiyo inafadhili  elimu ya sekondari kwa watoto ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

WAMA imejenga mabweni ya wasichana katika shule za Sekondari, kutoa vifaa vya maabara,huduma ya maji safi na  kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi pia kupitia klabu mbalimbali za wanafunzi mashuleni wametoa  elimu ya uzazi na jinsia ili vijana waweze  kujilinda na maambukizi ya HIV na kujikinga na mimba za utotoni.

Akifungua mkutano huo Prof. Alaphia Wright  kutoka UNESCO alisema mambo watakayoyajadili  yatapelekwa katika Serikali za nchi husika ili ziweze kuongeza msukumo wa kisera na kibajeti na  kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto za afya na uzazi zinazowahusu vijana.

“Kama mnavyofahamu nchi zetu za kanda ya  Mashariki  na Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na tatizo la idadi kubwa ya maambukizi mapya ya VVU kwa vijana hivyo basi elimu ya afya ya uzazi inatakiwa kutolewa  kwao  ambayo itawasaidia kupambana na ugonjwa huu pia wanahitajika  kupata taarifa sahihi ambazo zitawasaidi kuchagua nini cha kufanya kutokana na jinsia zao na matarajio yao ya baadaye”, alisema Prof. Wright.

Kwa upande wake Msaidizi wa waziri wa Afya wa Botswana Gaotlhaetse Matlhabaphiri alisema katika kipindi cha miaka 30 nchi nyingi Duniani zimekuwa zikipambana na ugonjwa wa Ukimwi na kuweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani hivi sasa jamii inaelewa jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Tunakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na idadi kubwa  ya watu ambayo haiendani na huduma zinazotolewa za kuzuia maambukizi ya HIV, ukosefu wa upatikanaji wa huduma za afya, hali mbaya ya uchumi ambao inaongeza kasi ya maambukizi ya ugnjwa huo hasa kwa vijana”, Matlhabaphiri.

Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS), UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO), UNESCO lengo kuu likiwa ni  kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia waweze kufahamu zaidi  ugonjwa Ukimwi.


RAIS JK NA WAZIRI MKUU WA THAILAND WASHUHUDIA UTILIAJI SAINI HATI 4 ZA MAKUBALIANO


Rais Jakaya Kikwete na waziri mkuu wa serikali ya Thailand bibi Yingluck Shinawatra wameshuhudia utiliaji saini wa hati nne za makubalino ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ikiwemo makubaliano ya kuhamisha wafungwa  pamoja  na ushirikiano katika teknolojia.
 
Tukio hilo limetokea Ikulu jijini Dar es Salaam,baada ya kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa serikali ya Thailand kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam na kupokewa na mwenyeji wake rais Jakaya Kikwete huku zaidi ya wanawake 200 wakiwa wamejipanga mistari kuelekea Ikulu wakipungia kwa bendera za Tanzania na Thailand ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kiongozi huyo.
 
Katika hati ya makubaliano ya kwanza, mbele ya viongozi hao, mwakilishi wa serikali ya Thailand ametiliana saini na kukabirishana hati na naibu waziri wa mambo ya ndani mheshimiwa Pereira Silima kuhusu kuhamisha wafungwa, ambapo waziri wa fedha na uchumi mheshimiwa Dkt William Mgimwa amesaini hati mbili za makubaliano ya kuhamasisha na kulinda uwekezaji pamoja na ushirikiano wa teknolojia kati ya nchi hizo mbili. 
 
Ambapo katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini bwana Eliakim Maswi amesaini hati ya makubaliano ua ushirikiano na mkurugenzi mkuu wa taasisi gm ya nchini Thailand katika maswala ya nishati na madini.
 
Bibi Yingluck Shinawatra yuko nchi kwa ziara ya siku tatu ya kiserikali ambapo akiwa hapa nchni anatarajiwa kutoa msimamo wa nchi yake kwa bara la Afrika,kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam kuelekea katika mbunga ya wanyama ya Serengeti ambapo akiwa huko atasaini hati makubalinao ya ushirikiano wa mbuga za wanyana na umiliki wa wanyamapori kati ya Tanzania na Thailand, tarehe 1 Agosti anatarajiwa kuondoka nchni kuelekea Entebe nchni Uganda.


WATAALAMU WA UDHIBITI WA CHAKULA NA DAWA BANDIA WAKUTANA

 
Wataalamu wa vyombo vya udhibiti wa vyakula na dawa feki katika nchi 16 mashariki na kusini mwa Afrika wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili changamoto na kuweka mfumo wa pamoja chini ya uratibu wa shirika la afya duniani unaolenga kuliepusha bara la Afrika kugeuzwa dampo la bidhaa feki duniani.
Kwa mujibu wa taarifa ya meneja wa mradi wa udhibiti kutoka makao makuu ya shirika la afya duniani yaliyopo Geniva nchini uswis Bw. Michale Deats amesema mkutano huo wa siku tatu mbali na kujadili changamoto za udhibiti pia mkutano huo utaweka mikakati shirikishi ya kuhakikisha Afrika inafunga njia zote za uingizaji bidhaa za aina hiyo kwa usalama wa afya za binadamu huku akifafanua tatizo hilo na hatua za udhibiti katika eneo la Afrika na dunia kwa ujumla.
Awali katika taarifa ya mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya chakula a dawa nchini tfda bw. Hiit sillo pamoja na kueleza hatua za mamlaka katika udhibiti alipongeza shirika la afya duniani who kwa kuiteuwa tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu akieleza fulsa hiyo kuchochea mikakati ya mamlaka na taifa katika kudhibiti uingizaji wa vyakula na dawa vilivyopo chini ya kiwago.
Mkutano huo ulifunguliwa na naibu waziri wa afya na ustawi wa jamii dk. Seifu rashidi akijipambanua kuchukua hatua kali dhidi ya wanaokiuka taratibu na wakati huo akijikuta katika wakati mgumu kujibu maswaili ya waandishi wa habari yaliyomtaka kueleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya mmiliki wa kiwanda kilichothibitika kutengeneza Arv feki na kuelekeza lawama zake kwa mkurugenzi wa mashtaka dpp anayemtaja kutambua wajibu wake.
NA ITV


MGOMO WA WANAFUNZI LUTHERAN JUNIOR SEMINARY MOROGORO WAINGIA SIKU YA PILI

 
Mgomo wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lutheran junior Seminary inayomilikiwa na kanisa la kilutheri Tanzania umeingia siku ya pili baada ya wanafunzi  kugoma kutwa nzima kuingia madarasani na kuandamana katika barabara ya Morogoro Dar es Salaam na kulazimu jeshi la polisi kuingilia kati kuzuia maandamano.

Wanafunzi hao wamesikika wakiimba wanataka kuonana na askofu mkuu wa KKKT Alex Malasusa huku wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali ambapo wakiwa njiani katika barabara ya Morogoro Dar es Salaam jeshi la polisi walisitisha maandamano kwa madai ya kutofuata taratibu za kuomba kibali.

Wanafunzi hao walilazimika kurudi shuleni kwa maandamano wakisindikizwa na ulinzi wa jeshi la polisi lakini walipofika shuleni hapo mambo yalionekana kuwa magumu zaidi 

hata hivyo hawakutaka kusikiliza walimu na ikamlazimu mkuu wa wilaya Saidi Amanzi kufika shuleni hapo na kuzungumza na uongozi wa shule ambapo amesema inawalazimu kusubiri viongozi wa KKKT kutoka makao mjini Arusha.

Kwa upande wao wanafunzi wamesema wataendelea na mgomo huo kutokana na ahadi zilizotolewa kushindwa kutekelezeka na kushinikiza kutaka kuonana na askofu mkuu Alex Malalasusa ili awasaidie kutatua kero zao.
 
CHANZO:ITV


JUMA KASEJA ATAJA TIMU ATAKAYOICHEZEA HIVI SASA

Nahodha wa Taifa Stars Juma Kaseja yuko mbioni kwenda kukipiga katika klabu ya FC Lupopo inayoshiriki ligi kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Wakala wa klabu hiyo amesema tayari wameshakubaliana baadhi ya mambo na mchezaji huyo na yamesalia masuala machache kabla ya Kaseja ambaye ni mchezaji huru kwa sasa kujiunga na timu hiyo.


HENRY KILEO NA WENZAKE WAPANDISHWA TENA MAHAKAMANI TABORA HII LEO


Leo mawakili wa pande zote wametoa maelezo yao huku Upande wa Henry Kilewo na wenzake wakitaka mahakama Kuu ifute mashtaka yanayowakabili kutokana na kutokuwa na uhalali wa kisheria. 

Mahakama Kuu kanda hiyo ya Tabora imepanga kuwa itatoa maamuzi yake juu ya shauri hilo ifikapo Agosti Tano mwaka huu. Haki huwenda ikatendeka


WAZIRI MKUU WA THAILAND AWASILI TANZANIA KWA ZIARA YA SIKU 3

 Waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra akiwasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu leo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
  Waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra akikagua gwaride la heshima la vikosi vya ulinzi na usalama vya Tanzania mara baada ya kuwasili nchini Tanzania leo.
 Gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vya Tanzania likipita mbele ya jukwaa kutoa heshima kwa Waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra (kulia) na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete wakati wa mapokezi ya kiongozi huyo leo jijini Dar es salaam.
 Waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra akiangalia vikundi vya ngoma akiwa na mwenyeji wake rais Jakaya Kikwete leo jijini Dar es salaam.
 Rais Jakaya Kikwete (kulia) akimkaribisha Ikulu jijini Dar es salaam waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra (kushoto) mara baada ya kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.
 Rais Jakaya Kikwete (kulia) akimkaribisha Ikulu jijini Dar es salaam waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra (kushoto) mara baada ya kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.
 Waziri mkuu wa Thailand Bi. Yingluck Shinawatra akiwa katika mkutano wa pamoja na viongozi wa Tanzania Ikulu jijini Dar es salaam.
 Naibu Waziri mkuu wa Thailand ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Thailand Dr. Surapong Tovichakchaikul (kushoto) na Waziri wa Fedha wa Tanzania Mh. William Mgimwa (kulia) wakibadilishana hati za makubaliano ya kudumisha, kutunza na kuendeleza uwekezaji kati ya Tanzania na Thailand Ikulu jijini Dar es salaam.
 Rais Jakaya Kikwete akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa Tanzania na Thailand walioongozwa na Waziri mkuu wa nchi hiyo Bi. Yingluck Shinawatra ambapo Tanzania na Thailand zimesaini mikataba minne ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa, uendelezaji wa shughuli za uwekezaji, ushirikiano katika masuala ya Ufundi na ushirikiano katika sekta ya Nishati na Madini.Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.


 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo