Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion.
CHAMA cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kimetishia kuitisha mgomo mwingine iwapo walimu hawatalipwa mishahara yao ya Julai.
Viongozi wa
chama hicho wamesema tayari wamewasilisha ilani kwa serikali, na
watachukua hatua Jumanne ijayo bila kutoa ilani nyingine yoyote.
Kwenye kikao
na wanahabari katika afisi za Knut Nairobi, Katibu Mkuu wa chama hicho
Mudzo Nzili, amesema serikali imedhihirisha haiwezi kuaminika, kwa kuwa
imeenda kinyume na makubaliano yao yaliyopelekea kusitishwa kwa mgomo
uliodumu kwa siku 24.
“Tuliweka
makubaliano ya kurejea kazini na mwajiri, na yalishuhudiwa na waziri wa
leba pamoja na wakuu wengine wa serikali. Makubaliano lazima yaheshimiwe
na pande zote mbili za mwajiri na mwajiriwa,” alisema.
Kulingana na
Bw Nzili, walimu walikubali kuongeza muda wa muhula ili kujaza kipindi
kilichopotezwa wakati wa mgomo, huku TSC ikikubali kuwa walimu
hawataadhibiwa kwa kuhusika kwenye mgomo.
Uamuzi wa TSC
kutolipa walimu waliohusika kwenye mgomo ulitokana na pendekezo
lililowasilishwa kwao na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), iliyodai
si haki kwa mfanyakazi kulipwa ilhali hakufanya kazi anayolipiwa.
Bw Nzili
alisema inashangaza kuwa serikali ilikubali kuwalipa tu marupurupu ya
Sh11.5 bilioni kwa awami ya miaka mitatu, ilhali inataka kuchukua Sh13bn
ambayo walimu wangelipwa mwezi huu.
Chama hicho
pia kilisema TSC imekiuka sheria kwa kuchukua hatua hiyo, kwani
makubaliano yao yalisajiliwa katika Mahakama ya Viwanda ambayo sasa ina
mamlaka ya kusimamia utekelezaji wake.
Isitoshe,
mwenyekiti wa Knut Wilson Sossion, aliongeza tume hiyo imekiuka sera
zake za uadilifu kuhusu jinsi ya kuadhibu utovu wa maadili.
Kulingana na Bw Sossion, walimu wanaolengwa kuadhibiwa wangepewa nafasi ya kujitetea kabla hatua yoyote kuchukuliwa dhidi yao.
“Hakuna
mwalimu aliyesikizwa, ilhali TSC imechukua hatua ya kukata mishahara
yao. Tunashangaa walichukua hatua hii kwa msingi gani,” alisema.
Septemba
Huku shule zikitarajiwa kufungwa Agosti 16, Bw Sossion alisema wanaweza kugoma hadi Septemba ikiwa hilo litahitajika.
“Walimu ni
binadamu na hawana mbinu nyingine ya kujipatia riziki, na huku tuko na
serikali ambayo ni mbaya zaidi ya ile ya mkoloni na zingine
zilizotangulia,” alisema Bw Sossion.
Kamati ya
Ushauri ya chama hicho ambayo ndiyo kuu zaidi, inayojumuisha wanachama
500 kutoka kila tawi nchini, inapangiwa kukutana Jumatatu na kuamua
hatua itakayochukuliwa.
Bw Sossion alisema hawatashtushwa na kufungiwa gerezani, ikiwa hiyo itapelekea walimu kutendewa haki.