RAIA wa Zimbabwe wanapiga kura katika uchaguzi wa
Urais unaotajwa kuwa na ushindani mkali huku kukiwa na madai ya
udanganyifu. Rais Robert Mugabe wa miaka 89 amesema atang’atuka ikiwa
yeye na chama chake cha Zanu-PF watashindwa.
Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na chama chake cha Movement for
Democratic Change (MDC) wamelalamikia Zanu-PF kwa kuhitilafiana na
utaratibu wa uchaguzi ili kunyakua ushindi, lakini chama tawala
kimekanusha madai hayo.Shughuli za kampeini zimekua ghasia zozote huku
kukiwa na visa vichache sana vya kuwatisha wapiga kura.
Vyama vya Zanu-PF na MDC viliunda serikali ya muungano mwaka wa 2008
baada ya muafaka wa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi kufuatia
matokeo ya Urais yaliyozua utata. Bw. Tsvangirai alishinda awamu ya
kwanza, lakini akajiondoa kwa raundi ya pili akilalamikia mashambulizi
yaliyolenga wafuasi wake.
Serikali ya Zimbabwe imewapiga marufuku waangalizi wa magharibi
kuchunguza uchaguzi wa leo. Hata hivyo Muungano wa Afrika (AU), Kanda ya
Kusini mwa Afrika (SADC) na makundi ya kijamii nchini Zimbabwe
yamekubaliwa kufuatilia jinsi uchaguzi utakavyoendeshwa.
Watu milioni 6.4 wamejiandikisha kupiga kura hii, na maelfu
walijitokeza kwenye kampeini za uchaguzi. Matokeo yanatarajiwa kutolewa
kwa siku tano zijazo. Mwandishi wa BBC aliyeko Harare amesema kuna
foleni ndefu katika vituo vya kupigia kura ikiwa siku ya mapumzoko
kuhakikisha raia wanapata nafasi ya kuamua serikali mpya.
Mshindi wa moja kwa moja sharti apate asili mia 50 ya kura zote
kutangazwa Rais. Ikiwa hakuna mgombea atapata kura hizo, raundi ya pili
imepangwa kufanyika Septemba 11. Uchaguzi huu ndio wa kwanza kufanyika
Zimbabwe chini ya katiba mpya iliyopitishwa mnamo mwezi Machi mwaka huu.
-BBC