Na Anna Nkinda- Gaborone, Botswana.
Imeelezwa kwamba ndoa za
utotoni ni moja ya sababu inayowafanya watoto wa kike kukatiza masomo yao huku
asilimia 24 ya watoto hao wenye umri wa
kati ya miaka 15 hadi 18 wakiolewa katika nchi zilizopo kanda ya Mashariki na
Kusini mwa Afrika.
Kutokana na umri wao watoto hao walitakiwa
kuwa wanafunzi wa shule za Sekondari na siyo kuishi na wanaume hivyo basi
jitihada za pamoja zinatakiwa ili kuhakikisha kuwa sheria na sera za kumlinda mtoto wa kike na kumjengea mazingira salama ya
kuishi zinatungwa.
Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais Mama
Salma Kikwete wakati akiongea na wajumbe waliohudhulia mkutano wa kamati maalum
ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka
nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo
ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya
Lansmore Masa Square iliyopo mjini Gabarone nchini Botswana.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa mkutano huo unafanyika kipindi
ambacho jitihada kubwa zinafanywa na nchi wanachama wa EAC na SADC ili
kuhakikisha kuwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na mimba za utotoni
zinapungua.
“Taarifa ya Kanda inaonyesha kuwa Ugonjwa
wa Ukimwi ni changamoto kwa vijana wetu kwani kati ya maaambukizi mapya 620,000 yanatokea
kila mwaka kuna vijana wadogo wenye umri wa miaka 15hadi 24
kati ya hao asilimia 60% ni wasichana
hii inamaana kuwa kwa saa moja wasichana
31 na wavulana 21 wanapata maambukizi”, alisema Mama Kikwete
Alisema ili kukabiliana na tatizo
hilo jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa kuwa mtoto wa kike anapata elimu ingawa idadi ya watoto wa kike ni kubwa
katika elimu ya msingi lakini wakifika elimu ya sekondari idadi yao inapungua.
Mama Kikwete alisema, “Ingawa kuna
jamii zingine ni mwiko kwa wazazi kuongea na watoto wao kuhusu afya ya uzazi
lakini watoto hawa wanatakiwa kufahamu afya ya uzazi na mabadiliko ya miili yao
ili waweze kujikinga na ugonjwa wa
Ukimwi na mimba za utotoni”.
Alisema nchini Tanzania kupitia
Taasisi ya WAMA kuna kampeni isemayo mtoto wa mwenzio ni wako mkinge dhidi ya
ugonjwa wa Ukimwi ambayo inaihamasisha jamii kuwalinda watoto pia taasisi hiyo
inafadhili elimu ya sekondari kwa watoto
ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
WAMA imejenga mabweni ya wasichana
katika shule za Sekondari, kutoa vifaa vya maabara,huduma ya maji safi na kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya
sayansi pia kupitia klabu mbalimbali za wanafunzi mashuleni wametoa elimu ya uzazi na jinsia ili vijana waweze kujilinda na maambukizi ya HIV na kujikinga na
mimba za utotoni.
Akifungua
mkutano huo Prof. Alaphia Wright kutoka
UNESCO alisema mambo
watakayoyajadili yatapelekwa katika
Serikali za nchi husika ili ziweze kuongeza msukumo wa kisera na kibajeti
na kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto
za afya na uzazi zinazowahusu vijana.
“Kama
mnavyofahamu nchi zetu za kanda ya Mashariki
na Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na tatizo la idadi kubwa ya maambukizi
mapya ya VVU kwa vijana hivyo basi elimu ya afya ya uzazi inatakiwa kutolewa kwao ambayo itawasaidia kupambana na ugonjwa huu
pia wanahitajika kupata taarifa sahihi
ambazo zitawasaidi kuchagua nini cha kufanya kutokana na jinsia zao na
matarajio yao ya baadaye”, alisema Prof. Wright.
Kwa upande wake Msaidizi wa waziri wa
Afya wa Botswana Gaotlhaetse Matlhabaphiri alisema katika kipindi cha miaka 30 nchi
nyingi Duniani zimekuwa zikipambana na ugonjwa wa Ukimwi na kuweza kufanikiwa
kwa kiasi kikubwa kwani hivi sasa jamii inaelewa jinsi ya kukabiliana na
ugonjwa huo.
Tunakabiliwa na matatizo mbalimbali
ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya watu ambayo
haiendani na huduma zinazotolewa za kuzuia maambukizi ya HIV, ukosefu wa
upatikanaji wa huduma za afya, hali mbaya ya uchumi ambao inaongeza kasi ya
maambukizi ya ugnjwa huo hasa kwa vijana”, Matlhabaphiri.
Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS), UNFPA, Shirika la Umoja
wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO),
UNESCO lengo kuu likiwa ni kuhakikisha
kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo
ambalo litawasaidia waweze kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi.