Mgomo wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lutheran junior Seminary
inayomilikiwa na kanisa la kilutheri Tanzania umeingia siku ya pili
baada ya wanafunzi kugoma kutwa nzima kuingia madarasani na kuandamana
katika barabara ya Morogoro Dar es Salaam na kulazimu jeshi la polisi
kuingilia kati kuzuia maandamano.
Wanafunzi hao wamesikika wakiimba
wanataka kuonana na askofu mkuu wa KKKT Alex Malasusa huku wakiwa na
mabango yenye jumbe mbalimbali ambapo wakiwa njiani katika barabara ya
Morogoro Dar es Salaam jeshi la polisi walisitisha maandamano kwa madai
ya kutofuata taratibu za kuomba kibali.
Wanafunzi hao walilazimika kurudi shuleni kwa
maandamano wakisindikizwa na ulinzi wa jeshi la polisi lakini walipofika
shuleni hapo mambo yalionekana kuwa magumu zaidi
hata hivyo hawakutaka
kusikiliza walimu na ikamlazimu mkuu wa wilaya Saidi Amanzi kufika
shuleni hapo na kuzungumza na uongozi wa shule ambapo amesema
inawalazimu kusubiri viongozi wa KKKT kutoka makao mjini Arusha.
Kwa upande wao wanafunzi wamesema wataendelea na
mgomo huo kutokana na ahadi zilizotolewa kushindwa kutekelezeka na
kushinikiza kutaka kuonana na askofu mkuu Alex Malalasusa ili awasaidie
kutatua kero zao.
CHANZO:ITV