CCM kusimamia mchakato wa Katiba Mpya

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo, amesema kuwa shughuli ya usimamizi na uratibu wa upatikanaji wa Katiba Mpya ya kisasa utasimamiwa na chama hicho na si vinginevyo.


Chongolo ameitoa kauli hiyo hii jana Juni Mosi, 2023, mkoani Iringa wakati akihitimisha ziara yake mkoani humo iliyokuwa na lengo la kukagua utekelezwaji wa ilani ya chama hicho, kuangalia uimara wa chama pamoja na mambo mengine.

"Watu wanapigapiga kelele huko ngoja niwaambie, CCM ndiyo chama kiongozi, na ndiyo chama kitakachoongoza mchakato wa Katiba ya kisasa, iliyoandaliwa kisasa,na itatengenezwa kupitia mikono, uongozi, usimamizi na uratibu wa CCM na si vinginevyo," amesema Chongolo

Aidha Chongolo ameongeza kuwa, "Msidanganyike watu wengi wanataka Katiba kwa maslahi binafsi, wengi ukiangalia hawazungumzii pembejeo za kilimo, usalama wa Watanzania wala miundombinu ya barabara, wao wanataka tume hutu ya uchaguzi, wanataka mambo ambayo yatawapa nafasi ya kwenda kwenye madaraka."


Tyson Nduguru rafiki wa marehemu MC Joe aliyepotea, apatikana

Kijana Tyson Nduguru, Rafiki wa karibu wa Joel Misesemo (MC Joel) aliyejirusha ghorofa ya 7 Makumbusho Dar es salaam na kufariki dunia, ambaye aliripotiwa kutoweka ghafla siku tatu tangu kutokea kwa kifo cha Joel, amepatikana jana June 1 2023.


Mke wa Tyson, Grace Rashid ameithibitisha kwa kusema; “Ni kweli Tyson amepatikana mchana wa leo (jana), mimi nilitoka kama kawaida nilikua naendelea na mizunguko akanipigia simu yeye mwenyewe.

“Nimefika nyumbani nimeshaonana nae ni mzima wa afya, mpaka sasa sijaongea nae lolote Watu wapo wengi tupo na familia, nitawajulisha zaidi baadae."

Ripoti za kutoweka kwa Tyson ziliibua maswali mengi kutokana na ukaribu wa wawili hao pamoja na matukio mawili tofauti yaliyowatokea kwa kupishana siku chache yakiwa na mazingira ya kutatanisha.


Nyama ya Nguruwe yaruhusiwa kwa masharti Ludewa

Baada ya kutolewa katazo la kutumia mazao yatokanayo na mnyama aina ya Nguruwe wilayani Ludewa mkoani Njombe ambalo lilitolewa kwa zaidi ya miezi miwili na nusu iliyopita kwa kile kilichodaiwa ni kutokana na uwepo wa ugonjwa wa homa ya Nguruwe hatimaye mnyama huyo ameweza kupunguziwa masharti ya katazo hilo baada ya kupungua kwa matukio ya ugonjwa huo.


Akizungumza na Wasafi media Afisa Kilimo Mifugo na Uvuvi Festo Mkomba amesema mnyama huyo ameruhusiwa kuchinjwa pamoja na kutumika mazao yake kama nyama, mifupa, nywele, samadi na damu ila hairuhusiwi kutoa mazao hayo nje ya kijiji ambacho mnyama huyo amechinjwa ambapo na kabla ya kuchinjwa kwake anatakiwa kufanyiwa ukaguzi kwa masaa yasiyopungua 48.

Ameongeza kuwa mpaka sasa zaidi ya nguruwe 417 wamekufa kwa ugonjwa huo na wamefanya jitihada za kutosha kuhakikisha ugonjwa huo hauenei zaidi na wamefanikiwa ambapo kwa sasa hakuna nguruwe hata mmoja mwenye ugonjwa.

"Tumekuwa tukioa elimu na kupita kukagua nguruwe katika maeneo mabalimbali ya wilaya hii na tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa huu japo haikuwa rahisi kwakuwa kuna baadhi ya watu wasio waaminifu walikuwa wakichinja kwa siri na kuuza nyama hiyo huku wakiwa wameipa jina la Mbolea ya Ruzuku ili wasigundulike kwa urahisi".

Chanzo:Wasafi media


Mwenyekiti CHADEMA Mbeya afutwa Uanachama

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mbeya vijijini kimetangaza kumfutia uanachama Joseph Mwasote ‘China wa China’ ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya akidaiwa kuwa chanzo cha migogoro ndani ya chama hicho.


Akitangaza maazimio ya Kamati Tendaji ya CHADEMA Mbeya vijijini mwenyekiti wa jimbo hilo Jackson Mwasenga amesema mwanachama wake Joseph Mwasote ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA na makamu Mwenyekiti Kanda ya Nyasa amesema amekuwa chanzo cha migogoro ndani na nje ya jimbo hilo.

Wasema kuwa wamemwita mara kadhaa lakini hakuitikia wito na kwamba amekuwa akizunguka kwenye kata mbalimbali kupanga timu ya kuwapindua viongozi wa jimbo.

“Haijalishi tumekosea au hatujakosea lakini Kamati Tendaji ya Jimbo (Mbeya vijijini) kwa pamoja tumeazimia kumfutia uanachama Joseph Mwasote. Migogoro mingi chanzo ni yeye, kwenye kata huko anazunguka kwa nia yake binafsi anaunda kikundi cha kwenda kuwaondoa viongozi wa jimbo” amesema Jackson Mwasenga, Mkiti CHADEMA Mbeya vijijini.

Hata hivyo bado wako wanachama wanaodaiwa kukamatwa kwa saa kadhaa na Polisi wakidaiwa kutaka kuandamana kwenye ofisi ya jimbo mjini Mbalizi walipofika kutaka kujua hatma ya mwenyekiti wao kuondolewa.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo Joseph Mwasote mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya ameeleza kusikitishwa na maamuzi ya jimbo lakini pia bado hajakabidhiwa barua ya kufutiwa uanachama wake.

“Lakini wameikosea katiba sana (ya CHADEMA). Anayeshikilia uanachama wangu ni Tawi (Isanga-Imezu), anayeshikilia uanachama wangu ni mamlaka yangu ya nidhamu ngazi ya juu. Yaani leo mkuu wa wilaya akamuondoe Mkuu wa Mkoa! ni shida”,” amesema Mwasote.


Tume: Kifo cha mwanafunzi UDOM hakina uhusiano na ajali ya Naibu Waziri

Tume ya Haki za Binadamu (THBUB) imetoa matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nusura Abdallah, huku ikidai hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya Naibu Waziri Dk Festo Dugange iliyotokea Aprili 25 kuamkia 26 mwaka huu.


Akizungumza na Waandishi wa Habari, leo Juni 2, 2023, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amesema walitembelea mikoa ya Dodoma, Singida na Kilimanjaro na kwamba matokeo yanaonyesha kuwa kifo cha Nusura kilisababishwa na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

Kwa mujibu wa Jaji Mwaimu, katika uchunguzi wa tume hiyo, wamegundua kuwa Mei mosi mwaka huu marehemu aliandaa chakula cha jioni nyumbani kwa mpenzi wake Juma Kundya mjini Moshi ambacho alikula yeye, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake.

Hata hivyo baada ya kumaliza kula, marehemu Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu, hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu.

Jaji Mwaimu ameongeza kusema kuwa, pamoja na jitihada na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na madaktari wa hospitali hiyo, Nusura alifariki majira ya saa 5 usiku Mei mosi mwaka huu.

Mwenyekiti huyo amesema vipimo vilivyofanywa na hospitali hiyo vilionesha kifo cha Nusura kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

"Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya maziko na kuuona mwili huo kabla ya maziko walithibitisha haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha," amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema mabaki ya chakula walichokula marehemu, mchumba wake na mpwa wake na matapishi yaliwasilishwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi na taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili yoyote ya kuwepo kwa sumu.

Pia, Mwenyekiti huyo amesema Tume imebaini kifo cha Nusura hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya Naibu Waziri Dk Festo Dugange iliyotokea Aprili 25 kuamkia 26 2023.

"THBUB haikuweza kudhibitisha mtu yoyote kuhusika na kifo cha marehemu kutokana na vielelezo vya Hospitali, Mkemia Mkuu wa Serikali na maelezo mengine ya mashahidi," amesema Mwenyekiti huyo.

Nusura, alifariki dunia Mei mosi katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro, huku mazingira ya kifo hicho yakizua utata baada ya kuhusishwa na ajali iliyotokea Dodoma, ikimhusisha pia Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange.

Marehemu Nusura alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii.


Mwanaume aomba mahakama ivunje ndoa yake kutokana na uzuri wa mkewe

Mwanaume mwenye umri wa miaka 40 kutoka nchini Zambia, Arnold Masuka, ameiomba mahakama kuvunja ndoa yake kutokana na urembo wa kipekee alionao mke wake.


Masuka aliwashangaza viongozi na mashahidi katika mahakama ya mji mkuu wa Lusaka wakati alipomwambia hakimu kwamba urembo wa mkewe, Hilda Mleya umemfanya kukosa usingizi mara kadhaa.


Mzaliwa huyo wa Lusaka ameongeza kuwa amekuwa akiishi kwa hofu kwa muda mrefu ya kumpoteza mke wake kwa mwanamume mwingine, na hata anahofia kumuacha mke wake nyumbani peke yake anapotaka kwenda kazini kwa kuogopa huenda akashawishiwa na wanaume wengine.


Mwanaume huyo amemtaja mke wake, Hilda anayetokea Gokwe nchini Zimbabwe, kuwa ndiye mwanamke mrembo zaidi aliyewahi kukutana naye.


Katika mazungumzo na wanahabari baada ya kesi hiyo, Karani wa mahakama hiyo, Chenjerai Chireya amekiri kwamba hajawahi kushuhudia tukio kama hilo mahakamani katika miaka yake yote ya utumishi.Wajawazito 2000 washiriki mbio za Mamathon Korogwe

Na David John, Tanga

WANAWAKE wajawazito zaidi ya 2000 wilayani Korogwe mkoani Tanga  wameshiriki katika mbio za Mamathon ambazo zimefanyika kwa mara ya kwanza wilayani humo zilizoandaliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo.


Lengo la kufanyika kwa Mamathon ni kutoa hamasa kwa wanawake wajawazito kujifungua salama na hatimaye kupunguza vifo vya mama na mtoto kama ambavyo Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Akizungumza mbele ya wanawake hao,  wananchi pamoja na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Korogwe , Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Mary Chatanda aliyekuwa mgeni rasmi amempongeza Jokate kwa ubunifu huo.

“Tunakupongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kote alikopita amekuwa akifanya kazi nzuri hivyo wananchi wa Wilaya ya Korogwe wajue wamepata jembe na ndio maana Rais Dkt Samia Hassan Suluhu ameendeea kumteua katika nafasi hiyo ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe .

“Wananchi wa Korogwe mmepata jembe na muendelee kumpa ushirikiano na sisi viongozi tutaendelea kumuunga mkono na katika hili la ambalo ameliazisha aendelee nalo kwani linagusa maisha ya wamama wajawazito na watoto moja kwa moja kulinda afya zao, ” amesema Chatanda.

Pia amewataka wananchi wa Korogwe kumtumia Mkuu wa Wilaya hiyo kwani ana mambo mazuri yatakayowezesha kuwaletea maendeleo na wao kama viongozi wa Chama na Serikali watatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anatekeleza majukumu yake vizuri.

Akifafanua kuhusu mbio za Mamathon amesema ni jambo jipya katika Wilaya ya Korogwe na Jokate ameonesha  ubunifu mkubwa,  hivyo anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mkuu huyo wa Wilaya kwani mambo yamekuwa moto.

amewapongeza wanawake wajawazito pamoja na wote walioshiriki na kumaliza mbio hizo kwani kufanya mazoezi kwa mjazito kuna faida nyingi.”Kupitia mbio hizi kuna mama mjamzito mmoja amepelekwa hospitali na tunamuombea ajifungue salama.”

Amewataka kuhakikisha baada ya mbio hizo wanaendelea kushiriki mazoezi ,kuzingatia lishe Bora kipindi chote cha ujauzito wao jambo litakalosaidia  kujifungua salama na kuwezesha mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Pamoja na mambo mengine Chatanda amesema mbali ya mbio hizo,  amepokea vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Korogwe na hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuboresha huduma za afya ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

“Kuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt Samia Kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya afya na kwa kipindi cha miaka miwili kwa nchi nzima ameboresha  miundombinu kwenye sekta ya afya katika ngazi zote za Zahanati ,vituo vya afya ,Hospitali za Wilaya , na kungineko na kupeleka vifaa tiba Kwa ajili ya kutolea huduma za afya.” 

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wahudumu katika vituo vya afya Zahanati ,na Hospitali zote kuzingatia maadili ya kazi zao, na kuepuka na vitendo vinavyokwenda  kinyume na maadili ya kazi wanayoifanya huko akitolea mfano vitendo vilivyojitokeza wilayani Kaliua mkoani Tabora na anashukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora Baltida Burhan kwa kuchukua hatua.Mapacha wanachuo wafariki wakiogelea Ziwa Victoria

Kenny na Lenny Makomonde (24), mapacha na wanafunzi wa Chuo cha Mipango Kampasi ya Mwanza wamefariki dunia kwa kuzama majini walipokuwa wakiogelea ndani ya Ziwa Victoria.


Tukio hilo lililoacha simanzi na vilio miongoni mwa wanafunzi wa chuo hicho, ndugu, jamaa na marafiki limetokea jioni ya Mei 28, 2023 wakati wawili hao walipokuwa wakiogelea kwenye ufukwe wa Mihama Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Miili ya mapacha hao wanaosemekana kuwa na ujuzi na uzoefu wa kuogelea tayari imepatikana na kuopolewa kutoka majini na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakishirikiana na wananchi.

Mkuu wa Jeshi la Zima Moto Wilaya ya Ilemela, Insekta Deusdedith Rutta amesema taarifa za mapacha hao waliokuwa wanasoma kozi ya Mipango na Maendeleo kuzama maji ziliifikia Jeshi hilo Saa 1:00 usiku jana Mei 28, 2023.

‘’Juhudi za uokoaji zilishindikana kutokana na kiwazo cha giza,’’ amesema Inspekta Rutta

Amesema askari wa Zimamoto na Uokoaji walirejea eneo la tukio leo alfajiri kuendelea na uokoaji na kufanikiwa kuopoa miili ya mapacha hao Saa 5:00 asubuhi.


Makamba: Msituhukumu, tupeni muda miradi ikamilike

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema takribani nusu ya miradi ya kimkakati iliyoainishwa na serikali ipo kwenye sekta ya nishati.


January amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini na kuwapa jukumu hilo na akasema hata utamaduni wa kazi katika wizara hiyo umebadilika. 

Alisema hayo baada ya kujibu maswali katika programu ya mjadala katika Clubhouse ya Msemaji Mkuu wa Serikali.

“Sisi tunachoomba ni muda na subira kwa sababu kazi hizi matokeo yake yanachukua muda kupatikana na hukumu ya kazi tunayoifanya sasa tungeomba itolewe mbele kidogo na sio sasa,” alisema.

January alisema miaka ya nyuma wizara hiyo ilikuwa na sifa mbaya ya rushwa, mikataba mibaya lakini sasa wizara hiyo na taasisi zake wana mipango mahususi kuhakikisha wanazingatia maadili.

Alisema takribani kila siku kuna zabuni inatolewa katika wizara hiyo na takribani watu 30 wanazikosa zabuni hizo kila siku hivyo wanaokosa wanakuwa na hisia kwamba waliopata hawakupata kihalali.


Wazika maiti si yao, wafukua na kuzika upya

Ukistaajabu ya Musa, utayaona ya firauni. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya ndugu wa familia ya marehemu Gudluck Munuo (53), mkazi wa Kijiji cha Mese, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, kuchukua maiti ya mtu mwingine iliyokuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Kibong'oto na kwenda kuzika.


Tukio hilo limezua taharuki, lilitokea Mei 26, mwaka huu wakati ndugu hao bila kujua, walichukua maiti ya Eliudi Mbaga (68) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Matadi.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu Mmbaga walipoenda kuchukua mwili katika hospitali hiyo ya Kibong'oto walikuta mwili wa ndugu yao haupo ndipo walipofuatilia kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo na kubaini umeenda kuzikwa katika Kijiji cha Mese.

Baada ya kufanya taratibu zinazotakiwa Mei 26, mwili huo ulifukuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu Mbaga na ulizikwa siku hiyo hiyo. Mwananchi lilifanikiwa kuzungumza na Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka alikiri kuwapo kwa tukio hilo na ndugu wameshachukua miili ya ndugu zao na kwenda kuizika.” alisema

Akisimulia mkasa huo, mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mese, Alex Munuo alisema changamoto iliyojitokeza ni kwa waliopeleka maiti hospitali si waliokwenda.

"Hili tukio kweli limezua taharuki kidogo hapa kijijini maana ni tukio la kushangaza, mimi ndiye niliyepeleka mwili wa Gudluck Munuo hospitali lakini siku ya kwenda kuchukua mwili sikwenda mimi walienda ndugu wengine," alisema.

“Muda ambao tunaaga mwili wa marehemu baada ya kufikishwa hapa nyumbani kwake tuliingiwa na wasiwasi kidogo kama vile mwili ulikuwa umebadilika, tukajiuliza mbona kama sio yeye, tuliitana pembeni lakini tuliona labda kwa kuwa mwili ulikuwa mochwari ulibadilika rangi, hivyo tuliamua kuzika, lakini baadaye ndio ikaja kubainika si yeye, tukalazimika kufukua Mei 26 na kuukabidhi kwa wahusika na sisi tukachukua mwili wetu tukazika siku ileile."

Akisumulia namna walivyoenda kuchukua mwili hospitalini na kuukosa, ndugu wa familia ya Mmbaga, Kiloliki Mbaga alisema walipofika hospitali mwili wa ndugu yao wahudumu waliwaongozana kwenda chumba cha maiti na walishangaa walipofungua sanduku walikuta maiti siyo yao.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Matadi wilayani humo, Asanterabi Ng'unda alitaka umakini uwepo kwa wanaokwenda mochwari kuchukua miili ya wapendwa wao


Awekewa chumvi kwenye tenki la pikipiki yake, Kisa anakemea Wizi

Kijana aliyetambulika kwa jina la George Mahundi mkazi wa kijiji cha Kiyogo kata ya Masasi Wilayani Ludewa Mkoani Njombe, amedai kuwekewa chumvi kwenye tanki pamoja na Injini ya pikipiki yake kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kukemea matukio ya wizi kijijini hapo.


Akitoa malalamiko ya tukio hilo mbele ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo Deogratius Massawe amesema hivi karibuni walikuwa na mkutano wa kijiji ambapo waliwapigia kura watu wanaohisiwa kuwa na tabia hizo za wizi hivyo kutokana na yeye kuwa muwazi katika kuwafichua wezi hao kumepelekea kukumbwa na maswahibu hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ludewa Deogratius Massawe amewataka wale wote waliopigiwa kura za kuhusika na matukio ya wizi kufika katika kituo cha Polisi cha Wilaya hiyo ili kufanyiwa mahojiano huku Diwani wa kata ya Masasi Daniel Mhagama akiwaasa wananchi kufuata maelekezo waliyopewa.


Msimamo wa CCM kuhusu Elimu ya Tanzania

 


Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo ameeleza wazi Msimamo wa Chama hicho katika Sekta ya Elimu, kwa kubainisha kuwa maono ya CCM ni kuona Tanzania kama Taifa linakuwa na mitaala ambayo itatoa Elimu ya Taaluma ya Kujiajiri kuliko Kutegemea Ajira kwa Sekta ya Umma ama Binafsi.


Chongolo amebainisha Msimamo huo Leo Mei 28, 2023 alipokuwa akizungumza na Wananchi pamoja na Wana CCM katika Kata ya Malangali ambayo ipo katika Jimbo la Mufindi kusini mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 7 mkoani humo ikilenga kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020/2025 pamoja na Kuzungumza na Makundi mbalimbali ya Kijamii.

Amesema tayari Mwenyekiti wa Chama hicho ambae ni Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatoa idhini kwa kamati ambayo imekabidhiwa Jukumu la kupitia na kuangalia Upya mfumo wa Elimu ili kuja na mapendekezo ya Mitaala itakayokidhi soko la Ajira katika Muktadha wa Kujiajiri baada ya kumaliza masomo kuliko kutegemea Ajira Pekee.

Aidha Katibu mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo, amesema Serikali imeweza kutatua Changamoto ya pembejeo kwa Wakulima, ikiwemo suala la mbolea ambapo kwa imeweka ruzuku na hivyo kufanya bei kushuka na hivyo wakulima wengi kumudu kununua.

"Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kushughulikia upatikanaji wa Pembejeo kwa njia ya haraka Urahisi, ambapo kazi kubwa iliyobaki kwa Wakulima ni kuendelea na kilimo chenye tija kwa kuwa Changamoto zingine kwenye Sekta ya Kilimo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi wa Kudumu" amesema Chongolo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Ndugu Daud Yasin (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini (CCM) Ndugu David Mwakiposa Kihenzile pamoja na Viongozi na wanachama wengine wakitembea kwa miguu kuelekea Nyololo kuhudhuria kikao cha shina namba 27, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku 7 mkoani Iringa .

Katibu Mkuu ameongozana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi Gavu na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema.Polisi: Kifungu cha sheria ya uchawi kipo na watu hupewa hukumu

Watu wengi wamekuwa wakiamini kuwa serikali haiamini uchawi na hakuna sheria inayombana mtu katika masuala hayo, lakini ukweli ni kwamba kifungu cha sheria ya uchawi kipo na watu hupewa hukumu pale wanapobainika kuhusika na masuala hayo.


Deogratius Massawe ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe amefika katika kijiji cha Kiyogo kilichopo katika kata ya Masasi na kutoa elimu hiyo katika mkutano wa hadhara baada ya hivi karibuni kijijini hapo kutokea tukio la baba mmoja aliyefahamika kwa jina la Lucas Mahundi kupigwa na kujeruhiwa na watoto wake wakimtuhumu kumuua mama yao kichawi kwa kutumia mamba.


Kwa upande wa Lucas Mahundi ambaye ndiye aliyejeruhiwa na watoto wake hao amesema kujeruhiwa kwake hakuhusiani na tuhuma za uchawi lakini wananchi wenzake walipinga kauli hiyo na kumtaka kuwa muwazi huku wengine wakieleza namna ambavyo wachawi hutumia mamba kuondoa uhai wao.


Adaiwa Kumuua Babake, Aupika na Kuula Mwili Wake

 


Mwanaume kutoka kijiji cha Giankaja, kaunti ya Tharaka Nithi NCHINI Kenya alitiwa mbaroni baada ya kudaiwa kumuua baba yake na kupika sehemu za mwili wake.


Mwanamume huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi kaunti ya Tharaka Nithi.


Polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha wakisema mwathiriwa ambaye ni mzee mwenye umri wa miaka 70, aliripotiwa kutoweka kwa siku tatu. Msako ulifanyika katika kijiji kizima na wakazi wa eneo hilo katika juhudi za kumtafuta mzee huyo.


Baada ya saa kadhaa za msakao, upekuzi wao uliwaelekeza kwenye mtaro wenye kina kirefu ambapo waliupata mwili wa marehemu ambao tayari ulikuwa umeshaanza kuoza. Marehemu alikuwa amekatwa kichwa na sehemu za mwili wake kukatwa na miguu yake ikiwa kando ya mwili wake. 


Walikimbia haraka kwa chifu wa eneo hilo ili kumjulisha kuwa wamempata mtu aliyepotea. Hata hivyo, waliporejea kwenye mtaro, mwili huo haukuonekana.


Wakiwa wamechanganyikiwa na jinsi mambo yalivyobadilika, wenyeji hao katika udadisi wao pamoja na polisi na chifu walitafuta ndani zaidi ya mtaro. Walizunguka kwenye mtaro wa kina kirefu uliowaelekeza kwenye nyumba ambayo polisi wanasema huenda ilikuwa ya mshukiwa. Walipofika katika nyumba hiyo, walishangaa kupata chungu cha kupikia kimejaa nyama na mboga. 


Katika eneo la tukio, kulikuwa na fuvu la kichwa cha binadamu na nguo zilizojaa damu pamoja na viatu vya marehemu. Polisi walimhoji mshukiwa huyo kuhusu aliko baba yake lakini alibaini kuwa pia alikuwa hafahamu kwa kuwa anaendelea kumtafuta.


Sehemu nyingine za mwili zilizopotea ambazo ziligunduliwa kwanza na wenyeji zilipatikana zikiwa zimetupwa kwenye gunia na kufunikwa kwa mawe ndani ya Mto Nithi. 


Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye alidai kuwa mshukiwa huyo alianza kuchimba mtaro huo mwaka 2017, alieleza kuwa mshukiwa na mwathiriwa wake walizozana kuhusu hali ya mtaro huo kabla ya kupotea. "Wawili hao walizozana baada ya mwanamume huyo kumzuia babake kukata nyasi za Napier kuzunguka mtaro," Johnson Mutembei mkazi aliambia jarida moja la eneo hilo.


Kwa sasa mshukiwa yuko rumande akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.


Chanzo: TUKO.co.ke Kichwa chazikwa baada ya mwili kuliwa na mamba

Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limetoa taarifa ya mwanamke mkazi wa kijiji cha Nachui Kata ya Nyengedi Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi akidaiwa kufariki dunia baada ya kuliwa na mamba katika mto lukuredi.


Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Alhaji Salim Kabaleke ambaye amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Mei 24, 2023 katika mto Lukuledi uliopo Kijiji cha Nachui.

Alisema kuwa mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Somoe Saidi (65) alienda kuoga katika mto huo na kuchota maji ndipo alipokumbwa na madhira hayo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo inasemekana kuwa siku ya tukio mama huyo alikwenda mtoni kwa ajili ya kukoga na kuchota maji lakini baada ya muda kupita wanakijiji wengine walikwenda mtoni ndipo wakakuta ndoo ya maji pamoja na nguo pembezoni mwa mto huo bila kuwapo na mtu hali ambayo iliwapa mashaka kwakuwa waliona michirizi ya damu pembezoni mwa mto.

ACP Kabeleke alisema kuwa mwili wa marehemu ulipatikana siku ya tatu baadaye baada ya kufanya msako kwa kushirikiana na askari wa maliasili huku mwili wake ukiwa umeliwa na mamba na kusalia kichwa pekee.

"Jeshi la Polisi limewataka wakazi wanaoishi na kufanya shughuli zao karibu na mto Lukuledi kuwa makini na mamba huku akiwaomba kushirikiana na watu wa maliasili ili kutambua maeneo hatarishi"


 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo