Jessica Ngassa akimuhudumia mumewe, Jackson Ngassa ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Idara ya Usambazaji wa Magazeti aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi na majambazi Jumamosi usiku jijini Dar es Salaam.
Watu ambao wanasadikiwa kuwa ni
majambazi wamemjeruhi kwa risasi mfanyakazi wa Idara ya Usambazaji ya
Mwananchi Communications Limited, Jackson Ngassa.
Tukio hilo lilitokea juzi Jumamosi saa 4 usiku
eneo la Tabata Matumbi baada ya watu hao kumfuatilia Ngassa tangu
alipokuwa anatoka ofisi za Mwananchi eneo la Tabata Relini.
Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Taasisi ya Mifupa (Moi), Ngassa alisema wakati akitoka ofisini siku hiyo
aliona pikipiki tatu zikiwa nyuma yake lakini hakuhisi kama zilikuwa
zinamfuata mpaka walipofika taa za kuongozea magari za Tabata Dampo.
“Nilipofika Tabata Dampo nilihisi kufuatiliwa kwa
sababu kila nilipopunguza mwendo nao walipunguza mpaka nilipofika
Matumbi ndipo nikasikia wakiniambia simama haraka na kisha wakapiga
risasi moja ambayo ilitoboa tanki la mafuta la pikikipiki,” alisema
Ngassa.
Alisema baada ya kuona hivyo akataka kukimbilia
Benki ya Access iliyoko eneo hilo la Matumbi lakini kabla hajafanya
hivyo pikipiki nyingine ilimzuia kwa mbele na ghafla akasikia risasi
ambayo ilipasua sehemu ya goti mguu wake wa kulia.
Hata hivyo, Ngassa alisema begi hilo halikuwa na
pesa zozote zaidi ya kadi ya benki na magari ya kuchezea watoto
aliyowanunulia watoto wake
Kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa
upasuaji mdogo wa kuunganisha mifupa iliyovunjika kwani risasi
aliyopigwa iliingia na kutoka upande wa pili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari alikwishamtembelea
majeruhi katika hospitali ya Muhimbili alikolazwa