Wanafunzi 1555 wa Msingi na 7457 wa Sekondari Wapata Mimba

Serikali imesema katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 Wanafunzi wa Shule za Msingi waliopata ujauzito ni 1,554 na Sekondari ni 7,457.


Hadi kufikia mwezi January, 2023 Wanafunzi waliorejea Shuleni baada ya kukatiza masomo kwasababu ya ujauzito na kuendelea na masomo ya Elimu ya Sekondari ni 1,692.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo January 31, 2023 na Naibu Waziri wa Elimu Omary Kipanga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mchafu Chakoma aliyetaka kujua ni Wanafunzi wangapi waliokuwa wajawazito na wangapi wamerejeshwa Shuleni baada ya agizo la Rais.

Aidha Omary Kipanga amesema kwa upande wa Elimu ya Msingi Serikali inaendelea kukusanya taarifa za Wanafunzi waliorejea Shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito.


Atangaza kuuza Nguo za ndani za mume na mke baada ya kukataa kulipa kodi ya nyumba


Tangazo la madalali wa kupiga mnada mali zilizopigwa tanji katika kaunti ya Kisumu limezua vichekesho vikubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kampuni moja ya madalali kwa jina Nyaluoyo kutangaza kupiga mnada vitu mbalimbali kwa nyumba ya mpangaji mmoja aliyekwama kulipa kodi ya nyumba hiyo.


Madalali hao wa Nyaluoyo waliweka tangazo la kupiga mnada mali hiyo kwenye gazeti la Jumatatu Januari 30, 2023. Baadhi ya mali ambayo madalali hao walitangaza kupiga mnada ni pamoja na chupi za mwanamume na mwanamke waliokuwa wamepangisha katika nyumba hiyo.


Nyaluooyo walitoa wito kwa umma kujitokeza ili kuweka maombi yao ili kuuziwa chupi hizo, zikiwemo 4 za mwanamume, 4 za mwanamke, mabegi mawili ya watoto, miongoni mwa vitu vingine.


Tangazo hilo lilikuwa linasema kuwa ni mzozo uliokuwa kati ya mmiliki wa nyumba na mpangaji wake kwa jina Zacharia Sichenje Masika.


Yeyote ambaye alitaka kuuziwa mali hiyo iliyopigwa tanji kutoka kwa mpangaji mkaidi alitaarifiwa kujitokeza katika ofisi za kampuni hiyo ya madalali mnamo Februari 7 saa tano asubuhi katika kaunti ya Kisumu.


Tangazo hilo lilionekana kwenye jarida moja la Jumatatu na wengi walilitupia vijembe kwa utani mwingi, wakisema kuwa hiyo ilikuwa kama njia moja ya kumdhalilisha mpangaji huyo na familia yake kwani hakuna mtu anayeweza kujitokeza kununua chupi zilizotumiwa wakati mpya sokoni huuzwa hadi kwa bei ya jioni ya shilingi mia tu.


Inasemekana kuwa mpangaji huyo alikuwa amekodisha chumba kimoja jijini Kisumu ambapo alikuwa anakitumia kama duka la kuuza nguo na malimbikizi ya kodi ya kila mwezi yalikuwa yamefikia laki moja na elfu ishirini ambayo alishindwa kulipa na mali yake yakapigwa tanjia alipofungiwa nje.

Chanzo;Radiojambo



Afiwa na Mke Siku 11 baada ya Harusi Yao

 


Mwanaume kwa jina la Twitter Idris Almustapha Daja (@almustapherr) ameibua hisia na taarifa za kifo cha ghafla cha mkewe mpya.


Kulingana na Daja, marehemu mkewe aliaga dunia siku 11 baada ya kufunga pingu za maisha katika sherehe ya maridadi.. Mwanamume aliyevunjika moyo alishiriki picha za harusi yao, ambapo alipiga naye ili kunasa wakati maalum ambapo rasmi alikuwa akiitwa mume. Jinsi Idris Almustapha Daja alivyonukuu picha za hisia.


''Innalillahi Wa'inna'ilaihi Raju'un. Nilimpoteza siku 11 baada ya harusi yetu. Tarehe 6 Januari 2023- 17 Januari 2023,'' alinukuu chapisho hilo. Wanandoa hao walipiga picha za kitamaduni kwa hafla yao. Walionekana maridadi kweli kweli. Zaidi ya watu 4,000 wameomboleza na Daja, huku wengi wakishiriki jumbe za kumpa pole kutokana na kifo cha marehemu mpendwa wake. 



Afia gesti akiwa na mwanamke wake

Mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 25, alipatikana amefariki katika chumba cha hoteli alichokuwa amekodisha kumumunya urojo na mpenziwe.


Ali Musstafa anaripotiwa kuanguka na kukata roho katika Hoteli ya Avenue Lodge mjini Arua, Uganda kutokana na kushindwa kupumua alikokuwa akirusha roho na mpenzi wake. “Mwathiriwa alianguka na kufia chumbani. Mpenziwe alienda na kuwajulisha wasimamizi wa hoteli ambao mara moja walitoa taarifa kwa polisi wa Arua. Eneo la tukio lilikaguliwa na kuhifadhiwa vizuri," ilisoma ripoti ya polisi.


Polisi katika Wilaya ya Arua eneo la Nile Magharibi walisema hawakupata dalili zozote za sumu, dawa za kulevya au athari zingine za mwili kutoka eneo la tukio.


"Hakuna chembechembe za matumizi mabaya ya dawa za kulevya, sumu au athari zingine za mwili zilizopatikana katika eneo la tukio. Mwili huo ulipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Arua na kuchunguzwa,” msemaji wa polisi, SCP Fred Enanga alisema Jumatatu, kama alivyonukuliwa na Daily Monitor. Enanga anaamini kuwa mfanyabiashara huyo kutoka OZU, wadi ya Kenya katika Wilaya ya Arua alifariki dunia mwendo wa saa tatu usiku. Mwili wa marehemu baadaye ulichukuliwa kutoka chumba cha hoteli na kupelekwa kufanyiwa uchunguzi wa maiti. "Kifo wakati wa kujamiana kinaweza kutokea kwa sababu kadhaa, ambazo ni pamoja na mkazo wa mwili kutokana na shughuli hiyo au kwa sababu ya hali isiyo ya kawaida ," aliongeza.


Katika tukio sawia na hilo, siku tatu zilizopita mzee wa miaka 71, alipatikana amefariki kwenye gesti baada ya kurushana na mpenziwe mwenye umri wa miaka 22. Kulingana na uchunguzi wa polisi, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 22, alichukuliwa kutoka Githurai na mzee huyo kabla ya kuelekea kwenye gesti. Wakiwa katika hali ya kujamiana, mwanamume huyo alisemekana kuanza kulalamika kuhusu matatizo kadhaa ya kiafya. Alikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambapo alithibitishwa kufariki baada ya kuwasili.


Chanzo: TUKO.co.ke



Aliyesombwa na mto Lindi akutwa kichwa na mifupa pekee


Mwili wa Mwanahawa Abdallah (65), mkulima na mkazi wa Kijiji na Kata ya Kiwalala, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi aliyepotea wiki iliyopita kwa kusombwa na maji kwenye Mto Lukuledi, umeonekana ukiwa umebaki kichwa na mifupa baada ya kuliwa na wanyama.


Kwa mujibu wa mashuhuda walioshiriki kumtafuta mama huyo, mwili wake ulikutwa pembezoni mwa mto huo Januari 24, mwaka huu, majira ya saa saba mchana ukiwa hauna ngozi wala nyama isipokuwa kichwani.

Wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, baadhi ya mashuhuda hao walioshiriki kumtafuta mwanakijiji mwenzao huyo, wakiwamo Semi Dume, Issa Selemani, Paulo Daniel na Ibrahim Mkonogile, walidai kuwa mwili wa Mwanahawa ulikutwa ukiwa umebaki kichwa na mifupa kutokana na nyama yote kuliwa na wanyama waliokuwapo majini.

"Tulichokikuta na kubaini ni yule mama ni kichwa chake, lakini nyama yote ya mwili wake imeliwa na kubaki mifupa mitupu," alidai Daniel.

Washiriki walimtafuta mama huyo kwa siku nne mfululizo tangu aliporipotiwa kusombwa na maji Januari 20, mwaka huu.

Walidai kuwa kulingana na hali na mazingira yalivyokuwa, familia ya marehemu, hasa watoto wake, waliamua mabaki ya mifupa na kichwa kilichokutwa pembeni mwa mto, yazikwe hukohuko mtoni badala ya kupelekwa nyumbani kwa maziko.

"Mifupa tuliyoikuta ni ya mikono na miguu pekee. Kichwa kilikuwa na ngozi na nywele zake," alidai Mkonogile.

Rashidi Mega, Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kiwalala na mtoto wa tatu wa marehemu, walikiri kuonekana kwa mabaki ya mwili wa mama huyo na kuamua yazikwe hukohuko kando ya mto kutokana na mazingira waliyoyakuta.

“Ilikuwa vigumu kufikisha nyumbani mabaki yale, hivyo tukaamua kuyazika hukohuko," alisema Mega.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwalala, Zaituni Chilinga, alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia tukio hilo, alikiri mabaki ya mifupa ya mwili wa mwanakijiji huyo kupatikana.

Iliripotiwa na wanakijiji hao Januari 20, mwaka huu kwamba, siku hiyo majira ya saa nane mchana, Mwanahawa, akiwa ameongozana na jirani yake, Fatu Dadi wakitokea shambani kurejea nyumbani kwao, walipofika Mto Lukuledi, aliamua kuoga ndipo maji yaliyokuwa yanatiririka mtoni yakamchukua na kumpeleka eneo alilokutwa ameshafariki dunia.

Chanzo:Nipashe


Mwili wa mtoto mchanga wakutwa shambani bila kichwa


Wakazi wa kijiji cha Gacuku katika kaunti ya Embu walipigwa na butwaa baada ya kukuta mwili wa mtoto mchanga ukiwa bila kichwa umetupwa shambani.


Mwili huo ulipatwa na mwanamke mmoja ambaye alikuwa shambani mwake akivuna maharagwe alipoukanyaga ghalfa na kuita watu

Wanakijiji hao walisema kwa mshangao kuwa hawajawahi shuhudia tukio la kustaajabisha kama hilo, huku wakisema mwili huo ulikuwa na dalili za kukatwa na mtu wala si kuliwa na wanyama kama ambavyo ingesemekana.

Mkuu wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Embu Mashariki Bw Emmanuel Okanda alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusu kisa hicho.

“Tumeanza uchunguzi wa tukio hilo na tunatoa wito kwa wanakijiji kutusaidia kumfichua muuaji,” alinukuliwa na jarida moja la humu nchini.

Bw Okanda alisema maafisa wa upelelezi walikuwa wakishughulikia suala hilo kwa uzito unaostahili na hakuna jiwe litakaloachwa bila kugeuzwa.

"Hili ni suala zito na hatutapumzika hadi mhalifu atambuliwe na kufikishwa mahakamani," alisema Bw Okanda.

Tukio hilo linajiri wiki mbili tu baada ya tukio sawia kuripotiwa katika eneo la Loitoktok kaunti ya Kajiado ambapo mwili wa mtoto wa gredi 6 ulipatikana umefungwa ndani ya gunia.

Mtoto huyo alisemekana kung’olewa macho, kuvunjwa mguu mmoja na sehemu zake za siri zilikuwa zimeharibiwa vibaya sana dalili kuwa wauaji huenda walimbaka kabla ya kumuua na kufunga mwili wake ndani ya gunia kabla ya kuutupa shambani.

Alisema mwili huo umepelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Embu huku msako wa kichwa hicho ukiendelea.


Watu watano wafariki kwa kunywa dawa ya kuacha pombe

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Hassan Ngoma amesema Watu watano wamefariki dunia katika Kijiji cha Nambilanje Wilayani Ruangwa, Lindi baada ya kunywa dawa waliyopewa na Mganga wa tiba asili, Shigela Malehe(39), ili iwasaidie kuacha pombe.



DC Ngoma amesema; “Wamefariki walipopewa dawa ya kuwafanya waache pombe, tumefika eneo la tukio ni mashambani mbali kabisa na Kijiji kama KM 10 hivi, kuna Mtu anaitwa Shabani Macheni alitembelewa na Rafiki yake Mfugaji wa Kabila la Kisukuma anayeitwa Shigela akamwambia ana dawa ya kuacha pombe, Shabani na wenzake wakakubali kunywa”

"Mganga alikuwa na kidumu na kikombe akawaambia masharti unasimama kwenye kizingiti cha mgongo unaupa mgongo mlango unakunywa dawa unaondoka kisha akawaambia waende Mtoni kwa maana watatapika na kuhara na yeye akawafuata baadaye kule hali ikawa mbaya Mganga akarudi akamwambia Mke wa Shabani pika uji walipofika kule Shabani akawa tayari amefariki”

"Wakarudi tena akamwambia Mke wa Shabani ampe ngano wawape wapunguze kuhara, waliporudi wote wakawa wamefariki, waliofariki ni Shaban Machenn(52), Omari Libungu (48), Mikidadi Chilika (42), Mohamedi Juma (41) na Maulidi Alli (40).

"Mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi na vielelezo vimechukuliwa kutoka kwenye miili ya marehemu ili kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kufahamu nini kimewaua, wito wangu kwa Wananchi wajiepushe kutumia tiba za asili ambazo hazijathibitishwa na ikitokea Mganga wa tiba asili anayekutibu amethibitishwa basi kama ni dawa mwambie na yeye aijaribu kwanza ili kujua kama sio sumu.”


DC mteule ambaye hakujitokeza kuapishwa ahojiwa kwa dakika 50

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japheth Maganga amesema kwa sasa hawezi kutoa sababu kwanini hajaripoti wilaya aliyopangiwa ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera huku akihojiwa na Jeshi la Polisi, mkoani Tanga.


Waliomhoji Maganga ni Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga wakitumia zaidi ya dakika 50. 

Bado Polisi hawajaweka wazi sababu za mahojiano hayo.

Maganga na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa wiki iliyopita na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya lakini wakati wenzao wakiapishwa kwenye maeneo yao leo Jumatatu, Januari 30, 2023 wao wapo jijini Tanga wakiongoza mkutano wa viongozi wakuu wa CWT.

Ulaya aliteuliwa kuwa DC wa Mbogwe, Mkoa wa Geita ambapo wenzake wanaapishwa leo Jumatatu na Mkuu wa Mkoa huo, Martin Shigela.

Mara baada ya kumaliza kuhojiwa na polisi kuanzia saa 4:36 hadi saa 5:24 asubuhi  nje ya ukumbi wa mkutano huo unaofanyikia Hoteli ya Regal Naivera, Mtaa wa Bombo jijini Tanga alirejea ukumbini na baadaye kidogo alitoka nje.

Nje ya ukumbi ambapo Mwananchi Digital limeweka kambi lilizungumza na Magamba ambaye amesema, “kwa sasa nimeziba mdomo labda usubiri tutakapomaliza kikao ndipo nitazungumza kuhusu nafasi ya U-DC na CWT."

Wakati Maganga akisema hayo, Rais wa CWT hakuweza kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano huo huku maofisa wa CWT wakisema hajaruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Kitendo cha viongozi wakuu hao wa CWT kuonekana Tanga wakati wenzao wakiapishwa kimezua mjadala maeneo mbalimbali ikiwemo mitandaoni na kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba wameomba wateuliwe wengine kwenye nafasi hizo za U-DC ili kuwawezesha wao kuendelea na majukumu yao ya CWT.

Chanzo: Mwananchi Digital


Mwenyekiti Chadema Mikumi atimkia CCM

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mikumi, Bakari Hasani amekihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema ameridhika na kazi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na ameamua kumuunga mkono.


“Sijalazimishwa na mtu yeyote sijagombana na ndugu zangu wa Chadema, najua matusi yatakuwa mengi ila hakuna tusi jipya. Nimeona sura aliyoonesha mama Samia kwenye ujenzi wa taifa, acha nije kumuunga mkono, ” amesema Hasani.

Tukio hilo limefanywa leo katika Kijiji cha Dumila Juu wilayani Kilosa, mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akiwa katika mwendelezo wa ziara yake mkoani Morogoro ya kukagua na kuimarisha uhai wa chama ngazi ya mashina.


Amuua mkewe kwa jembe akimtuhumu kuchepuka


 Polisi katika eneo la Navakholo, kaunti ya Kakamega wanachunguza kisa ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 67, anadaiwa kumuua mkewe mwenye umri wa miaka 54.


Marehemu, Rose Atieno alikuwa amemtembelea fundi wa kushona viatu ambaye ni jirani wakati mume wake alipomvamia.

Kwa mujibu wa ripoti ya Citizen, marehemu aligongwa na jembe huku mshukiwa akimtuhumu kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa yao.

Kamanda wa polisi wa kaunti hiyo Joseph Kigen alithibitisha kisa hicho akisema mshukiwa atafikishwa mahakamani punde baada ya uchunguzi utakapokamilika.

Mwili wa marehemu umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kakamega.


🔴🔴Breaking News: Matokeo ya kidato cha nne 2022 yatangazwa, Angalia hapa kuyaona


Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yaliyofanyika Novemba 14 hadi Desemba 1, 2022, Tanzania Bara na Visiwani.

Matokeo hayo yametangazwa leo Jumapili, Januari 29, 2023, makao makuu ya Necta jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Athumani Amasi.






‘Magari ya wagonjwa yasisafirishe maiti’


Wananchi wa Wilaya ya Mukono na Buikwe nchini Uganda wameiomba serikali kupiga marufuku magari ya wagonjwa kutumika kusafirishia maiti.


Mkazi wa Kijiji cha Lubumba wilayani Buikwe, Richard Tamale, alisema imekuwa mazoea kwa magari ya wagonjwa hasa yanayomilikiwa na wanasiasa kutumika kusafirishia maiti hali inayofanya jambo hilo kuwa kama sehemu ya kampeni zao za kisiasa.

“Fikiria kwamba imetokea dharura ya mgonjwa wakati dereva wa gari la wagonjwa ndiyo ametoka kushusha maiti, je, dereva atakuwa na muda hata wa kupulizia dawa ya kuua vijidudu gari yake? Kwa hiyo serikali lazima iingilie kati na kuzuia jambo hilo,” alisema.

Mkazi wa Kijiji cha Kisoga wilayani Mukono, Adams Lubinga, alisema si sahihi kuruhusu magari ya wagonjwa kusafirishia maiti kwa kuwa madereva hawataheshimu wala kujali wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura wakidhani ni sawa na kubeba maiti.

“Mara nyingi magari ya wagonjwa hayapewi nafasi na watumiaji wengine wa barabara kama madereva wa malori kwa sababu magari mengi ya wagonjwa yanatumika kwa shughuli nyingine ikiwemo kusafirisha maiti au kusafirisha watu wanaokwepa msongamano wa magari,” alisema Lubinga.

Mmoja wa madereva wa magari hayo ya wagonjwa, Fred Kiyimba, alikiri kuwa kubeba maiti kwenye magari ya wagonjwa ni kinyume cha sheria lakini mara nyingi madereva hujikuta njia panda katika hilo.

Kiyimba alisema baadhi ya magari  hununuliwa na wanasiasa, hivyo wapiga kura wao wanadhani kuwa wana haki ya kuyatumia kwa jambo lolote.

Mbunge wa Manispaa ya Mukono, Betty Nambooze, ambaye anamiliki magari mawili ya kubebea wagonjwa, alisema ili kuepuka hali hiyo, alinunua gari maalumu la mazishi ili kusaidia wapiga kura wake.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao waliomba uongozi wa Manispaa ya Mukono kuiomba serikali kupitia Wizara ya Afya kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva wa magari ya wagonjwa na namna ya kuhudumia masuala ya dharura.


763 wakamatwa kwa kutopeleka watoto shule


Zaidi ya wazazi 763 wamekamatwa katika operesheni maalum ya nyumba hadi nyumba, ya kuwasaka wazazi na walezi wasiopeleka watoto wao waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu katika wilaya yaTunduru mkoani Ruvuma.


Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema,kukamatwa kwa wazazi hao kumetokana na muda wa siku 14 waliopewa kupeleka watoto shule kwa hiari kumalizika licha ya uhamasishaji mkubwa uliofanywa na viongozi wa serikali,kamati ya ulinzi na usalama na madiwani.

Kwa mujibu wa Mtatiro,msako huo unafanyika usiku na mchana,na ni mkakati wa kuwapata watoto wote 5,869 waliomaliza darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza,lakini hadi mwishoni mwa wiki iliyopita wamebaki nyumbani.

amesema,katika msako huo wazazi wengine 600 wamejisalimisha kwa kupeleka watoto wao shule baada ya kushuhudia wenzao wamekatwa na kufikishwa polisi kwenye operesheni inayoendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Mtatiro alisema,operesheni hiyo imekuwa yenye mafanikio makubwa kwani katika muda wa siku tatu wamewapeleka zaidi ya watoto 1,335 shule kati ya 5,868 wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza na wanaendelea kuwatafuta watoto waliobaki.

Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Tunduru alisema,watahakikisha hadi Jumatatu ya wiki ijayo watoto wote wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza katika muhula wa masomo ulioanza tangu tarehe 9 Januari wanaripoti kwenye shule walizopangiwa.


Ufafanuzi kwa nini Shaka anastahili kuwa mkuu wa Wilaya Bara


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kumteua aliyekuwa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi Komredi Shaka Hamdu Shaka katika nafasi ya Ukuu wa Wilaya ya Kilosa.


Wakosoaji wengi wamejikita katika Uzanzibari na Ubara na kushindwa kujadili uhalali wa Kikatiba na Kisheria juu ya nafasi ya Ukuu wa Wilaya na sifa za wateule.

Ibara ya 61 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha nafasi ya Mkuu wa Mkoa na Ibara ya 61 (3) imempa Rais Mamlaka kikatiba kuteua wakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara kwa kushauriana na Waziri Mkuu na wake wa Zanzibar watateuliwa na Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na Rais wa JMT.

Ibara ya 61 inanukuu.-(1) Kutakuwa na Mkuu wa Mkoa kwa kila mkoa katika Jamhuri ya Muungano ambaye, bila ya kuathiri ibara ndogo ya (3), atakuwa ni kiongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

(2) Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

(3) Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar watateuliwa na Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na Rais.

Ibara ya 145 ya Katiba imeanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa ikiwemo ofisi za Wakuu wa Wilaya ambazo uteuzi na shughuli zake zimeainishwa na Sheria ya Tawala za Mikoa.

Sheria ya Tawala za Mikoa imeweka bayana kuwa Rais anaweza kugawa Madaraka yake katika ngazi za Mikoa kwa Wakuu wa Mikoa chini ya Kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Tawala za Mikoa na pia anaweza kukasimu madaraka yake katika ngazi ya Wilaya kwa Wakuu wa Wilaya chini ya Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Tawala za Mikoa. Vifungu husika vimenukuliwa:-

6.-(1) The President may by writing under his hand and the public seal, delegate any of hiss functions and duties under any written law to any Regional Commissioner.

13.-(1) There is hereby established in respect of each district in Mainland Tanzania the office of District Commissioner.

(2) Subject to the Constitution, every District Com- missioner shall be a public officer and shall be ap- pointed by the President.

(3) Subject to this Act and to any other written law, the District Commissioner shall, in. the exercise of his functions under this Act be subject to the directions, guidance or

instructions of the Regional Commissioner of the region in which the district for which he is appointed is situated.

Kwa mantiki hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kukasimu madaraka yake ya Urais katika eneo la Mkoa au la Wilaya kwa mtu yeyote ambaye ni Raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali ametoka upande upi wa Muungano.

Jambo ambalo watu wengi ama kwa kutokujua ama kwa lengo la kupotosha ni juu ya majukumu na nafasi zinazotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Nafasi ya Ukuu wa Wilaya au Ukuu wa Mkoa ni Madaraka yatokanayo na Madaraka ya Rais wa Jamhuri hivyo kama Rais wa Jamhuri anaweza kutoka upande wowote wa Jamhuri, maana yake (impliedly) hata Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya anaweza kutoka katika eneo lolote la Muungano vivyo hivyo kwa nafasi za Kazi katika masuala ya Muungano kama Fedha, Ulinzi, Mawasiliano n.k Mtanzania anaweza kufanya kazi upande wowote wa Muungano. Mifano ipo mingi ya Watanzania Bara ambao wameteuliwa katika nafasi nyeti na kubwa visiwani kuliko hata za uDC.

Vivyo hivyo nafasi za Ubunge wa Jamhuri, Mtanzania yeyote anaweza kugombea popote, hapa hakuna sababu ya kutumia nguvu kujadiliana ni suala la logic tu, Mtu unaishi Songwe huwezi tu kuamka asubuhi ukaenda kugombea Ubunge Kigoma, ndivyo ilivyo, kulalamika kuwa kuna wazanzibari wamepata nafasi za Ubunge bara ni ubaguzi usio na haya, swali la kujiuliza ni je kuna Mbara yeyote aliwahi kugombea ubunge Zanzibar akakataliwa, je, wanaolalamika wana ushahidi kuwa hakuna wabara ambao ni wabunge Zanzibar kwa kuchaguliwa kutokana na kukidhi sifa na vigezo?

Mamlaka ya uteuzi humteua mtu kwa vigezo vingi na sio kwa sababu ya eneo atokako, dini wala kabila yake, siku Rais wa Zanzibar akiona kuna Mbara mwenye sifa ya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Wete ninaamini hatasita kufanya hivyo.

Kikatiba na Kisheria hakuna mahala popote ambapo Rais Samia amekiuka kumteua Shaka, malalamiko yaliyopo ni kelele tu za kibaguzi na kutokujua misingi ya kisheria.


Safari ya mwisho ya Nemes aliyeuawa vitani Ukraine, hapa ndipo alipolala


Ndugu, jamaa na marafiki wa Mtanzania, Nemes Tarimo wamekusanyika kijijini kwao huko Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya kwa ajili ya kumuaga na kumhifadhi katika nyumba yake ya milele kijana huyo.



Simba yatangaza CEO mpya

Uongozi wa Klabu ya Simba umefikia makubaliano ya kumuajiri Ndugu Imani Kajula kuwa Afisa mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo kwa mkataba wa miezi sita.


Kajula anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Barbara Gonzalez ambaye alijiuzulu nafasi yake Desemba 2022


Kajula amewahi kuwa kwenye Kamati ya maandalizi ya Michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 akiwa na uzoefu kwenye masuala ya Uongozi wa mpira wa miguu


Aliwahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Masoko na mawasiliano ya EAG Group akihudumu kwenye nafasi hiyo tangu mwaka 2013.



BIbi wa miaka 80 adaiwa Kujinyonga Hadi Kufa


Mkazi mmoja wa kitongoji ya Bulengahasi, Kata ya Katoro, Wilaya ya Geita, Mkoani Geita anayefahamika kwa jina la Kwilavia Luvinza anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 80 amekutwa amejinyonga kwenye mti wa mwembe chanzo kikiwa bado hakijafahamika.


Mtoto wa mama huyo Mashaka Machibiya ameeleza tukio hilo lilivyotokea.

Nae Balozi wa shina namba 18 kijijini hapo ameelezea juu ya tukio hilo huku akisema kwa taarifa aliyopokea kutoka kwa Daktari ni kwamba mama huyo huenda ameuawa.

Wakazi wa Bulengahasi nao wamesikitishwa na tukio hilo huku juhudi za kulitafuta Jeshi na Polisi na kutolea ufafanuzi zikiendelea.

Chanzo: Storm FM


Mahakama yamwachia huru anayedaiwa kumuua mhasibu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwachia huru, Omary Hassan maarufu kama Mbegu aliyekuwa anakabiliwa na shitaka la kumuua kwa kukusudia Mwasiti Yasin aliyekuwa mhasibu wa Kampuni ya Grants Care Limited, baada ya ushahidi wa upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Renatus Rutta alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo upande wa mashitaka walipeleka mashahidi wanane.

Hakimu Rutta alisema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi hao, hakuna sehemu ambapo mshitakiwa ameguswa moja kwa moja, hivyo alimwachia huru.

“Katika mashahidi ambao waliletwa na upande wa mashitaka kutoa ushahidi dhidi yake, hakuna ushahidi ambao umeweza kumgusa mshitakiwa, ninamwachia mshitakiwa huru,” alisema Hakimu Rutta.

Kwa mujibu wa hati inadaiwa kuwa katika eneo la Uhuru na Sikukuu, Omary Hassan maarufu kama Mbegu alimuua kwa kumshambulia kwa risasi Mwasiti Yasin.

Inadaiwa marehemu akiwa ni Mhasibu wa Kampuni ya Grants Care iliyoko eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, akiwa njiani mtaa wa Uhuru /Swahili kuelekea katika benki ya Habibu Afrika akiwa na Sh milioni 7.2 alivamiwa na majambazi kisha walimpiga risasi nakuchukua fedha hizo.



Wanandoa watelekeza watoto wao watano

OFISI ya ustawi wa jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imeanza kuwatafuta wanandoa wanaodaiwa kutelekeza watoto wao watano.


Wazazi na watoto wao walikuwa wanaishi katika Kitongoji cha Mwabuluki Kijiji cha Ng’wang’osha Kata ya Nyamalogo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.


Ofisa Ustawi wa Jamii katika halmashauri hiyo, Kulian Mlalama alisema hayo jana alipoitembelea familia hiyo akiwa amefuatana na Ofisa Mthamini na Mfuatiliaji kutoka Shirika la Thubutu Africa Intiative (TAI) la wilayani Shinyanga, Paschalia Mbugani.


Mlalama alisema wazazi hao wanatafutwa hata kama wameachana ili wawapeleke shule watoto hao na watimize wajibu wa kulea kwa ujumla.


“Sisi tutawaandikisha shule, tumeanza kuwatafuta wazazi tulikwenda kwa ndugu zao kwenye kijiji jirani kupata mawasiliano lengo ni watoto wapate haki zao za msingi ikiwemo elimu,” alisema.


Mtendaji wa kijiji hicho, Nyosoku Wambura alisema walifanya uchunguzi na wakabaini kuwa mama wa watoto hao ameolewa na mwanaume mwingine mkoani Geita na baba yao hajulikani alipo.


Mbugani alisema kitendo cha kutelekeza watoto na kusababisha wakose haki ya kupata elimu ni ukatili.


Mlezi wa watoto hao, Joyce Robert alisema anaishi na mumewe, Mashimba Usumahu anayefanya vibarua vya kulima na kwamba wao wana watoto sita hivyo familia imewaelemea.


Kwa mujibu wa Joyce, Mwenyekiti wa kitongoji, Marco Luhende ndiye aliyewapeleka watoto waliotelekezwa waishi kwenye familia yake.



Wengi wafurika kumpokea Tindu Lissu

Hatimaye Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amewasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Ubelgiji na kupokelewa na wafuasi wa chama hicho.


Mwanasiasa huyo nguli wa upinzani ambaye awali alikuwa Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria nguli, amerejea baada ya miaka mitano kuishi nje ya nchi.


Lissu aliwahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amepokelewa na viongozi na wanachama wa Chadema.


Mamia ya wafuasi wa CHADEMA wamekusanyika nje ya lango hilo wakiimba na kucheza huku ngoma pamoja na mavuvuzela.


Hata hivyo Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi na kuhakikisha wafuasi hao hawaingii ndani ya eneo la uwanja na badala yake wanabaki nje ya lango kuu pembezoni mwa barabara ya Nyerere.


Pia hali ya ulinzi na usalama iliimarishwa ili kuhakikisha kuwa shamrashamra hizo zinamalizika bila ya kuwepo kwa fujo.




Kairuki awajia juu walimu wanaowalamba viboko kwa wanafunzi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki,amewaonya walimu wanaokiuka Kanuni za Elimu za mwaka 2002 na kutoa adhabu kali kwa wanafunzi Serikali haitosita kuchukua hatua kali dhidi yao.


Waziri Kairuki ameyasema hayo Januari 25,2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Viongozi wa Elimu ngazi ya Halmashauri kwenye kikao kazi cha uboreshaji wa Usimamizi wa Elimu Msingi na Sekondari Jiji la Dar es Salaam.


Waziri ametoa rai kwa walimu kwa kukumbuka kuwa wamekasimiwa ya kuwa walinzi wa watoto wanapokuwa shuleni kwa hiyo wasiwe sehemu ya kuwafanya watoto kuwa watoro kupitia adhabu wanazozitoa zinazokiuka taratibu, miongozo na kanuni mbalimbali.


“Suala zima la adhabu ya Viboko shuleni linaongozwa na Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 na umeeleza bayana kabisa hivyo ni vyema walimu wakafuata taratibu zilizoanishwa kwenye Waraka namba 24 wa mwaka 2002 ambao umeeleza wazi ni nani mwenye Mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko na viboko vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi vinatolewa kwa wanafunzi.


“Hatusemi watoto wasichapwe lakini wachapwe kwa kufuata taratibu na vigezo na kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa.” amesisitiza Waziri Kairuki.


Waziri Kairuki amesema kuwa mwongozo huo unaeleza wazi ni nani mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko na viboko vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi vinatolewa kwa wanafunzi.


Ameendelea kufafanua kuwa waraka huo na Kanuni za Elimu za mwaka 2002 lazima zifuatwe katika utolewaji wa adhabu ya viboko shuleni.


“Kwa Mujibu wa mwongozo huo umeelekeza adhabu hiyo ya viboko inaweza kutolewa pale ambapo umetokea utovu wa nidhamu uliokithiri au makosa ya jinai yaliyotendeka ndani au nje ya shule yenye muelekeo wa kuishushia heshima shule.


“Kwa mujibu wa waraka huo adhabu hiyo inavyotolewa lazima izingatie vigezo ikiwemo ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na haipaswi kuzidi viboko vinne kwa wakati mmoja.


“Waraka huo umeeleza jinsi adhabu hiyo inapaswa kutolewa kwa mtoto wa jinsia ya kike na kiume. Kwa Mtoto jinsia ya kike adhabu inapaswa kutolewa mikononi, na kwa mtoto jinsia ya kiume ni kwenye makalio.


“Pia Waraka huo umeeleza kuwa mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko ni Mwalimu Mkuu au Mkuu wa shule husika au Mwalimu mwingine atakayekuwa ameteuliwa tena kwa maandishi,” amesema.


Pia ametanabaisha kuwa kwa mtoto wa kike imeelekezwa aadhibiwe na mwalimu wa kike au labda tu kama shule hiyo haina mwalimu wa kike ndipo anaweza kuadhibiwa na mwalimu wa kiume.


Hata hivyo kumekuwa na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na mwanafunzi kufanyiwa ukatili na mwalimu kwa kupewa adhabu isiyo na staa na kuibua hisia kwa wazazi.



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo