Aliyesombwa na mto Lindi akutwa kichwa na mifupa pekee


Mwili wa Mwanahawa Abdallah (65), mkulima na mkazi wa Kijiji na Kata ya Kiwalala, Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi aliyepotea wiki iliyopita kwa kusombwa na maji kwenye Mto Lukuledi, umeonekana ukiwa umebaki kichwa na mifupa baada ya kuliwa na wanyama.


Kwa mujibu wa mashuhuda walioshiriki kumtafuta mama huyo, mwili wake ulikutwa pembezoni mwa mto huo Januari 24, mwaka huu, majira ya saa saba mchana ukiwa hauna ngozi wala nyama isipokuwa kichwani.

Wakizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, baadhi ya mashuhuda hao walioshiriki kumtafuta mwanakijiji mwenzao huyo, wakiwamo Semi Dume, Issa Selemani, Paulo Daniel na Ibrahim Mkonogile, walidai kuwa mwili wa Mwanahawa ulikutwa ukiwa umebaki kichwa na mifupa kutokana na nyama yote kuliwa na wanyama waliokuwapo majini.

"Tulichokikuta na kubaini ni yule mama ni kichwa chake, lakini nyama yote ya mwili wake imeliwa na kubaki mifupa mitupu," alidai Daniel.

Washiriki walimtafuta mama huyo kwa siku nne mfululizo tangu aliporipotiwa kusombwa na maji Januari 20, mwaka huu.

Walidai kuwa kulingana na hali na mazingira yalivyokuwa, familia ya marehemu, hasa watoto wake, waliamua mabaki ya mifupa na kichwa kilichokutwa pembeni mwa mto, yazikwe hukohuko mtoni badala ya kupelekwa nyumbani kwa maziko.

"Mifupa tuliyoikuta ni ya mikono na miguu pekee. Kichwa kilikuwa na ngozi na nywele zake," alidai Mkonogile.

Rashidi Mega, Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Kiwalala na mtoto wa tatu wa marehemu, walikiri kuonekana kwa mabaki ya mwili wa mama huyo na kuamua yazikwe hukohuko kando ya mto kutokana na mazingira waliyoyakuta.

“Ilikuwa vigumu kufikisha nyumbani mabaki yale, hivyo tukaamua kuyazika hukohuko," alisema Mega.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwalala, Zaituni Chilinga, alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia tukio hilo, alikiri mabaki ya mifupa ya mwili wa mwanakijiji huyo kupatikana.

Iliripotiwa na wanakijiji hao Januari 20, mwaka huu kwamba, siku hiyo majira ya saa nane mchana, Mwanahawa, akiwa ameongozana na jirani yake, Fatu Dadi wakitokea shambani kurejea nyumbani kwao, walipofika Mto Lukuledi, aliamua kuoga ndipo maji yaliyokuwa yanatiririka mtoni yakamchukua na kumpeleka eneo alilokutwa ameshafariki dunia.

Chanzo:Nipashe


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo