DC mteule ambaye hakujitokeza kuapishwa ahojiwa kwa dakika 50

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Japheth Maganga amesema kwa sasa hawezi kutoa sababu kwanini hajaripoti wilaya aliyopangiwa ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera huku akihojiwa na Jeshi la Polisi, mkoani Tanga.


Waliomhoji Maganga ni Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga wakitumia zaidi ya dakika 50. 

Bado Polisi hawajaweka wazi sababu za mahojiano hayo.

Maganga na Rais wa CWT, Leah Ulaya waliteuliwa wiki iliyopita na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya lakini wakati wenzao wakiapishwa kwenye maeneo yao leo Jumatatu, Januari 30, 2023 wao wapo jijini Tanga wakiongoza mkutano wa viongozi wakuu wa CWT.

Ulaya aliteuliwa kuwa DC wa Mbogwe, Mkoa wa Geita ambapo wenzake wanaapishwa leo Jumatatu na Mkuu wa Mkoa huo, Martin Shigela.

Mara baada ya kumaliza kuhojiwa na polisi kuanzia saa 4:36 hadi saa 5:24 asubuhi  nje ya ukumbi wa mkutano huo unaofanyikia Hoteli ya Regal Naivera, Mtaa wa Bombo jijini Tanga alirejea ukumbini na baadaye kidogo alitoka nje.

Nje ya ukumbi ambapo Mwananchi Digital limeweka kambi lilizungumza na Magamba ambaye amesema, “kwa sasa nimeziba mdomo labda usubiri tutakapomaliza kikao ndipo nitazungumza kuhusu nafasi ya U-DC na CWT."

Wakati Maganga akisema hayo, Rais wa CWT hakuweza kutoka ndani ya ukumbi wa mkutano huo huku maofisa wa CWT wakisema hajaruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Kitendo cha viongozi wakuu hao wa CWT kuonekana Tanga wakati wenzao wakiapishwa kimezua mjadala maeneo mbalimbali ikiwemo mitandaoni na kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba wameomba wateuliwe wengine kwenye nafasi hizo za U-DC ili kuwawezesha wao kuendelea na majukumu yao ya CWT.

Chanzo: Mwananchi Digital


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo