‘Magari ya wagonjwa yasisafirishe maiti’


Wananchi wa Wilaya ya Mukono na Buikwe nchini Uganda wameiomba serikali kupiga marufuku magari ya wagonjwa kutumika kusafirishia maiti.


Mkazi wa Kijiji cha Lubumba wilayani Buikwe, Richard Tamale, alisema imekuwa mazoea kwa magari ya wagonjwa hasa yanayomilikiwa na wanasiasa kutumika kusafirishia maiti hali inayofanya jambo hilo kuwa kama sehemu ya kampeni zao za kisiasa.

“Fikiria kwamba imetokea dharura ya mgonjwa wakati dereva wa gari la wagonjwa ndiyo ametoka kushusha maiti, je, dereva atakuwa na muda hata wa kupulizia dawa ya kuua vijidudu gari yake? Kwa hiyo serikali lazima iingilie kati na kuzuia jambo hilo,” alisema.

Mkazi wa Kijiji cha Kisoga wilayani Mukono, Adams Lubinga, alisema si sahihi kuruhusu magari ya wagonjwa kusafirishia maiti kwa kuwa madereva hawataheshimu wala kujali wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura wakidhani ni sawa na kubeba maiti.

“Mara nyingi magari ya wagonjwa hayapewi nafasi na watumiaji wengine wa barabara kama madereva wa malori kwa sababu magari mengi ya wagonjwa yanatumika kwa shughuli nyingine ikiwemo kusafirisha maiti au kusafirisha watu wanaokwepa msongamano wa magari,” alisema Lubinga.

Mmoja wa madereva wa magari hayo ya wagonjwa, Fred Kiyimba, alikiri kuwa kubeba maiti kwenye magari ya wagonjwa ni kinyume cha sheria lakini mara nyingi madereva hujikuta njia panda katika hilo.

Kiyimba alisema baadhi ya magari  hununuliwa na wanasiasa, hivyo wapiga kura wao wanadhani kuwa wana haki ya kuyatumia kwa jambo lolote.

Mbunge wa Manispaa ya Mukono, Betty Nambooze, ambaye anamiliki magari mawili ya kubebea wagonjwa, alisema ili kuepuka hali hiyo, alinunua gari maalumu la mazishi ili kusaidia wapiga kura wake.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao waliomba uongozi wa Manispaa ya Mukono kuiomba serikali kupitia Wizara ya Afya kutoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa madereva wa magari ya wagonjwa na namna ya kuhudumia masuala ya dharura.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo