763 wakamatwa kwa kutopeleka watoto shule


Zaidi ya wazazi 763 wamekamatwa katika operesheni maalum ya nyumba hadi nyumba, ya kuwasaka wazazi na walezi wasiopeleka watoto wao waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu katika wilaya yaTunduru mkoani Ruvuma.


Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema,kukamatwa kwa wazazi hao kumetokana na muda wa siku 14 waliopewa kupeleka watoto shule kwa hiari kumalizika licha ya uhamasishaji mkubwa uliofanywa na viongozi wa serikali,kamati ya ulinzi na usalama na madiwani.

Kwa mujibu wa Mtatiro,msako huo unafanyika usiku na mchana,na ni mkakati wa kuwapata watoto wote 5,869 waliomaliza darasa la saba mwaka jana na kuchaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza,lakini hadi mwishoni mwa wiki iliyopita wamebaki nyumbani.

amesema,katika msako huo wazazi wengine 600 wamejisalimisha kwa kupeleka watoto wao shule baada ya kushuhudia wenzao wamekatwa na kufikishwa polisi kwenye operesheni inayoendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Mtatiro alisema,operesheni hiyo imekuwa yenye mafanikio makubwa kwani katika muda wa siku tatu wamewapeleka zaidi ya watoto 1,335 shule kati ya 5,868 wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza na wanaendelea kuwatafuta watoto waliobaki.

Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Tunduru alisema,watahakikisha hadi Jumatatu ya wiki ijayo watoto wote wanaotakiwa kuanza kidato cha kwanza katika muhula wa masomo ulioanza tangu tarehe 9 Januari wanaripoti kwenye shule walizopangiwa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo