DAR ES SALAAM, TANZANIA
Rais Jakaya Kikwete leo, Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la
Msingi la ujenzi wa Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam, huku akiwaonya
watu ambao amewaeleza kuwa wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha
tabia hiyo na kuelekeza nguvu kwenye maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa Kigamboni ambao
wanaondolewa katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa daraja
hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki
zao zote.
Daraja hilo la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa
mara ya kwanza zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh.
bilioni 214.6 na litakuwa tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa
muda huo unaweza kupungua na kubakia miezi 30.
