Wanasayansi wamebaini kuwa inawezekana kuondoa maambukizi
mapya ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (EMCTC) tofauti na
ilivyozoeka kuwa ni kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto(PMCTC)
Pia malengo, mipango na mikakati ilivyowekwa na wadau
mbalimbali wanaohusika na mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI ikifuatwa na
kutumiwa ipasavyo ndiyo njia pekee itakayowezesha kuondoa maambukizi mapya ya
virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Akizungumza kwenye kikao cha wadau mbalimbali kilichofanyika
kwenye ukumbi wa hospitali ya wilaya Makete Dkt. Rugola Mtandu, (CEO,
PHARMKONSULT AFRICA LTD) amesema mpango huo unatekelezwa kwenye nchi 42 duniani
ambazo zina maambukizi makubwa ya virusi vya UKIMWI ikiwemo Tanzania
Amesema inawezekana kuondoa maambukizi hayo kwa asilimia 90
na pia kuhakikisha kina mama nao wanazidi kuwa hai, na unatekelezwa kwa
wanawake waliopo katika uwezo wa kubeba mimba, miaka 15-49
Ameyataja malengo makubwa ya kuondoa maambukizi ya mama
kwenda kwa mtoto kuwa ni kupunguza maambukizi hayo hadi kuwa chini ya asilimia
5, kupunguza kwa asilimia 90 ya maambukizi mapya ya vvu kwa akina mama na wao
wawe hai,njia za uzazi wa mpango zipatikane kwa wanawake wote, pamoja na upatikanaji
kwa asilimia 90 wa ART kwa wajawazito ambao wana vvu
Wilaya ya Makete ni miongoni mwa wilaya zilizopo hapa nchini
ambazo zina maambukizi ya virusi vya ukimwi hivyo jitihada mbalimbali zimekuwa
zikichukuliwa na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wananchi
kupambana na changamoto hiyo