Jela kwa kumpiga mchepuko wa mkewe na mkewe katika fumanizi


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela mkazi wa Kongowe, Singbard Buchard na ndugu zake wawili baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumshambulia na kumdhuru mwili Rashid Mohamed na Anitha Rauyan.


Pia mahakama hiyo imeamuru washtakiwa hao kulipa jumla ya Sh 1 milioni kwa ajili fidia ya maumivu waliyoyapata wakati waliposhambuliwa walalamikaji hao.

Mbali na Singbard wengine ni Albert Buchard na Delfina Buchard.

Akitoa hukumu hiyo hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi alisema mahakama hiyo imetoa adhabu hiyo baada ya kuzingatia kuwa washtakiwa hao ni kosa lao la mara ya kwanza.

Kyaruzi alisema kitendo walichokifanya washtakiwa hao kwa kuwapiga, kuwatembeza mitaani  na kuwafunga mikono walalamikaji hao inaonyesha ni zaidi ya kipigo hivyo haikubaliki kwenye jamii.

"Mtuhumiwa Singbard anasema Anitha ni mke wake hata kama alijihusisha na haya alitakiwa asichukue sheria mkononi kwa kumpiga mkewe kufanya hayo si sahihi,"alisema Kyaruzi.

Alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kwa kuangalia washtakiwa hao hawatarudia tena kufanya makosa kama hayo kwa kupitia hawa watajitekebisha.

Kyaruzi alisema kosa linalowatia hatiani adhabu yake miaka isiyopungua mitano lakini mahakama hiyo imezingatia utetezi waliotoa mahakamani hapo ikiwemo kutegemewa na familia zao na kosa lao la kwanza.

"Hivyo mahakama hii inawahukumu kila mmoja kifungo cha mwaka mmoja na washtakiwa hao kwa pamoja wanatakiwa kuwalipa fidia ya Sh1milioni kwa ajili ya maumivu waliopata wakati walipofanya shambulio," alisema Kyaruzi.

Awali, Wakili wa Serikali, Monica Ndekidemi alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo la kiwango cha juu na kuwasababishia majeraha walalamikaji hao.

"Walitumia silaha katika kuwaumiza walalamikaji, hivyo naiomba mahakama hii washtakiwa hao iwalipe walalamikaji Sh5 milioni kwa ajili ya fidia ya maumivu waliyoyapata," alidai Ndekidemi.

Naye mshtakiwa Singbard alieleza mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa Aneth bado ni mke wake hajamuacha na amemuachia watoto wadogo na sijui kama wanaenda shule au la.

Inadaiwa kwamba, Mohamed na Anitha  walikuwa wapenzi  ambapo siku ya tukio, washitakiwa hao  waliwavamia wakiwa chumbani .

Washtakiwa hao waliwavamia kwa madai kwamba Mohamed alikuwa anatembea na  Anitha ambaye alikuwa mke wa Singbard.

Inadaiwa kuwa washtakiwa hao baada ya kumvamia Mohamed na Anitha waliwapiga sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia fimbo, waliwafunga mIkono na kisha kuwapeleka kwa kiongozi wa eneo hilo wakiwatuhumu kwa ugoni.

Katika utetezi wao, washtakiwa hao walikana kuhusika kuwadhuru Mohamed na Anitha, huku wakikiri kufika eneo la tukio.
Chanzo: Mwananchi digital


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo