Wanawake wawili wanaodhaniwa kuwa ni washirikina wamekutwa wakiwa watupu (bila nguo) alfajiri ya leo Machi 15, 2025, katika madhabahu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Jimbo la Hai, Usharika wa Nkwarungo, Machame Kaskazini, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Tukio hilo limezua taharuki kubwa wilayani hapa, ambapo wanawake hao walikamatwa na kuzungukwa na wananchi, baada ya kuhojiwa walidai kuwa walitumwa kwenda kuchukua ulimi wa mwanamke mmoja aliyezikwa hivi karibuni katika makaburi ya usharika huo.
Akizungumza eneo la tukio, Msaidizi wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Bomang’ombe, (ASP) Daudi Kimashi, amethibitisha kuwakamata wanawake hao na kusema kuwa wanashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Tukishindwa kwa njia za kibinadamu tutawapeleka hata kwenye maombi, uwepo wao hapa ni kosa kisheria, kwa hiyo tutawauliza wametokeaje hapa,” amesema Kimashi.
Akizungumza Mwinjilisti wa Usharika wa Nkwarungo, Jeremiah Nkya, amesema wanawake hao walinaswa na walinzi wa usharika huo wakiwa na mabunda ya vitu visivyoeleweka, ambavyo walinzi waliamua kuvichoma.