Mchungaji Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama, Dar es Salaam, Dkt. Eliona Kimaro aliyepewa likizo ya siku 60 amesamehewa na kupewa ruhusa ya kurudi.
Msamaha huo umetangazwa leo na Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Pwani, Askofu Alex Malasusa katika ibada ya misa iliyofanyika katika kanisa la KKKT Usharika wa Kinyerezi.
Askofu Malasusa amesema kuwa Mchungaji Kimaro aliandika barua kwa uongozi wa kanisa hilo na kwa wachungaji wenzake kuomba msamaha kwa kanisa jambo ambalo limeufanya uongozi wa kanisa kuona haja ya kumsamehe na kumrejesha katika kazi yake ya kulitumikia kanisa.
"Mchungaji Eliona Kimaro umeomba msamaha kwa Kanisa, kwa wachungaji wenzako na kwa jamii, kwangu na hata kwa Baba Askofu Mkuu wa Kanisa. Sisi pia tunakupa pole kwanza, jambo lolote linapopita lazima liumize nafsi.
"Kanisa linapopita katika Ulimwengu, shetani naye hujihudhurisha, tunapoonq mitikisiko ya Kanisa hasa sisi washarika tusiwe mashabiki, kwa sababu pale ni nuru na giza vinagomba. Shetani anaweza akaingia katikati ya watu wa Mungu na akatutikisa.
"Nafahamu zipo taratibu nzuri za Kanisa ambazo ulikuwa ukizifuata, na wewe umekiri kwamba zimekusaidia, lakini watu hawajui. Wewe endelea kuutafuta uso wa Mungu na huduma ya Mungu ambayo Mungu alikuita kwayo.
"Mchungaji Kimaro kama ulivyoomba, kwa niaba ya washarika natamka umesamehewa, endelea kukaa, kutafakari na kukaa karibu na Mungu, shetani kamwe asituondoe katika msitari," amesema Askofu Malasusa.