Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ni miongoni mwa waombolezaji wa kifo cha Linah, mke wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kilichotokea juzi.
Kikwete amewasili msibani leo, Julai 17 saa sita mchana na kuweka saini kwenye kitabu cha maombolezo.
Kikwete amemfariji Dk Mwakyembe na kumtaka awe mvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
"Mwakyembe ni rafiki yangu wa siku nyingi, hata wakati mama anaumwa aliniambia na nilienda kumjulia hali alipokuwa Muhimbili, nimtake awe mvumilivu tunajua ana majonzi msiba huu ni wetu sote,"amesema.
Wengine waliofika kumfariji Dk Mwakyembe ni Jaji Mstaafu Damian Lubuva, ambaye pia alimjulia hali Linah wakati akiwa hospitali.
"Nimekuja kumpa pole Harrison, tunafahamiana muda mrefu na mkewe alipokuwa anaugua pale Muhimbili nilikuwa naenda kumtembelea lakini juzi nilivyokuwa kijijini ndiyo nimepata taarifa za mama yetu ametutoka. Ni msiba wetu sote tunaelewa majonzi yake, uchungu aliyokuwa nao yeye na familia yake lakini kifo kimeumbwa na Mwenyezi Mungu kinapotokea sote ni tunatakiwa tumshukuru Mwenyezi Mungu,"amesema.
Wengine waliofika kumfariji Dk Mwakyembe ni Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji; Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi; Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga na viongozi wengine wa Serikali waliopo madarakani na wastaafu.
Mjumbe wa kamati ya mazishi, Andrew Magombano amesema mwili wa Linah utaagwa kesho baada ya ibada itakayofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kunduchi kuanzia saa nne asubuhi.
"Baada ya ibada tutaaga na saa saba kamili tutaelekea uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kwenda Mbeya," amesema Magombano.