Mkazi wa Kijiji cha Mngoji kilichopo Kata ya Dihimba Mkoani Mtwara, Abdul Shaha (47) amekutwa amefariki pembezoni mwa Bahari ya Hindi Mkoani Mtwara huku baadhi ya Wananchi wakidai enzi za uhai wake alikuwa anawaingilia Watu kimwili wakiwa wamelala usiku.
Diwani wa Kata hiyo ya Dihimba Idrisa Ally amesema Mwanaume huyo amekutwa pembezoni mwa Bahari akiwa na majeraha kwenye mwili wake ambapo amesema yapo madai kwamba Abdul alikuwa anawaingilia Watu (Wanawake na Wanaume) wa eneo kimwili kwa njia ya ushirikina wakiwa wamelala usiku ingawa madai hayo hayajathibitishwa.
Diwani huyo amewasihi Wananchi wa Kijiji hicho kuendelea kuwa watulivu kwani Jeshi la Polisi bado linafanya uchunguzi juu ya tukio hilo.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Isack Mushi amesema uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na Madaktari umebaini chanzo cha kifo ni kuvuja kwa damu nyingi kutokana na jeraha alilolipata marehemu kichwani baada ya kupigwa “Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza sababu za mauaji hayo na halitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria Wahalifu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na uvunjifu wa amani”.