Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya imeahirishwa tena leo Jumatatu, Novemba 21, 2022 baada ya upande wa mashitaka kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwa hakimu anayesikiliza shauri hilo, Salome Mshasha yupo kwenye shughuli nyingine za kimahakama.
Sabaya na wenzake wanne walifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi kwa mara ya kwanza Juni Mosi, 2022, wakikabiliwa na mashitaka saba ikiwemo uhujumu uchumi ambapo leo Novemba 21 anatimiza siku 174 akiwa mahabusu.
Septemba 6 mahakama hiyo iliwaachia huru washirika wa wanne wa Sabaya, Sylivester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey baada ya kukiri kutenda makosa ya uhujumu uchumi ambapo mahakama iliwatia hatiani na kuwaamuru kulipa kila mmoja faini ya Sh50,000 na fidia ya Sh1milioni kwa mwathirika wa tukio hilo ambaye ni Alex Swai
Leo Novemba 21, 2022, upande wa mashitaka ukiongozwa na Suzy Kimaro kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) aliieleza mahama hiyo walikuwa tayari kuwasilisha nyaraka za kuipa nguvu mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo na hati ya kuruhusu shauri hilo liendelee.
"Leo upande wa mashitaka tulikuwa tayari kuwasilisha nyakara za kuipa mamlaka mahakama hii kusikiliza kesi hii pamoja na hati ya kuruhusu shauri hili liendelee lakini tumepata taarifa hakimu anayesikiliza shauri hili hatasikiliza kwa kuwa yupo kwenye (session) nyingine hivyo tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa kesi hii," amesema
Hivyo, wakili wa upande utetezi, Hellen Mahuna ameisisitiza mahakama hiyo kufanya uharakishwaji wa usikilizwa kwa wakati kesi hiyo kwani mteja wao ni mgonjwa na anazidi kuteseka.
Hata hivyo, Hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Jenifa Edward alieleza upande wa mashitaka wameeleza hakimu anayesikiliza kesi hiyo yupo kwenye shughuli nyingine akaahirisha kesi hiyo mpaka Disemba 5, 2022.
"Kwa maelezo yaliyotolewa na wakili wa upande wa mashitaka hakimu anayesikiza shauri hili yupo kwenye session nyingine, ninahairisha shauri hili mpaka Disemba 5 kama kuna chochote mtaelezwa," amesema