Hofu
ya kupoteza soko kwa makampuni ya kigeni yanayozalisha umeme dhidi ya
makampuni ya kitanzania imetajwa kuwa chanzo cha vita dhidi ya kampuni
ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Chanzo
cha uhakika kutoka Wizara ya Nishati na Madini kimetoa taarifa hiyo kwa
gazeti hili jana kuwa kwa zaidi ya muongo mmoja, kampuni za kigeni
zimekuwa zikipata faida kubwa kwa kuzalisha umeme na kuuza kwa bei ya
juu nchini.
Kampuni
ya IPTL ambayo inamilikiwa na kampuni ya kizalendo, Pan African Power
Solutions Tanzania Limited (PAP) iliishtua dunia mwishoni mwa mwaka jana
pale ilipotangaza dhamira yake ya kushusha bei zake kutoka senti za
Kimarekani 26 na 30 ya sasa mpaka senti za Kimarekani sita (6) na nane
(8) kwa kila unit, pale itakapobadilisha mitambo yake kuweza kutumia
gesi badala ya mafuta.
Kwa
sasa, makampuni mengine katika soko yanatoza kati ya senti za Kimarekani
38 na 60 kwa kila unit. “Watanzania wasidanganywe na taarifa
zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa IPTL ilinunuliwa na
PAP bila kufuata sheria. Kuna kampeni ya kupakana matope kwa tamaa ya
kuzalisha umeme kwa watanzania kutokana na biashara hii kuwa na faida
kubwa katika sekta hii muhimu kiuchumi ", chanzo hicho kilisema.
Aidha,
kampuni ya PAP katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa
jijini Dar es Salaam jana, imesema kuwa kampuni imeshtushwa na baadhi ya
wawekezaji katika sekta hiyo pamoja na wanasiasa kuanzisha vita dhidi
yao mara baada ya kutangaza kupunguza gharama za umeme.
Uongozi
wa kampuni hiyo umesema kuwa watanzania watafurahia gharama hizo za
chini baada ya utekelezaji wa mkakati wao wa utanuzi na ubadilishaji wa
mfumo wa mitambo yao ambao utaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme
kutoka mega wati 100 za sasa mpaka mega wati 500.
Taarifa
fupi iliyotolewa jana na katibu na mshauri wa maswala ya sheria wa
IPTL/PAP, Bw Joseph Makandege, imesema kuwa kampuni hiyo imekuwa
ikikumbana na changamoto ambazo zinajaribu kuzorotesha jitihada za
uongozi mpya za kuleta mabadiliko ambayo yatapelekea kampuni hiyo kuanza
kuzalisha umeme wenye gharama nafuu kwa watanzania wote.
Taarifa
hiyo imetolewa baada ya machapisho mbalimbali ya vyombo vya habari
yanayoishutumu kampuni hiyo kutoa hongo kwa wajumbe wa kamati ya bunge
ya nishati na madini kulinda matakwa yao au kuwalinda dhidi ya tuhuma
mbali mbali wanazo husishwa nazo.
"Uongozi
wa PAP katu haijapendezwa na jitihada za kuiangusha kampuni badala ya
kushirikiana katika kuhakikisha kuwa tunazalisha umeme ambao utakuwa na
manufaa makubwa kwa taifa hili na walaji wote nchi nzima.
"Tukiwa
kama kampuni ya ufuaji umeme, tunaelewa faida za kiuchumi zitokanazo na
umeme wa gharama nafuu kwa mteja mmoja mmoja na kwa maendeleo ya
kiuchumi ya nchi nzima. Kwa sababu hiyo ndiyo maana sasa tumeelekeza
jitihada zetu katika kuona ni jinsi gani ya kuzaliza umeme wa gharama
nafuu ambao utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi ya nchi hii, pasipo
kuingia katika malumbano ambayo yataturudisha nyuma na kushindwa
kutekeleza lengo letu la kuwekeza vilivyo katika sekta hii muhimu,"
ilisomeka taarifa hiyo.
Bw.
Makandege alisema kuwa kampuni yake imeamua kutafuta njia nzuri ya
kuzalisha umeme wa gharama nafuu, ukilinganisha na wazalishaji wengine
katika soko, sababu inaamini katika kutumia uwepo wake kuboresha maisha
ya wateja wake na kuleta mabadiliko katika jamii inayoizunguka.
"Uongozi
mpya wa IPTL/PAP unaamini katika kuwapatia wateja wake matokeo yaliyo
chanya. Njia pekee ya kulifanya hili ni kutoa bidhaa/huduma zenye
gharama nafuu kwa wateja, licha ya wateja hao kuwa na viwango tofauti
vya kimapato," alisema.
Mbali
na uzalishaji wa umeme, IPTL/PAP imekuwa ikijihusisha na shughuli mbali
mbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuwajengea vijana uwezo wa kifedha
ili kuweza kuanzisha Saccos yao ambayo itawasaidia kujijenga kiuchumi.
Kampuni
hiyo pia imekuwa ikiunga mkono jitihada za serikali za kufikia malengo
ya Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika elimu kwa kutoa misaada
mashuleni pamoja na taasisi za kijamii kama makanisa.
