Watu hawa kunyongwa hadi Kufa

Mahakama Kuu kanda ya Tabora, imewahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa watano wakazi wa Wilaya ya Igunga baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kumuua mume wa Mwanamke mwenye ualbino, wakati akimtetea mkewe kukatwa mkono kutokana na imani za kishirikina.


Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora, aliyekasimiwa Mamlaka ya Ziada ,Jovin Katto, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Mashitaka.

 Katika hukumu hiyo Hakimu Katto, amesema upande wa mashitaka umethibitisha pasipo shaka kwamba washitakiwa hao, ndio waliotenda kosa hilo la kinyama ambalo adhabu yake ni moja tu ya kunyongwa hadi kufa.

 Waliopewa adhabu hiyo ni Mussa Njile Masanilo, Mhoja John Shija, Regina Kashinje Kulwa, Elizabert Masanja Shija na Biria Masanja.

Hakimu Katto ambaye ni miongoni mwa mahakimu waliongezewa Mamlaka ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu, ameongeza kwamba washitakiwa baada ya kumshambulia kwa mapanga hadi kufa, Mapambano Mashiri, walimkata mkono Mkewe ambaye ana ualbino na kuondoka nao.

Awali Upande wa Mashitaka ukiongozwa na wakili Merito Ukongoji, uliiambia mahakama  washitakiwa walitenda kosa hilo mnamo Agosti 16,2014 majira ya saa nne usiku katika kijiji cha Buhekela Wilayani Igunga.

 Amesema    siku hiyo  washitakiwa walivamia nyumbani kwa Mapambano Mashiri ambaye kwa sasa ni Marehemu na kumkata kata kwa mapanga hadi kusababisha kifo chake wakiwa na lengo ovu la kutaka kuuchukua mkono wa mkewe.

 Katika shauri hilo Hakimu Katto pia amemhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela, Bahati Kulugu, ambaye alikutwa na Mkono wa  mama huyo mwenye ualbino akiwa ameuhifadhi akitafuta mnunuzi.

Upande wa mashitaka ulikuwa umeandaa mashahidi 48 lakini kwa vile maelezo yao yalikuwa yanafanana waliofika mahakamani ni mashahidi  12 tu kati yao.

Hili lilikuwa ni moja ya matukio mabaya na ya kusikitisha yaliyotokea mwaka 2014 yakihusisha watu waliokuwa wakisaka viongo vya watu wenye ualbino kutokana na imani za kishirikina. 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo