Mabweni zaidi yateketea kwa moto Njombe

CHANGAMOTO ya kuteketea kwa mabweni ya shule za sekondari mkoani Njombe imezidi kuwatesa viongozi kufuatia kutokea kwa matukio hayo mfululizo mkoani humo.
Hivi karibuni yameshuhudiwa mabweni katika shule tatu mfululizo yakiteketea kwa moto ikiwemo lile la Shule ya Sekondari Maguvani iliyopo Makambako lililosababisha wanafunzi 92 kushindwa kuendelea na masomo.
Lingine ni la Shule ya Sekondari Mang'oto lililopo wilayani Makete ambapo chanzo chake kimetajwa kuwa ni mmoja wa wanafunzi wa kidato cha pili  kudaiwa kuchoma bweli hilo kwa lengo la kuwakomoa wenzake kwa kile alichodai wamekuwa wakimshutumu kwa wizi shuleni hapo.
Tukio hilo limetokea Machi 12, saa tatu usiku ambapo mwanafunzi huyo alikusanya magodoro bwenini ya wanafunzi wenzake na kisha kuyachoma ndani ya bweni hali iliyopeleka bweni lote kuwaka moto.
Inadaiwa kuwa siku moja kabla ya kuchoma bweni hilo mtuhumiwa alidaiwa kubomoa na kuiba bidhaa katika kibanda cha mmoja wa walimu shuleni hapo.
Akizungumzia tukio hilo mwalimu wa shule ya sekondari Mang'oto Pangani Mgaya alisema kwa mujibu wa barua aliyoiandika mwanafunzi Essau Msigwa alikiri kufanya makosa hayo ikiwemo la kuchoma bweni hilo.
Alisema tukio hilo limesababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 120 ikiwemo thamani ya jengo ambayo ni Sh milioni 80. Jeshi la polisi linamshikilia mwanafunzi huyo kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano zaidi.
Katika hatua nyingine bweni la wavulana wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Chief Kidulile iliyopo kata ya Ludewa mjini jana liliteketea kwa moto.
Bweni hilo lililokuwa likitumiwa na wavulana 83 limeteketea majira ya saa tatu usiku wakati wanafunzi wakiwa darasani wanajisomea masomo ya jioni.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Aloyce Kapelela alisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa katika ajali hiyo.
IMEANDIKWA NA SALOME MWASAMALE, NJOMBE


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo