MKAZI mmoja wa Shilabela katika Kijiji cha Taba, kata ya Ulyankulu, wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, Ndilu Mbogashi (65) ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Machi 16, Mwaka huu usiku katika kijiji cha Shilabela.
Kamanda Mutafungwa amebainisha kuwa, katika ufuatiliaji wa tukio la mauaji hayo imebainika kuwa marehemu ameuawa kwa imani za kishirikina na watu wasiojulikana na kwamba baada ya kufanya mauaji hayo walitokomea kusikojulikana.
Amesema mtoto wa marehemu aitwaye Amina Lufungulu (49) ambaye alikuwa mgonjwa anasumbuliwa na kichomi na alipelekwa na mumewe Kwilasa Ntulwa (50) kwa mganga wa kienyeji ili ashughulikiwe.
Habari zaidi zinadai kuwa baada ya kufika kwa mganga alipiga ramli, ndipo wakaambiwa mama yake ndiye mchawi wakaamua kumfuata kwenda kufanya mauaji hayo.
Kamanda wa polisi mkoani Tabora Wilboad Mutafungwa alisema watuhumiwa watatu wamekamatwa ambao ni Kwilasa Ntulwa (50) mkwe wa marehemu, Amina Lufungulu (49) mtoto wa marehemu na Therezia Paulo (57) mkazi wa kitongoji cha Sangete Wilaya ya Ulyankulu ambaye ndiye alipiga ramli chonganishi.
