Zahanati yafungwa kwa kukosa daktari

ZAHANATI ya Kijiji cha Igunga wilayani Chemba mkoani Dodoma iliyojengwa kwa msaada wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), haifanyi kazi kwa kukosa daktari. Zahanati hiyo ilizinduliwa na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka juzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa shughuli ya uhawilishaji fedha kwa kaya masikini juzi, wakazi wa kijiji hicho walisema kuwa pamoja na Tasaf kuwajengea jengo zuri la zahanati, lakini limekuwa halina maana kutokana na kukosa mtaalamu hata mmoja wa afya.
Mmoja wa wakazi hao, Amina Chande alisema pamoja na kuwapo kwa zahanati hiyo, bado wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 10 kufuata huduma kijiji jirani.
Chande alisema uzinduzi wa zahanati hiyo ulikuwa unawapa matumaini ya kupata unafuu wa uuguzi, lakini kwa sasa hali sivyo.
Waliiomba serikali kuwaletea muuguzi ili kuwasaidia kuondokana na adha wanayoipata hivi sasa. Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Chemba, Simon Butondo alisema katika kuhakikisha miradi inayoanzishwa na mfuko huo inakuwa endelevu, serikali inatakiwa kuisimamia zahanati hiyo ili kuendelea kuwanufaisha wanachi.
Hata hivyo, alisema Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini, Tasaf, awamu ya tatu, walengwa wengi wamejikwamua kiuchumi kupitia fedha ambazo wamekuwa wakizipata kama ruzuku, kwa kujenga nyumba za kisasa, kuanzisha miradi ya ufugaji kuku pamoja na kilimo tofauti na ilivyokuwa awali.
IMEANDIKWA NA SIFA LUBASI, KONDOA


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo