Sakata la baadhi ya wananchi wa kijiji cha Tandala wilayani Makete mkoani Njombe kuomba waongezewe muda wa kunywa pombe siku za wikiendi limeendelea kuchukua sura mpya, baada ya kiongozi wa dini kujitokeza na kukemea jambo hilo
Akizungumza ibadani hii leo Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Posta Tandala Mchungaji Amasha Nsemwa, amekemea vikali jambo hilo na kusema halileti picha nzuri kwa maendeleo ya Nchi na ni kinyume na maandiko matakatifu ya Mwenyezi MUNGU
Amesema inashangaza kuona mwananchi ambaye pia ni Mkristo kusimama hadharani katika mikutano na vikao mbalimbali vya kijiji kutetea suala la watu kuongezewa muda wa kunywa pombe
Amesisitiza kuwa endapo atajitokeza Mkristo yeyote Mlutheri atakayetetea jambo hilo, amejitangaza rasmi kujitenga na kanisa hilo
Mchungaji huyo amewaomba viongozi wa serikali wanaosimamia sheria za nchi kutokata tamaa juu ya jambo hilo huku akiwaomba kuwatoza faini kubwa wakristo watakaokamatwa kwa kuvunja sheria hiyo
Pia amewataka wananchi wa namna hiyo kuwa makini na maswala wanayoyatetea hadharani na kuwaomba kujikita kutetea masuala ya kimaendeleo na sio ya anasa kama pombe
Mchungaji huyo amewataka wananchi wa Tandala kutambua kuwa wana viongozi wazuri wenye maono ya mbali na ndiyo maana wanafuata sheria na kuzisimamia hivyo waache kuwakatisha tamaa
Hayo yameibuka baada ya hivi karibuni katika mkutano wa kijiji cha Tandala baadhi ya wananchi kuomba sheria zibadilishwe ili waruhusiwe kunywa pombe muda wowote kwa siku za wikiendi ambazo ni jumamosi na Jumapili
Zaidi bonyeza Play Hapo Chini:-
