Kivuko cha Mv Ukara kinachotoa huduma ya usafiri wa abiria kati ya kisiwa cha Ukara na Bugorora wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, kimezimika ghafla ndani ya ziwa Victoria baada ya kuanza safari ya kutoka Ukara hii leo majira ya saa 1.30 asubuhi na kusababisha taharuki kwa abiria zaidi ya 80 waliokuwemo ndani ya kivuko hicho.
Diwani wa kata ya Bukungu wilayani Ukerewe, Mtebe Bujege ambaye alikuwa ni miongoni mwa abiria ndani ya kivuko hicho amesema kwamba, kivuko hicho kinachotumia injini moja kilizimika wakati kilipokuwa kinakaribia kufika katika kisiwa kidogo cha sizu na kulazimika kukaa majini kwa nusu saa kusubiria matengenezo ya injini kabla ya kuendelea na safari.
Kivuko kingine cha Mv. Nyerere, kinachomilikiwa na wakala wa huduma za ufundi na umeme ( TEMESA ) mkoani Mwanza, ambacho pia kinatoa huduma ya usafiri kati ya Ukara na Bugorora wilayani hapa, siku mbili zilizopita kilizimika ghafla ndani ya ziwa Victoria kikiwa na abiria zaidi ya 100 baada ya injini yake moja kupata hitilafu na kushindwa kufanya kazi.
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe, Estomiah Chang’ah amekiri kuharibika kwa injini ya kivuko cha Mv. Nyerere na kusababisha usumbufu kwa abiria wanaotumia usafiri huo,huku afisa mfawidhi wa kivuko cha mv. Nyerere Victor Byabato akieleza juhudi zinazofanyika kuhusu matengenezo ya kivuko hicho.
Changamoto ya kuzimika mara kwa mara kwa vivuko hivyo viwili vya serikali vinavyotoa huduma ya usafiri kwa wakazi wa Ukara na Ukerewe imesababisha baadhi ya abiria kuvuka kwa kutumia usafiri wa mitumbwi.
Wilaya ya Ukerewe inayoundwa na visiwa 38 ina huduma ya vivuko vitatu kikiwemo kivuko cha Mv. Ujenzi kinachotoa huduma ya usafiri kati ya Rugezi na Kisorya mkoani mara. Vivuko vingine ni pamoja na mv nyerere kilichojengwa wakati wa uongozi wa rais mtaafu wa serikali ya awamu ya tatu mh. Benjamin mkapa na kile cha mv. Ukara kilichoanza kutumika mara tu baada ya tanganyika kupata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 60.
Chanzo:ITV
