MWILI uliokuwa umeanza kuoza wa mwanafunzi mmoja wa kidato
cha nne umepatikana katika choo chenye kina cha futi ishirini
kinachoendelea kujengwa katika Shule ya Sekondari kijijini Ekalakala
kaunti ndogo ya Masinga.
OCPD wa eneo hilo Bw Musha Juma amesema kuwa polisi
walipashwa habari na raia ambao waliingiwa na wasiwasi baada ya harufu
mbaya kuanza kutoka kwa vyoo hivyo ambavyo ujenzi wake unaendelea.
Bw Juma alisema mwendazake mwenye umri wa miaka 19
alikuwa mwanafunzi katika shule ya mseto ya Secondari ya Kakuku katika
kijiji cha Ekalakala.
"Mwili aliondolewa kutoka kwa shimo hilo la futi 20 na
maafisa wa polisi wakisaidiwa na majirani karibu na shule ukiwa bado
katika sare za shule yake," akasema Bw Juma.
Bw Juma alisema kuwa marehemu alikuwa miongoni mwa
wanafunzi ambao walitumwa nyumbani Julai 31 baada ya bweni moja katika
shule kuchomwa na watu wasiojulikana.
Kushuku
Alisema kuwa polisi wanashuku kuwa mwendazake aliteleza na kuanguka ndani ya shimo kabla ya utawala wa shule kuwatuma nyumbani.
"Mwanafunzi huyo aliripotiwa kupotea katika ofisi yetu mnamo Agosti 10, nasi tukaanza uchunguzi," OCPD akasema katika mahojiano Swahilihub kwa simu.
Bw Juma alisena kuwa mwili umepelekwa katika chumba
cha kuhifadhi maiti jijini Nairobi ili kubaini kiini cha kifo cha
mwanafunzi huyo.