AFISA wa polisi Jumatano alinusurika kifo katika Kaunti ya
Migori wakati aliposhambuliwa na wahudumu wa boda boda kwa kushukiwa
kuwa mwizi. Polisi huyo alishambuliwa na waendeshaji hao wa boda boda
katika soko lililo mjini ambapo alipewa kichapo alipokataa juhudi zao za
'kumkamata’.
Hata hivyo, aliponyoka kifo kwani aliokolewa na
wenzake waliofyatua risasi hewani mara kadha na kutawanya umati huo
wenye ghadhabu.
Milio ya risasi ilisababisha mtafaruku sokoni na kupelekea wafanyabashara na wateja kukimbilia usalama wao.
Afisa huyo alikuwa amedaiwa kuiba pikipiki iliyomilikiwa na Bw Dan Omollo mwezi uliopita, ingawa alikana madai hayo. Pikipiki haikuwa imepatikana kufikia Jumatano.
Afisa huyo alikuwa amedaiwa kuiba pikipiki iliyomilikiwa na Bw Dan Omollo mwezi uliopita, ingawa alikana madai hayo. Pikipiki haikuwa imepatikana kufikia Jumatano.
Lakini katika hali ya kushangaza, Bw Omollo na
mwendeshaji mwingine wa pikipiki walikamatwa baadaye na kufungwa seli
kwa “kujaribu kusababisha kifo cha afisa wa polisi”.
“Mbona wanamkamata mlalamishi badala ya kukabiliana na
mshukiwa mkuu? Hatutapumzika hadi achukuliwe hatua za kisheria,”
akasema dadake, Bi Jemimah Anyango.
Bw Omollo alikuwa tayari ameandikisha taarifa kwa
polisi katika kituo cha Migori mnamo Julai 11, siku ambapo pikipiki yake
ilipotea katika mtaa wa Chamkombe.
Alidai mshukiwa alikuwa mteja wake lakini baadaye
alitoroka na pikipiki yake. Mkuu wa polisi wa Kaunti ya Migori Bw David
Kirui alisema hawatamlinda afisa huyo kama atapatikana na hatia.
“Tumeanzisha uchunguzi kubainisha ukweli. Kama
tutapata ana hatia, ataadhibiwa,” akasema Bw Kirui. Alisema wahudumu wa
boda boda waliopelekwa kituoni hawakuwa wamekamatwa bali “wanahojiwa
kutoa habari zaidi kuhusu tukio hilo.”