KULIZUKA hekaheka Alhamisi katika kituo cha uchukuzi cha mji
wa Isiolo baada ya maafisa wa polisi kushambuliwa na raia kwa mawe
walipojitokeza kumkamata mhalifu.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Isiolo Bw George
Natembeya, maafisa hao walikumbana na umati uliokuwa na nia ya
kuwazuilia kumkamata mshukiwa mmoja na ambaye alitambuliwa kama Bw
Mohammed Ali aliyekuwa ameripotiwa kwa kupiga na kuvunja kioo cha gari
kwa mawe.
“Kuna mmiliki wa gari la uchukuzi aliyejitokeza katika
kituo cha polisi cha mji wa Isiolo akilalamika kuwa gari lake lilikuwa
limeharibiwa na mshukiwa mmoja anayehudumu katika steji hiyo. Ndipo
maafisa walitumwa kumkamata mshukiwa huyo,” akasema.
Lakini, akaongeza, maafisa hao walipoonekana katika
steji hiyo wakimuulizia mshukiwa huyo, umati uliwakabili kwa mawe hadi
afisa mmoja akabaki akiwa ameumizwa kwa kupigwa mawe kifuani.
“Ilibidi maafisa wa polisi kufyatua risasi kadhaa
angani ili kujinusuru. Waliitisha usaidizi wa maafisa wengine ili
kudhibiti hali lakini ikawa ni kazi bure tu kwa kuwa mshukiwa alihepa,”
akasema.
Uhalifu
Bw Natembeya alisema kuwa polisi hao waliwakamata
washukiwa 20 ambao walinaswa wakishiriki uhalifu huo wa kushambulia
maafisa wa polisi kinyume cha sheria.
“Washukiwa hao wote watafikishwa mahakamani Ijumaa
kujibu mashtaka ya kuzua fujo iliyovuruga amani ya umma, kushambulia
maafisa wa polisi kwa nia ya kuwazuia kutekeleza wajibu wao wa kisheria
na pia kumsaidia mshukiwa wa uhalifu kukwepa mkono wa kiasheria,”
akasema.
Bw Natembeya alisema kuwa “makanga huwa na dhana
potovu kuwa wako juu ya sheria na wanaweza wakatekeleza utundu wowote
pasipo kujali.”
Alisema wakati umewadia kwa makanga wote wa Isiolo
kuwelewa kuwa kuna sheria ya kufuatwa na kila Mkenya na “ukiikiuka, kuna
uwajibikaji katika kujitetea ni kwa nini ukafanya maamuzi ya kukaidi na
ukaishia kuyatekeleza.”