MTOTO aliyezaliwa ndani ya ndege iliyokuwa ikisafiri angani
ametunukiwa zawadi ya kilomita 1.6 milioni ambazo atasafiri bila kulipa
nauli katika ndege za shirika la Cebu Pacific atakapokuwa mkubwa.
Mtoto huyo, Haven, alizaliwa wakati
ndege ya shirika la Cebu Pacific la Ufilipino, ilikuwa ikisafiri kutoka
Dubai kuelekea Manila.
Kulingana na madaktari, mama ya Haven alijifungua mnamo Agosti 14, wiki tano mapema kabla ya muda wake kuwadia.
Wauguzi wawili ambao walikuwa
wameabiri ndege hiyo walimsaidia mwanamke huyo kujifungua. Rubani wa
ndege hiyo alitua ndege hiyo kwa dharura katika uwanja wa Hyderabad,
India ambapo mwanamke huyo alipelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Kulingana na shirika la CNN,
mkurugenzi wa Cebu Pacific, Lance Gokongwei, alimtuza mtoto huyo maili
1,000,000 ambapo atasafiri bila kulipia tiketi kama zawadi ya kuzaliwa.
"Tunafurahi sana kwani mtoto na mama yake wanaendelea vyema kiafya,” akasema mkrugenzi huyo.
Zawadi hiyo inamaanisha kuwa mtoto huyo anaweza kwenda na kurudi nchini Amerika kutoka Kenya mara 32.