Siku chache baada ya Rais John Magufuli
kuvunja Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini
(TPA) kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ipasayo shughuli
za taasisi hiyo, mmoja wa wajumbe wake, Donata Mgassa
amevuliwa uongozi wa kitengo cha manunuzi cha Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM).
Bodi ya TPA ilivunjwa Desemba 7 baada ya kugundulika kuwa
zaidi ya makontena 2,670 yalipita Bandari ya Dar es Salaam bila
kulipiwa kodi, hivyo kuikosesha Serikali mapato yake.
Kutokana na uzembe huyo, Rais aliivunja na kutengua uteuzi wa mwenyekiti wake, Profesa
Joseph Msambichaka na katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Shaaban Mwinjaka huku mkurugenzi mkuu wa TPA, Awadh Massawe akisimamishwa kazi.
Licha ya Mgassa kuwa mjumbe wa bodi hiyo, pia alikuwa meneja wa idara ya manunuzi ya UDSM.
Alipotafutwa kuzungunzia sakata hilo, kwa ufupi Mgassa alisema: “Samahani, siwezi
kulizungumzia hilo.”
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala alithibitisha kuenguliwa kwa mjumbe
huyo. “Ni mabadiliko ya kawaida ambayo yanalenga kuimarisha utendaji uliotukuka wa chuo
kikuu hicho,” alisema na kuongeza kuwa:
“Alishamaliza muda wake ndiyo maana tukaona ni vema tubadili damu.
Tumeingiza damu mpya
ili kuendana na kasi ya miradi tunayotarajia kuwa nayo.”
Bila kuhusisha kilichotokea TPA, Profesa Mukandala alisema mabadiliko hayo yamefanywa
kuanzia Desemba 7, siku ambayo bodi ya TPA ilivunjwa na Rais Magufuli.
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vingine chuoni hapo vinaeleza kuwa huo ni utaratibu wa siku
nyingi miongoni mwa watendaji wake waandamizi na kwamba yeyote ‘anayeharibu’ sehemu moja
anakotumika akiwa mjumbe wa bodi chuo pia humwajibisha.
“Ni kanuni za chuo. Asingeweza kubaki.
Mara tu baada ya Rais kuvunja bodi ya Bandari chuo
nacho kilitangaza kumuondoa kwenye nafasi yake. Mtu mpya ameshapatikana na ameanza
kuisimamia ofisi hiyo,” kilisema chanzo hicho. Mbali na Mgassa, wajumbe wengine waliokuwa
kwenye bodi hiyo ni Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson, Dk Francis Michael, Crescentius Magori, Flavian Kinunda, Haruna Masebu, Gema Modu na Musa Nyamsibwa
Chanzo:gazeti mwananchi
