Rais Jakaya Kikwete amefungua daraja la mto Malagarasi lililopo barabara kuu ya Kigoma Tabora ambapo pamoja na mambo mengine linatarajiwa kuwa kichocheo cha kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa mikoa ya magharibi na kuwa kiungo kikuu cha mawasiliano kati ya mikoa hiyo na nchi jirani za ukanda wa maziwa makuu.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 275 lililopo katika bonde la mto Malagarasi lenye upana wa kilometa 2 linatajwa kufungua ukurasa mpya wa maisha ya wakazi wa mikoa ya Tabora Kigoma Rukwa Katavi kwa kuiungaisha na maeneo mengine nchini na nchi za jirani adha waliyokuwa wanakabiliana nayo kwa zaidi ya miaka 50 ambapo rais Kikwete anawataka kutumia fursa hiyo vizuri katika kujiletea maendeleo.
Awali akimkaribisha rais Kikwete kwa niaba ya waziri wa ujenzi Dk John Magufuli waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi amesema kuwepo kwa daraja hilo kumepunguza umbali wa zaidi ya kilometa 300 kutoka Kigoma mpaka Dar ambapo awali wasafiri walikuwa wakitumia zaidi ya siku mbili kufika maeneo hayo lakini hivi sasa safari hiyo ni ya siku moja tu.
Kwa upande wake mtendaji mkuu wa wakala wa barabara nchini Tanroads mhandisi Patrick Mfugale ameelezea utekelezaji wa mradi huo huku akiwataka watumiaji wa daraja hilo kuzingatia vigezo ikiwemo kuepuka kupitisha mizigo inayozidi viwango vinavyohitajika ili liweze kudumu kwa miaka mingi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
Kwa upande wake balozi wa jamuhuri ya watu wa Korea Kusini ambaye serikali yake imechangia asilimia 78.7 ya ujenzi wa daraja hilo amewataka watanzania kulitumia sambamba na utitiri wa rasilimali zilizoko ili kuinua uchumi wa taifa.