Nianze kwa kukuuliza wewe mzazi; unapoweka picha ya mtoto wako
kila hatua tangu akiwa mchanga hadi anaanza kutembea na kuanza shule,
alikuomba au ulipata ruhusa yake?
Ingekuwa wewe umepigwa picha bila idhini yako halafu ukaikuta kwenye mtandao utafurahi?
Najua unampenda mtoto wako na ana haki zake za
msingi pamoja na kuheshimiwa faragha yake popote alipo. Haiwezekani
chochote anachofanya ukiweke kwenye mtandao.
Naomba kueleza madhara yanayoweza kutokea kwa
kuweka picha za mtoto wako au wa mwenzako kwenye mitandao hasa mitandao
ya kijamii kama facebook, instagram na mingineyo.
Kwanza fahamu kuwa kampuni karibu zote za mitandao
ya kijamii zimesajiliwa Marekani, chache zimesajiliwa Ulaya na Asia,
lakini karibu zote zinatumia sheria na sera za mataifa hayo.
Katika mataifa hayo wanasisitiza mtoto asijiunge
kwenye mitandao ya kijamii hadi atakapofikisha miaka 13, wengine miaka
15 au 16 .
Kampuni zote za mawasiliano zina utaratibu wa
kuhifadhi kila kitu kinachotokea kwenye shughuli zao za kila siku kwenye
chombo maalumu cha kuhifadhi taarifa za mtandao (server). Kwa hiyo
ukiweka picha za mtoto zinahifadhiwa huko hata kama utazifuta.
Hapo awali, nilisema mtoto anahitaji faragha yake,
unaporusha picha za mtoto wako kwenye hii mitandao au mawasiliano
yoyote, unaingilia faragha yake na huko mbele anaweza kukushtaki wewe au
wengine walioingilia faragha yake.
Mtoto anatakiwa kufunzwa kuanzia mdogo kabisa
kuhusu faragha yake, nini cha kusema au kutoa na nini asiseme au asitoe.
Hii ni pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, simu na huduma nyingine za
mawasiliano .
Umeshawahi kuona wanasiasa wanaweka picha za
watoto wao au ndugu zao wa karibu kwenye mitandao hasa ya kijamii ?
unajua ni kwa nini ?
Kwa sababu kila anachofanya yeye kinamwathiri
mtoto wake au watu wake wa karibu kwa ubaya au uzuri. Ni rahisi kuweka
rehani faragha za watoto na ndugu zake.
Kama ni mtoto wa kike anaweza kuanza kufuatiliwa
na ‘mabazazi’ kwa sababu ya picha tu. Watatafuta anapoishi, shule
anayosoma na usishangae siku moja akabakwa.
Siku hizi kuna biashara ya kutangaza ngono mitandaoni ukiweka
picha ya mtoto hujui kina nani wanaangalia na kwa matumizi gani. Wapo
wanaoweza kuitumia picha hiyo kutangaza kuwa mwenye picha anafanya
biashara ya ngono, utajisikiaje kama mzazi?
Hata hivyo, picha ya mtoto wako inaweza kutumika kutangaza biashara fulani bila wewe kujua. Haya yameshatokea.
Kwa kuweka picha ya mtoto wako, unatoa fursa ya
kunyanyaswa na kufanyiwa vituko vingine mbalimbali shuleni au popote
atakapokwenda au kwenye kurasa zake mwenyewe za facebook.
Pia siku hizi kuna mitandao na tovuti nyingi
zinazotengenezwa kila siku, mtu anaweza kutumia picha ya mtoto wako
kutangaza tovuti yake, blogu au bidhaa zake mbalimbali bila ruhusa yako
wala ya mtoto wako.
Jijini Dar es Salaam kuliwahi kutokea mzazi kufiwa
na mtoto wake maeneo ya Kimara, aliposambaza picha akaweka ya mfano,
kumbe picha hiyo ni ya mtu mwingine, watu kwenye mtandao wakajua ndio
mtoto halisi.
Sikutishi ila nasisitiza mzazi uheshimu faragha ya mtoto wako na taarifa zake nyingine zinazomuhusu.
Na Yona Fares,Mwananchi
Na Yona Fares,Mwananchi