Halmashauri ya Wilaya ya Hai yazindua kituo cha huduma jumuishi cha kushughulikia ukatili wa wanawake na watoto.UNICEF Tanzania yawateua AY na Faraja K. Nyalandu kama Mabalozi wao wakuhamasisha umma juu ya ukatili dhidi ya watoto
Hai,
16 June, 2014 –Katika kusherehekea siku ya Mtoto wa Afrika tarehe 16
Juni, Halmashauri ya Wilaya ya Hai, ikishirikiana na viongozi wa
serikali, UNICEF na Save the Children, imezindua Kituo cha Huduma
Jumuishi, kitakachowasaidia wanawake na watoto ambao wameathiriwa na
ukatili.
“Katika
kituo hiki, huduma za kuwasaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia na
ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na huduma za afya, msaada wa
kisaikolojia, ulinzi/usalama na msaada wa kisheria vinaweza kutolewa
hapo katika eneo moja ndani ya kituo cha afya zikiwa zimeratibiwa vizuri
Zaidi,” alisema Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii.
Aliongeza,
“kituo hiki kitasaidia kupunguza madhara zaidi ya ukatili kwa sababu
wahanga wa ukatili wataweza kupata huduma zote muhimu katika eneo moja
na hawatakuwa na sababu ya kurudiarudia kuwaeleza watoa huduma
mbalimbali walio katika maeneo tofauti yale mambo mabaya waliyoyapitia,
au kutakiwa kwenda na kurudi kutokana na ukosefu wa uratibu na uwezo wa
watendaji wa sekta mbalimbali katika kuwahudumia wahanga wa ukatili kwa
ukamilifu.”
Mwakilishi
wa UNICEF Tanzania, Dk. Jama Gulaid, anaamini kuwa kama tukifanya kazi
kwa ushirikiano na serikali na wadau wengine, tunaweza kupata suluhu
katika kumaliza ukatili dhidi ya watoto. “Ukatili dhidi ya watoto uko
kila mahali na hatuwezi kuendelea kuufumbia macho. Watoto wote hapa
Tanzania wanahaki ya kuishi na kukua katika mazingira yasiyo na ukatili.
Kama sisi sote tukifanya kazi kwa kushirikiana pamoja, sina shaka
tutaweza kumaliza ukatili dhidi ya watoto.”
Katika
tukio hili huko Hai, UNICEF Tanzania imemteua msanii mahiri wa bongo
flava Ambwene Yessyah, anayejulikana zaidi kama AY, pamoja na aliyewahi
kuwa Miss Tanzania, Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi wao katika
‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto.’ Wote wameahidi kusaidia
kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’ na wameonyesha
kuhamasishwa na heshima hii waliyopewa kutoa sauti zao kutetea ulinzi wa
mtoto.
“Nimepewa
heshima kubwa kwa kuteuliwa kwangu kuwa Balozi wa UNICEF Tanzania na
nitajitoa katika kutumia sauti yangu na umaarufu wangu kusaidia
kutokomeza ukatili dhidi ya watoto hapa Tanzania,” alisema AY alipokuwa
akikubali wadhifa huo.
Kwa
kuwateua AY na Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi wa UNICEF Tanzania wa
kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’, UNICEF
inategemea kuongeza uzito na muonekano zaidi wa suala la ulinzi wa mtoto
katika mijadala inayoendelea kuhusu ukatili dhidi ya watoto na
kuonyesha kuwa kuna suluhisho la tatizo hili. Kama mwazo wa kazi yao
katika shughuli za UNICEF Tanzania, AY na Faraja Kotta Nyalandu
walitembelea Dawati la Jinsia na Watoto katika kituo cha Polisi cha Hai
kuona wenyewe kazi inayofanywa kusaidia wanawake na watoto waliofanyiwa
au kuathiriwa na ukatili.
Utafiti
juu ya Ukatili Dhidi ya Watoto, uliozinduliwa na Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2011, unaonyesha mambo yanayopelekea
uhatarishi wa watoto kwenye ukatili kimwili na kingono hapa Tanzania –
wastani wa msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 wamefanyiwa
vitendo vya ukatili wa kingono, na zaidi ya asilimia 70 ya wasichana na
wavulana wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kabla hawajafikia
umri wa miaka 18. Hata hivyo, wahanga wengi hawajamwambia mtu yeyote
ukatili waliofanyiwa na ni kesi chache sana zimefikishwa polisi.
Kumekuwa
na maendeleo katika kuboresha hali hii. UNICEF inasaidia serikali ya
Tanzania kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kuanzisha na kuboresha ‘mifumo
ya Ulinzi wa Mtoto’ katika halmashauri 13. Katika halmashauri hizi,
afya, ustawi wa jamii, polisi, sekta za elimu na mahakama, magereza,
wanasheria, asasi za kiraia pamoja na mifumo ya kijamii isiyo rasmi
wanaunda Timu ya Halmashauri ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto na
wanashirikiana kuhakikisha kuwa kesi za ukatili wa watoto
zinashughulikiwa vyema na pia wanazuia ukatili kwa kuongeza uelewa wa
jamii juu ya ukatili dhidi ya watoto. Lengo la Idara ya Ustawi wa Jamii ni kupanua utaratibu wa mfumo huu katika halmashauri 30 ifikapo mwaka 2016.
