Kamati ya bunge la bajeti imetaadharisha serikali kuwa bajeti ya
mwaka 2014/15 uenda ikashindwa kutekelezeka toka siku ya kwanza kutokana
kuwepo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya zaidi ya trilioni 2.9
ambayo ni sawa na asilimia 4 ya pato la taifa.
Akiwasilisha taarifa ya kamati ya bunge bajeti
kuhusu hali ya uchumi wa taifa na mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka
2014/15, mwenyekiti wa kamati ya bajeti Mhe. Andrew Chenge amesema
tatizo la kutosimamiwa kwa umakini matumizi ya serikali kumesababisha
kuongezeka kwa matumizi kila mwaka na malimbikizo ya madeni kutoka
bilioni 611.4 hadi trilioni 2.09 kutokana na kutolipwa katika bajeti ya
kila mwaka.
Msemaji mkuu wa kambi ya rasmi ya upinzani bungeni
Mhe. Esther Matiko akiwasilisha mpango wa maendeleo wa taifa mwaka
2014/15 amesema mpaka sasa serikali haijawa na uhalisia wa bajeti yenye
lengo la kupunguza umasikini kwa Watanzania yenye mtazamo wa kuwawezesha
watu masikini, wajasiliamali na walaji.
Kwa upande wake msemaji mkuu wa kambi ya upinzani
upande wa fedha Mhe. James Mbatia amesema tarakimu zilizowasilishwa
bungeni zimeonyesha kuwa serikali imeweka kipaumbele zaidi katika
matumizi ya kawaida kuliko ya maendeleo na kutaka deni la taifa
litenganishwe na matumizi mengine yanayohusu mfuko mkuu wa hazina hatua
mbayo mpaka sasa serikali haijatoa taarifa fasaha ya utekelezaji wa
mapendekezo hayo.
Aidha wakichangia mjadala wa bajeti kuu baadhi ya
wabunge wameitaka serikali kuwekeza katika utafiti wa kila tatizo na
kutupia lawama baadhi ya viongozi kutokuwa wabunifu wa katika kuongeza
mapato na badala yake kung’ang’ania vyanzo vilevile vya mapato ikiwemo
Juisi na Soda.
