AJALI MBAYA YAUA WAOMBOLEZAJI 12 MKOANI KILIMANJARO WALIOKUWA WAKIENDA MSIBANI


Waombolezaji 12 waliokuwa njiani kuhani msiba wa mtoto aliyepoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko, wamefariki dunia na wengine saba wamejeruhiwa, baada ya gari lao kugongwa na malori mawili kwa wakati mmoja.

Abiria hao walikuwa wanasafiri na gari dogo aina ya Toyota Pick Up namba T 170 AKZ kwenda kuhani msiba uliotokea katika kijiji cha Kongei kilichoko Hedaru mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz waliofariki ni Stella John (45), Salma Kizoka (33), Marry Senzige (49), Neema Daniel (52), Rehema George, (29), Sophia Mbike (51), Ritta Kallani (55) na Kallan Stephano (55), Kolina Mmasa (55) na Bahati Daudi (25),

Wengine ni Farida Kiondo (24) na Maria John (33) wote wakazi wa Kongei na kwamba miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Same.

Boaz aliwataja majeruhi kuwa ni Zubeda Mrindoko (42),Mipa Chediel (29) na Zubeda Mlita (32) ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kutokana na hali zao kuwa mbaya zaidi.

Wengine waliolazwa hospitalini Same ni Joyce Kandogwe (29), Subira Juma (22), Ramadhan Msangi (31) na Adinan Rajab (31).

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:00 usiku katika barabara kuu ya Tanga-Moshi, nje kidogo ya mji wa Hedaru, ikihusisha magari matatu ambayo ni Fuso (T 299 ANM) ikitokea Moshi kwenda Dar es Salaam na Scania (T 737 AKW) pamoja na tela lake namba T 776 CCN ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi.

Alisema watu hao walikuwa wamepanda gari la Diwani wa Kata ya Hedaru (CCM), Gerald Gwena aliyekuwa amewapakia waombolezaji hao kwenye pick-up yake ambayo iligongwa kwa nyuma na Fuso na baadaye gari hilo kuparamiwa kwa nyuma na Scania na kisha kusababisha vifo na majeruhi.

"Waombolezaji hawa walikuwa wanakwenda na diwani kuifariji familia ya marehemu mzee Mwanga ambaye mtoto wake wa kiume, Dismas Mwanga alifariki baada ya kusombwa na mafuriko”, alisema.

Alisema Dismas mwenye miaka tisa aliyekuwa anachunga kondoo milimani alifariki dunia juzi mchana baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha mfululizo.

Alisema hata, hivyo mpaka sasa haijafahamika iwapo mvua hizo zimesababisha vifo na hasara nyingine.

Kapufi alisema kamati yake ya ulinzi na usalama imekutana kwa dharura kujadili ajali hiyo na hatua ambazo wilaya hiyo itachukua.

Kamanda Boaz, alisema chanzo cha ajali hiyo ni kuzimika ghafla kwa  gari hilo mali ya diwani Gwena ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo.

"Ajali hiyo ilitokea baada ya gari hilo kuzimika na Fuso iliyokuwa karibu kuteleza barabarani baada ya kujaribu kusimama ili isigongane na Pick Up iliyokuwa na waombolezaji, lakini lilivutwa na tope lililokuwa limejaa barabarani kisha kugonga kabla ya kupinduka na kuangukia upande wa kulia wa barabara ambako kulikuwa na lori la Scania.

Kamanda alisema watu 10 walikufa papo hapo , wawili walifia hospitalini na saba wamejeruhiwa.
Alisema juhudi za kuwasaka madereva  hao wa Fuso pamoja na diwani huyo zinaendelea.

>>Nipashe


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo