Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Juma
Mwapachu leo ametangaza kujivua uanachama
wa chama hicho kutokana na chama kupoteza
dira.
Tamko la Balozi Mwapachu ambalo Mwananchi
imethibitisha kutoka kwake linasema kuwa
kuanzia kesho kada huyo wa CCM hatakuwa tena
mwanachama wa chama hicho tawala na
kuongeza kuwa bado hajaamua kujiunga na chama kingine.
‘’Kuanzia kesho mimi si mwana CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia
ofisi ya CCM ya kata yangu Mikocheni, Dar es Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga
na chama kingine. Mwenyezi Mungu anilinde,” inasema sehemu ya tamko hilo.
Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa miaka 48 sasa amesema
kuwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho, chama
kilidhihirisha kutokuwa chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia kwa
kumuengua waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye anapendwa na
wengi ndani ya chama.
Mwapachu amesema kuwa Lowassa na wanachama wengine wa CCM waliojitoa ni
sahihi hivyo naye anaungana nao.
‘’Kujitoa kwake uanachama wa CCM hivi karibuni ni sahihi kabisa kwasababu CCM
si chama tena cha watu. Kimetekwa, na mimi nakubaliana na msimamo wa
Lowassa na hao waliyofuata kutoka ndani ya CCM,’’ alisema Mwapachu.
Mwapachu ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho lakini pia
amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
CHANZO:
MWANANCHI.