POLISI WAACHA KAZI NA KUHUDHURIA MAZISHI YA MTU ALIYEJINYONGA NA KUACHA UJUMBE WA KUTAKA POLISI WAHUDHURIE MSIBA WAKE

 Nyeri
MAAFISA wawili wakuu wa Serikali katika kaunti ya Nyeri, jana walilazimika kuacha sherehe za siku kuu ya mashujaa na shughuli zao zingine za kikazi ili kuhudhuria mazishi ya mkazi aliyewaagiza wasikose kuhudhuria mazishi yake kabla ya kujinyonga.
Naibu kamishna wa wilaya ya Tetu Bw Haman Shambi na kamanda wa polisi wa utawala Bw Wilfred Chacha, walisema walifahamishwa kwamba John King’ori aliacha ujumbe akiwaagiza lazima wahudhurie mazishi yake.

Bw King’ori alijinyonga siku chache zilizopita nje ya nyumba yake katika lokesheni ya Hu-hoini kaunti ya Nyeri na kuacha ujumbe huo uliopatikana na maafisa wa polisi waliochunguza kifo chake.

Bw Shambi na Bw Chacha walishtushwa na agizo la marehemu la kuwataka wasikose kuhudhuria mazishi yake.
“Nilishtuka kwa sababu sijawahi kualikwa na marehemu maishani mwangu nihudhurie mazishi yake,” akasema Bw Shambi.

Maafisa hao wawili walikuwa wanamfahamu Bw King’ori alipokuwa mfanyakazi wa afisi za Hazina ya eneo Bunge la Tetu (CDF).

Walikiri kwamba hawakufahamu kwa nini aliandika ujumbe huo na kuongeza kwamba angesema sababu ya kuwataka wafike kwenye mazishi yake.

“Kulingana na desturi za Kiafrika, sio kawaida kupuuza ombi la marehemu, kwa hivyo nilifika ili kuepuka laana. Hata hivyo, ninashangaa kwa nini alitaka nihudhurie mazishi yake,” akasema Bw Chacha.

Maafisa hao walisema walilazimika kuacha shughuli zao ili kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.

“ Nilipasa kuchunguza kesi ya wizi wa mitambo ya stima lakini nikamtuma naibu wangu ili niitikie wito wa marehemu,” akasema Bw Chacha.

Alieleza kwamba awali marehemu alijaribu kujinyonga lakini familia yake ikamzuia.

“Kujaribu kujitoa uhai ni tendo la uhalifu na pengine angekuwa hai kama familia yake ingeripoti kwa polisi kwa sababu tunapowakamata wanaojaribu kujinyonga, tunawapa ushauri nasaha,” akasema.

Bw Shambi alisema marehemu alikuwa na shida tangu afutwe kazi katika ofisi za CDF.

“Binafsi nilimsaidia na magunia ya mahindi na maharagwe lakini sikuweza kumsaidia kupata kazi tena katika afisi za CDF kwa sababu kipindi chake kilikamilika,” akasema na kuwataka wakazi wawasaidie wenzao walio na shida.

Chifu wa eneo hilo Duncan Mureithi alisema marehemu alikuwa mtu mchangamfu aliyekuwa akitoa habari kwa wakazi kuhusu matukio muhimu.

Hata hivyo, aliongeza kwamba alikuwa akigombana na mkewe kila wakati.

Chifu huyo alisema kabla ya kujinyonga, mkewe alitembelea ofisi yake kutafuta ushauri kuhusu ndoa yao.

“Mke wangu alikuja kwa afisi yangu kutafuta ushauri wa jinsi ya kutatua mzozo wa ndoa yao, lakini mumewe alikataa kufika na kuamua kuzungumza kwa simu kusuluhisha mzozo huo,” akasema Bw Mureithi.

Aliongeza kwamba marehemu alikuwa na watoto watatu na kifungua mimba alikuwa shule ya upili.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo