Mkuu
wa Wilaya ya Arumeru Bw. Nyirembe Munasa (Kulia) akiongea na mmoja wa
washiriki wa mafunzo ya usimamizi wa Sheria ya Mazingira na Udhibiti wa
biashara haramu ya bidhaa zinazoharibu tabaka la Ozoni. Katikati ni
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Bi. Rogathe Kisanga. (Picha
Na Lulu Mussa).
======= =========== =============
Imeelezwa
kuwa zaidi ya asilimia 90 ya Kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni hutumika
katika vipoozi (refrigerants) kama majokofu na viyoyozi na matumizi ya kemikali
hizi yapo kwa wingi katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea kama Tanzania.
Hayo
yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake
na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Bw. Nyirembe Munasa katika ufunguzi wa Mafunzo ya
Siku mbili kwa washiriki kutoka Sekta mbalimbali
wakiwemo Maafisa Forodha, Maafisa Biashara, Polisi, Mahakama, Waendesha
Mashtaka, Uhamiaji, Wataalamu wa Mazingira na Vyombo vya Habari.
Amesema,
tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa mionzi ya kikiukaurujuani
(Ultraviolent-B radiation) husababisha kuongezeka kwa magonjwa ya saratani ya
ngozi, uharibifu wa macho na upungufu wa uwezo wa mwili kujikinga na maradhi.
Hata
hivyo, katika kukabiliana na changamoto za mionzi hiyo mwaka 1993 Serikali ya Tanzania iliridhia mkataba wa Vienna na
Montreal kwa lengo la kudhibiti na kusitisha utengenezaji na matumizi ya
kemikali zinazoharibu tabaka hilo kwa awamu kwa kuzingatia upatikanaji mbadala
na rafiki kwa Tabaka la Ozoni.
Japokuwa
juhudi za kuhamasisha wadau kuhusu faida za kutumia kemikali mbadala na
teknolojia mpya katika vifaa na mitambo mbalimbali zimeendeleshwa kwa kipindi
kirefu, matumizi ya kemikali haribifu bado yapo.
Changamoto
hii imetokana na kupungua kwa uingizaji wa vifaa hasa majokofu na viyoyozi
vilivyotumika na vinavyotumia kemikali zisizo rafiki wa tabaka la Ozoni, uhaba
wa mitambo ya kunasa na kurejereza vipoozi katika soko na ongezeko la mafundi
wasiokuwa na taaluma na vifaa sahihi vya kuhudumia majokofu na viyoyozi.
Mafunzo haya ya siku mbili yanafanyika
katika Chuo cha Utalii Arusha na yanahusisha washiriki kutoka mikoa ya Arusha,
Tanga na Kilimanjaro.
Na Lulu Mussa
Afisa Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais – Arusha