Polisi mkoani Mwanza, inawashikilia watu watatu kwa tuhuma za
kuiba fedha kwa kutumia kadi za ATM, kwenye akaunti za wateja katika
benki mbalimbali hapa nchini.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuiba takribani Sh milioni 500 kuanzia Oktoba mwaka 2012, hadi walipokamatwa.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher
Fuime, Februari 10 mwaka huu, saa sita usiku, mtuhumiwa mmoja alikamatwa
akiiba fedha za wateja katika benki ya NMB tawi la PPF Plaza.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Salim Nassoro mkazi wa Kinondoni
Dar es Salaam, Maniki Kimani na Leonard Masunga ambao ni ndugu na wakazi
wa Nyegezi jijini Mwanza.
Alisema baada ya kukamatwa usiku huo, siku iliyofuata mtuhumiwa
huyo, aliwapeleka askari Polisi walipo wenzake na kufanikiwa kuwakamata
watuhumiwa wengine wawili pamoja na vifaa mbalimbali vya kutengenezea
kadi feki, wanazotumia kuibia wateja wa benki.
Alisema walipopekuliwa, walikutwa na kadi takribani 231 za benki
mbalimbali, zikiwemo kadi 194 za wateja wa benki ya NMB, kadi 36 za
wateja wa Diamond Trust Bank (DTB), kadi moja ya KCB na kadi 18 zisizo
na nembo.
Pia watuhumiwa hao walikutwa na kompyuta ndogo za mkononi
(laptops) tatu, printa, vifaa vya kutengeneza kadi feki, kamera ya
kuchukua picha kwa siri na rangi makopo matatu wanazotumia kupulizia
kwenye kamera zilizoko katika ATM, ili sura zao zisionekane.
Pia watuhumiwa hao walikutwa na madaftari matatu aina ya ‘counter
book’, ambayo yalikuwa yameorodheshwa namba za siri za wateja
mbalimbali, ambao taarifa zao zilikuwa zimenaswa kwa kutumia vifaa
maalumu walivyokuwa wanavibandika kwa siri, katika mashine za ATM.
Kamanda Fuime alisema kwa kutumia zana hizo, watuhumiwa hao kwa
nyakati tofauti hususani usiku, wamekuwa wakienda katika mashine za ATM
na kuchukua fedha kutoka kwenye akaunti mbalimbali.
Fedha hizo wamekuwa ‘wakizichota’ kwa kutumia kadi
walizozitengeneza wao wenyewe na taarifa za wateja zilizokusanywa na
vifaa maalumu.
Fuime alisema watuhumiwa walikutwa pia na vifaa vingine vya
kielektroniki, ambavyo havikutambuliwa kwa urahisi, hadi pale
vitakapopelekwa makao makuu ya uchunguzi wa wizi kwa njia ya mtandao na
kemikali ambazo zitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya
utambuzi.
Alisema walipohojiwa watuhumiwa hao, walikiri kuhusika na wizi wa
fedha katika mashine za ATM na wanafanya wizi huo kwa kushirikiana na
wazungu watatu, raia wa Bulgaria ambao ndio mafundi wa kutengeneza zana
wanazotumia kuiba.
Kaimu Kamanda huyo alisema Polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio
hilo na watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi
kukamilika.

