Mahakama ya Mwanzo mjini Sumbawanga, imemtia hatiani aliyekuwa
Sista wa Shirika la Kitawa la Kanisa Katoliki, Jimbo la Sumbawanga,
Yasinta Sindani, kwa kufumaniwa na mume wa mtu.
Kutokana na kutiwa hatiani, Yasinta aliamriwa kumlipa fidia ya kimila ya Sh 700,000, malalamikaji, Asteria Mgabo.
Katika kesi hiyo ya msingi ya madai, Asteria alikuwa akimtaka
mshitakiwa alipe Sh milioni 3 ya fidia, baada ya kumfumania na mumewe wa
ndoa, Martin Msangawale (39), ambaye pia ni mkazi wa mjini hapa.
Mshitakiwa huyo ambaye ni mtumishi katika Hospitali ya Mkoa wa
Rukwa mjini hapa, kwa sasa anaishi nje ya nyumba ya utawa, eneo la
Kantalamba mjini hapa.
Inadaiwa mshitakiwa ambaye alikuwa mtawa wa Shirika la Masista wa
Maria Mtakatifu Malkia wa Afrika (MMMA), ameachana na maisha ya kitawa
miaka miwili iliyopita kwa hiyari yake mwenyewe.
Katika hati ya awali ya madai, mshitakiwa alikuwa akidaiwa
kufumaniwa na Asteria akiwa na mumewe Msangawale katika nyumba ya kulala
wageni ya Chipa iliyoko eneo la Katandala mjini Sumbawanga, usiku wa
Desemba 24 mwaka jana, siku ya Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Jaffar
Mkinga, alisema ushahidi uliotolewa na mlalamikaji, ulikuwa mzito
wenye kuondoa shaka zote kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo, tofauti
na utetezi uliotolewa na mdai kwamba ushahidi ulikuwa dhaifu.
Katika utetezi wake, mshitakiwa aliiambia mahakama hiyo kuwa
kwanza alikuwa hajui kuwa Martin alikuwa mume wa mtu. Alidai kuwa pia
mwanamume huyo, alimweleza kuwa hana mke na alimwomba wafunge ndoa.
Lakini Hakimu Mkinga alipinga na utetezi huo kwa sababu siku
hiyo ya Mkesha wa Krismas, mwaka jana saa saba na robo usiku,
mlalamikaji akiongoza na Mwenyekiti wa Mtaa na mashahidi wengine
watatu, walimfumania mshitakiwa akiwa na Martin.
Alisema mdai na mashahidi hao, walimfumania mshitakiwa na Martin
wakitoka katika moja ya vyumba vya kulaa katika nyumba yakulala wageni
ya Chipa, iliyopo katika eneo la Katandala mjini hapa.
Kwa mujibu wa Hakimu Mkinga, baada ya kufumaniwa mshitakiwa na
Martin walipokubali kusaini karatasi ya ya fumanizi ya ugoni,
iliyoaandaliwa na Mwenyekiti huyo wa mtaa.
“Hivyo kama mshitakiwa ulikuwa haufahamu kuwa Martin alikuwa
hana mke, ilikuwaje ukakubali kusaini karatasi hiyo ya fumanizi
iliyoandaliwa na Mwenyekiti huyo?” Alihoji.
Hata hivyo alisema kutokana na Sheria ya Ndoa na Mirathi ya 1971,
faini ya fumanizi la ugoni si adhabu, inapaswa itolewe kulingana na
mila na desturi za eneo la tukio.
Kutokana na sheria hiyo, Hakimu Mkinga alimuamuru mshitakiwa
kulipa mara moja faini ya fumanizi la ugoni ya Sh 700,000 kwa
mlalamikaji.
“Mlalamikaji alimtaka mshitakiwa alipe Sh milioni 3 kwa ajili
ya fumanizi la ugoni, kiasi hicho si tu ni kikubwa, lakini pia ni
adhabu.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa na Mirathi ya 1971, faini ya
fumanizi la ugoni, haipaswi kuwa adhabu kwani inatatozwa kulinga na
mila na desturi za mahali husika.
“Wafipa faini ya ugoni ni ng’ombe wawili ambao thamani yake ni
Sh 600,000, mshitakiwa unaamriwa na Mahakama umlipe mara moja
mlalamikaji Sh 700,000 ikiwa ni faini ya fumanizi la ugoni,“ alisema
Hakimu Mkinga.
Akizungumza nje ya chumba cha Mahakama mara baada ya kusomwa
kwa hukumu, Asteria alikiri kuwa hukumu iliyotolewa, ameridhika nayo.
Aidha alisema amedhamiria kufungua shauri lingine mahakamani hapo,
kudai talaka.
“Baada ya hukumu hii, kesho nitaanza mchakato wa kufungua
shauri mahakamani hapa kudai talaka kwani siko tayari tena kuendela
kuishi na Martin,“ alisisitiza.
Wakati hayo yakijiri ndani Mahakama hiyo, Martin alivyokuwa
akijiandaa kuingia ndani, ghafla alizuiwa na kuwekwa chini ya ulinzi
Mahakamani hapo.
Mwanasheria wa Manispaa ya Sumbawanga, Tulalemwa Mwenda
alithibitisha kukamatwa kwa Martin, akituhumiwa kujifanya Ofisa Ardhi
wa Manispaa hiyo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
“Tumekuwa tukimtafuta kwa muda mrefu, sasa leo tumepata.
Amekuwa akijifanya Ofisa wa Manipaa, mara mhasibu na sasa
anajifanya Ofisa Ardhi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,“
alidai Mwenda.
Kwa mujibu wa madai ya Mwenda, Martin awali alikuwa Ofisa
Mtendaji wa Kijiji, lakini baadaye alifukuzwa kazi na kwa muda mrefu
amekuwa akitapeli wakazi wa manispaa hiyo, akijifanya kuwa Ofisa
Ardhi Mwandamizi.
