![]() |
| Josephat Mwingira. |
Mlinzi wa shamba la mifugo la Shirika la Efatha Ministry
linaloongozwa na Joseph Mwingira, ameuawa na wengine wawili kujeruhiwa
baada ya wananchi kuwavamia wilayani Sumbawanga.
Wakazi zaidi ya 200 wa Kijiji cha Sikaunga wilayani Sumbawanga
mkoani Rukwa walivamia shamba hilo la Malonje, wakawashambulia walinzi
10 na kumuua mmoja na wengine wawili walijeruhiwa vibaya.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Peter Ngusa ambaye pia
ni Ofisa Upelelezi wa Mkoa amethibitisha kuwepo tukio hilo jana.
Kwa mujibu wa Ngusa mwili wa mlinzi huyo umehifadhiwa katika
chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini
Sumbawanga kusubiri uchunguzi wa kitabibu ambapo majeruhi wawili
wamelazwa katika hospitali hiyo kwa matibabu huku hali zao
zikielezwa kuwa tete.
Jina la marehemu halikuweza kufahamika mara moja . Mmoja wa
majeruhi ni Briton Ngimili. Kaimu Kamanda alisema hakuna mtu
aliyekamatwa kuhusiana na kisa hicho. Polisi inasaka wahusika wa vurugu
hizo.
Akisimulia mkasa huo Ngusa alisema uvamizi huo unatokana na
kuwepo mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya mwekezaji, Efatha
Ministry na wanakijiji wa Sikaunga.
“Tulipata taarifa za vurugu hizo jana na tulipofika huko
tulikuta tayari walinzi wawili wa shamba hilo wakiwa wamejeruhiwa
na kuhifadhiwa ndani ya ofisi kijijini hapo hivyo walikimbizwa
haraka katika Hospitali ya Mkoa mjini hapa ambako wamelazwa kwa
matibabu,” alisema.
Alisema baada ya msako wa muda mrefu ndipo polisi waligundua
mwili wa mlinzi anayedaiwa kuuawa kikatili na wanakijiji hao.
Mlinzi wa shamba hilo, Ngilimi aliyelazwa kwa matibabu alidai
kuwa kabla ya kutokea vurugu hizo kundi dogo la wakazi wa kijini
hapo walivamia eneo la shamba hilo.
Alisema walipohojiwa na walinzi wa shamba hilo, wanakijiji hao
walianza kuwasiliana kwa simu na wenzao huku wakipuliza filimbi.
Kundi kubwa la watu wakitokea kijijini walivamia shamba na walinzi kwa
silaha.
Meneja wa Shamba hilo , Peter Kibona alidai kikundi cha watu
hao wanaokadiriwa kufikia 200 kutoka Kijiji hicho cha Sikaunga
wakiwa na silaha mbalimbali za jadi zikiwemo marungu , mapanga na
fimbo waliwashambulia walinzi hao 10 waliojaribu kuwatoa
wanakijiji kwa kuingia shambani bila kuwa na vitambulisho.
Kibona alisema walinzi hao walipewa maagizo ya kuwatishia
wakazi hao kwa kupiga risasi juu ndipo walipoanza kushambuliwa
kwa silaha hizo za jadi na kusababisha kifo cha mmoja wao .
“ Tuliwakataza kabisa walinzi wetu wasiwafyatulie risasi
wanakijiji hao waliovamia shambani bali wafyatue hewani na ndivyo
walivyofanya,” alisema.
Shamba hilo la Efatha linadaiwa kuwa na ukubwa wa hekta 10,000. Mgogoro baina ya wanakijiji na mwekezaji ni wa muda mrefu.
