JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
__________
TAARIFA MAALUM KUHUSU BUNGE NA KAMATI
______________
Ofisi ya
Bunge imepokea kwa masikitiko taarifa kuhusu tafsiri ya kusitisha
matangazo ya Shughuli za Bunge na Kamati, kinyume na jinsi ilivyoakisiwa
katika mazungumzo ya pamoja kati ya Wanahabari na Katibu wa Bunge.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa, Bunge la Jamhuri ya Muungano halina
mpango wa kusitisha matangazo ya Bunge wala Kamati zake, ambazo kwa
mahitaji ya sasa nazo zinapaswa kurushwa moja kwa moja kama sehemu ya
mpango kabambe wa kuwapasha Wananchi yanayojiri katika Uendeshaji bora
wa Shughuli za Bunge.
Dhamira
ya Bunge ni kuhakikisha kuwa mpango kabambe uliopo ni kumfikia kila
Mtanzania alipo na kwa uwezo alionao aweze kupata na kushiriki katika
uendeshaji wa shughuli za Bunge.
Hivyo
Mpango mkakati uliopo utakuwa kuboresha mawasiliano ya kawaida kupitia
Teknolojia ya Mawasiliano TEKNOHAMA, kwa wale watakaokuwa na uwezo wa
kupata huduma za mtandao, na tayari tumeanza kurusha live video striping
kupitia tovuti ya Bunge, na hata wale watakaopenda kujua zaidi, basi
wanaweza kupitia majadiliano ya Bunge kwa nyakati tofauti.
Aidha,
kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kushika mawimbi ya Radio, basi wataweza
kufuatilia majadiliano ya Bunge katika Radio ya Bunge inayotarajiwa
kuzinduliwa hivi karibuni katika masafa yanayoweza kupatikana nchi
nzima, hii ikiwa ni jitihada za ziada kwa kuwa kuna Radio zinazotoa
huduma hiyo ya moja kwa moja vizuri hadi sasa, kama vile RTD, BBC, STAR
etc.
Aidha,
kwa wale watakaoweza kuwa na uwezo wa kumudu Luninga, basi Bunge
limejipanga kuwapatia huduma hiyo moja kwa moja kupitia katika mtandao
wake mpya utakaokuwa ukirushwa masaa 24, baada ya mitambo mipya ya
kunakili majadiliano Bungeni na katika Kamati kusimikwa. Hivyo basi
utaratibu uliopo sasa utaendelea kutumika ambapo vituo vyote vya
Television vitapewa fursa ya kurusha matangazo kwa utashi wao bila
kuwekewa mipaka ya aina yoyote sambamba na matangazo yatakayotolewa na
mitandao ya Bunge.
Utaratibu
huu unatokana na uamzi wa pamoja kati ya Bunge na Tume ya Mawasiliano,
ambapo vipindi vyote vya Bunge vitakuwa vinarushwa bila kudhaminiwa na
taasisi yoyote zaidi ya mamlaka tajwa juu ya mawasiliano TCRA.
Hivyo
basi kwa maelezo hayo ni dhahiri kwua Bunge halina mpango wa kusitisha
matangazo ya TV wala yale ya Radio au Tecknohama, bali linatarajia
kuboresha upatikanaji wa huduma kwa utaratibu ulio rahisi na unaoweza
kusimamiwa na pande zote, yaani Bunge na Wananchi.
Aidha,
kwa utaratibu uliopo sasa, Bunge halirushi matangazo ya aina yoyote,
bali hutoa nakala ya majadiliano hayo kwa mtu yeyote atakaye au TV na
Radio yoyote kupitia katika mitambo yake. TV zote zinazorusha matangazo
ya Bunge hupata feed toka katika mitambo ya Bunge, na pale wanapoona
yafaa basi huomba kutumia mitambo yao na hivyo kutumia fursa hiyo
kuingiza Camera na Wanahabari ndani ya kambi la Bunge kwa minajiri hiyo.
Kuzingatia
mabadiliko tajwa, utaratibu huo umepewa ukomo, ili sasa hapatakuwa na
fursa ya kuingiza Camera ndani ya Kumbi za Bunge, bali wote watakaotaka
kurusha matangazo ya Bunge kwa utashi wao, watapata clear feed toka
katika mitambo ya Bunge na hivyo kurusha live vipindi vyote vya Bunge
bila kuhaririwa kama ilivyonakiliwa katika makala mbalimbali. Hata
hivyo utaratibu huu wa kutumia Camera katika Kumbi utaendelea katika
Kamati za Bunge, hadi hapo mitambo mipya ya mawasiliano itakapofungwa
katika Kumbi zote za Kamati.
Hivyo
basi, ili kwenda sawia na taratibu hizo, Bunge litaendesha zoezi la
kuwatathmini Waandishi wote wa habari za Bunge na kuwasajili kwa vigezo
vitakavyoafikiwa kati ya Baraza la Habari, Idara ya Habari na Bunge
lenyewe.
Aidha ili
kulinda heshima na maadili ya utangazaji, Bunge litatoa utaratibu (Code
of Conducts for Media broadcasting) wa namna ya kunakili na kurusha
matangazo ya Bunge bila kujali yanarushwa kwa utaratibu upi. Hili
litasaidia kuweka misingi bora ya mawasilaino na hivyo kuwapa fursa
Wananchi kujua hali halisi ya matukio yote ndani ya Bunge na katika
Kamati, bila kuegemea upande wowote (Non Partisan).
Hivyo
basi, wakati zoezi la maboresho hayo likiendelea, Wananchi watajulishwa
kila hatua na matarajio tajwa na kwamba tunaendelea kusisitiza tena,
Wananchi wasiwe na hofu juu ya taarifa zilizopewa uzito usio stahili za
kusitisha matangazo ya Bunge, ambao hazikuwa sahihi na pia hazikuainisha
zoezi zima la maboresho ya upatikanaji na usambazaji wa habari za
Bunge.
Tunasikitika kwa usumbufu uliowasibu wote walioakisiwa na taarifa hiyo.
Dr. Thomas D. Kashililah
KATIBU WA BUNGE
