SERIKALI
imeombwa kuwezesha ujenzi wa mabweni kwenye shule za sekondari hasa
zilizopo vijijini kwani ukosefu wa mabweni huchangia kwa kiasi kikubwa kwa
wanafunzi wa kike kupata ujauzito pamoja na kukatiza masomo.
Ombi hilo
limetolewa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari ya Chief Gijaru
John wakati akichangia kwenye mdahalo wa wananchi wa jinsia na maendeleo
ulioandaliwa na Mtandao wa asasi za kiraia Mkoani Manyara (Macsnet) na
kufanyika katika kijiji cha Balang’dalalu Wilayani Hanang’ mkoani Manyara.
Alisema kuwa
endapo Serikali ingeliweka kipaumbele kwa kujenga mabweni mashuleni hasa
vijijini,wasichana wangesoma vizuri bila kurubuniwa kama ilivyo hivi sasa
ambapo baadhi yao hupewa ujauzito na kukatisha masomo yao na ukosefu wa mabweni
ndiyo chanzo cha upatikanaji wa mimba kwa wanafunzi wa kike.
Kwa upande
wake mmoja wa washiriki hao ambaye ni mjasiriamali Mary Gitagno amewataka
wasichana kuzingatia masomo ambayo ndiyo yatakayowakomboa kwenye
maisha yao yajayo na wasikubali kurubuniwa na wanaume ili hali bado wanaendelea
na masomo yao.
Aidha
aliongeza kuwa yeye ni mzaliwa wa kijiji cha Bassotu wilayani humo ambaye
alipata elimu yake mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo wanaume
walijaribu kumrubuni kipindi hicho akisoma lakini walishindwa kumpata.
Amewaasa
wanafunzi hao wasikubali kuhadaika na kudanganywa na mwanaume wakidai kuwa eti
wao ni my moyo,kidege changu,yeye ni nyota yake!kisha unakubali kurubunika,
hivyo wasome na wasiingie huko.
Pia kutokana
na shule nyingi za sekondari kukosa mabweni wanafunzi wengi wa kike
wanapangisha vyumba vijijini huku wakiendelea na masomo yao shuleni hivyo
kuwafanya warubuniwe na wanaume kwa urahisi zaidi.
