Rais Kikwete leo anatarajiwa kushiriki katika maziko ya aliyekuwa
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi
ya Kaskazini Kati, Dk Thomas Laizer.
Askofu Laizer anatarajiwa kuzikwa leo katika Kanisa Kuu la Usharika wa Mjini Kati, uliopo katikati ya Jiji la Arusha.
Waumini wa Kanisa hilo na wananchi wa Arusha tangu jana walianza
kuuga mwili wa Askofu Laizer katika Kanisa Kuu la KKKT la Usharika wa
Mjini Kati uliopo Barabara ya Goliondoi, sehemu ambayo imetengwa kwa
ajili ya maziko.
Askofu Laizer alifariki Alhamisi ya wiki iliyopita, katika
Hospital ya Rufaa ya Seliani, inayomilikiwa na Kanisa hilo alikokuwa
amelazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu, akisumbuliwa na saratani.
Miongoni mwa wageni wanaotarajiwa katika maziko hayo mbali na Rais
Kikwete ni Mwinyi na Mkapa. Wengine ni waaliokuwa mawaziri wakuu,
Fredrick Sumaye na Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli mkoani
Arusha.
Barabara za Goliondo, India na nyinginezo zilizoko karibu na
kanisa hilo, huenda zikafungwa ikiwa ni njia mojawapo ya kuondoa
msongamano wa magari kabla na wakati wa mazishi.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dk Alex Malasusa, aliwasili
Jijini Arusha tangu Jumamosi ya wiki iliyopita na Msaidizi wa Askofu,
Solomoni Massangwa, alikaimishwa rasmi Uaskofu wa Dayosisi hiyo Jumapili
iliyopita.