Simanjiro.
WAKULIMA wa
Kijiji cha Komolo Wilaya
ya Simanjiro Mkoani Manyara wamemlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Manyara
kutokana na kitendo cha wafugaji wa eneo hilo kuingiza punda kwenye
mashamba yao hivyo kuharibu mazao yao.
Wakiongea na
Mkuu wa
mkoa huo Elaston Mbwilo alipotembelea kijiji chao kuhamasisha wananchi
wajitokeze kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi Agosti 26 mwaka huu
walisema
punda hao wamewapa hasara kubwa.
Waliongeza kuwa
wamejaribu
kufikisha kilio chao kwa uongozi wa eneo hilo ili wafugaji hao
wachukuliwe
hatua kutokana na kitendo chao cha kuingiza punda kwenye mashamba yao
lakini
hakuna hatua yoyote wafugaji hao waliyochukuliwa.
Walibainisha
kuwa ipo siku
walitaka kuzikata kwa panga punda zilizoingia kwenye mashamba na
kuharibu mazao
yao lakini waliona jambo hilo ni ukatili na utasababisha vurugu baina ya
wakulima na wafugaji wa eneo hilo.
“Hapa kijijini
kwetu viongozi hawakai
kabisa ofisini yaani kila ukienda ofisini hukuti kiongozi yeyote
nashangaa leo
hii baada ya kusikia mkuu wa mkoa anatembelea eneo hilo ndiyo wanafika,”
alisema mmoja kati ya wakazi hao.
Aidha akiongea
kuhusu
hilo,Mbwilo aliuagiza uongozi wa wilaya hiyo kufuatilia suala hilo kwa
kuhakikisha kuwa viongozi wa kijiji hicho wanasimamia zoezi la kukamata
mifugo
inayoharibu mazao yao na kuwalipa fidia wakulima hao.
“Hatuwezi
kuvumilia hali hii hivyo
viongozi wa wilaya kupitia kijiji cha Komolo wahakikishe kuwa mifugo
inayokamatwa kwenye mashamba ifidiwe na wafugaji hao ili wakulima
wasione kama
wanaonewa,” alisisitiza Mbwilo.
Kwa upande wake
mkuu wa wilaya ya
Simanjiro Kanali Cosmas Kayombo alibainisha kuwa wakazi wa kijiji hicho
pamoja na viongozi wake wanatakiwa watunge sheria ndogo za kuweza
kudhibiti
uaribifu wa mazao mashambani.
Alisema kuwa
watakapokuwa na sheria
zao ndogo hapa kijijini kwao zitawasaidia kulipwa fidia na siyo na punda
tu
hata mifugo mingine ikiharibu mazao watafidiwa pindi watakapozipitisha
sheria
hizo ndogo.