WAAMINI WAMPA PADRI WAO ZAWADI YA GARI

 Simanjiro.
 
WAAMINI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali wa Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wamempa zawadi ya gari padri Gasto Sinkala ambaye amepata upadri hivi karibuni mjini Arusha.
 
Taarifa hiyo imetolewa na mwenyekiti wa kamati ya misa hiyo,Nobert Olomi wakati akiongea   na waandishi wa habari baada ya  misa ya shukrani ya kupata upadri iliyofanyika kwenye Parokia ya Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
 
Aidha mwenyekiti huyo wa kamati ya misa hiyo,Nobert Olomi alisema kuwa gari hilo aina ya Suzuki Escudo lina thamani ya sh11 milioni.
 
Aliongeza kuwa  waamini wameona wampe zawadi ya gari hilo ili kumrahisishia usafiri padri Sinkala kwenye eneo lake la uinjilishaji huko Loliondo na pia awakumbuke waamini wa Mirerani kwa sala kila akilitumia gari hilo. 

Aidha akitoa shukrani kwa waamini wa kanisa hilo wakiongozwa na mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha,Pastory Kijuu,Aloyce Kitomari,Raphael Loratare na Theopil Mroso,Padri Sinkala alisema anamshukuru Mungu kwa kufanikisha wito wake.
 
Padri Sinkala alibainisha kuwa  japokuwa amelelewa katika mazingira na mikono ya watu tofauti wakiwemo wazazi na ndugu zake hatimaye amefanikiwa kupata daraja la upadri ambalo alikuwa na wito nao tangu akiwa mdogo.
 
“Jamani namshukuru Mungu hata kunifikisha hapa leo ingawa wazazi wangu wapo hai lakini hivi sasa wapo nyumbani Mbeya hawajashuhudia umati huu uliopo leo hii lakini furaha yangu na yenu ndiyo furaha yao pia,” alisema Padri Sinkala.
 
Naye Padri Mroso ambaye ni mlezi wa imani wa Padri Sinkala alieleza kuwa  waamini wa Mirerani wameweka rekodi kwa kununulia gari ambalo litamsaidia Padri huyo kwenye uinjilishaji.
 
“Mirerani mpo juu kwani katika historia ya Jimbo Katoliki la Arusha hakuna padri aliyepewa gari na waamini ninyi ni wa kwanza nadhani vijana wa Mirerani miaka ijayo wakipata upadri mtawapa helkopta au ndege,” alisisitiza Padri Mroso
 
Kwa upande wake Padri Pastory Kijuu aliyekuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Mirerani na ambaye anasoma chuo kikuu cha Nairobi alifafanua kuwa  kila shughuli za kichungaji atakayofanya Padri Sinkala watu wa Mirerani watabarikiwa.
 
“Mimi nilipoanza upadri mwaka 1981 nilikuwa natumia baiskeli hivyo nawapongeza kwa kumtunza gari Padri Sinkala japokuwa hata asingepata hilo gari angetoa huduma ya upadri bila matatizo,” alisema Padri Kitomari. 
 
Paroko mpya wa Kanisa Katoliki Mirerani,AlouKitomari alifurahishwa na kitendo cha waamini hao kumpa gari Padri Sinkala kupewa gari ambalo litamsaidia kufanya uinjilishaji huko Loliondo,Dikodiko na Samunge wilayani Ngorongoro.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo