Zoezi
la Sensa ya Watu na Makazi Wilayani Mufindi limeanza kwa hali ya utulivu
mkubwa
na wananchi wameendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha
zoezi hilo
linafanikiwa.
Akiongea
katika mahojiano maalumu na Afisa habari mkoa wa Iringa Denis Gondwe, Mwenyekiti wa Kamati ya
Sensa
wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu amesema kuwa katika siku ya kwanza ya
Sensa
ya Watu na Makazi Wilayani Mufindi, “kwa kweli zoezi hili lilianza saa
sita
kamili usiku katika maeneo ambayo si ya makazi ya kudumu, kazi
ilifanyika
katika Mji wa Mafinga katika maeneo ya stendi, nyumba za kulala wageni
na
maeneo yanapopaki magari makubwa ya mizigo.
Aidha, zoezi kama hilo
lilifanyika
pia katika maeneo ya Nyololo, Igowole, Kibao, Malangali, Ihowanza,
Mgololo na
Usokami hadi asubuhi saa kumi na moja kazi hiyo ilikuwa imekamilika kwa
mafanikio makubwa”.
Amesema kuwa leo asubuhi pamoja na kuanza zoezi
kwenye
makazi ya watu, wagonjwa waliolazwa kwenye vituo vyote vya huduma
wamehesabiwa
asubuhi na zoezi linaendelea kwenye makazi ya kudumu ya watu.
Akiongelea
tathmini
yake, amesema kuwa kazi ya kuhesabu watu inaendelea vizuri sana na
muitikio wa watu ni mkubwa sana katika zoezi hilo. Amesema ukubwa wa
muitikio
wa watu katika wilaya yake unatokana uhamasishaji mkubwa unaoendelea
kufanyika na
kiu kubwa waliyonayo wananchi ya kushirikiana na Serikali katika
kujiletea
maendeleo.
Evarista
ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amesema kuwa ili zoezi hilo
liweze
kufanikiwa kwa asilimia 100, viongozi na jamii kwa ujumla hawana budi
kuendelea
kutoa hamasa na elimu ili wananchi wote waweze kushiriki kikamilifu
katika
upatikanaji wa takwimu hizo muhimu kwa mustakabali wa taifa.
Aidha,
ametoa wito
kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa
wanaoendelea
kupita katika kaya zao kukusanya taarifa mbalimbali.
Amesema wananchi
watakapo
jibu kwa usahihi maswali watakayoulizwa na makarani wa Sensa watakuwa
wametimiza wajibu wao wa kushiriki katika kupanga mipango ya maendeleo
yao kwa
namna moja ama nyingine.
Katika
mahojiano kwa njia ya simu na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Iringa, Fabian
Fundi
amesema, “kwa ujumla zoezi hili linaenda vizuri na tulianza saa sita
usiku na
kuendelea nalo hadi alfajiri. Na asubuhi hii tumeanza kuhesabu kaya
binafsi
ambazo ni makazi ya kudumu ya watu”.
Amesema kuwa kamati ya Sensa Mkoa
haijapata taarifa wala matukio yasiyo ya kawaida wala kupokea simu
yoyote
kutoka kwa makarani kutaarifu kuwa kuna mtu au kaya iliyogoma
kuhesabiwa, hii
ni dalili nzuri kuwa zoezi hili litakuwa la mafanikio katika Mkoa wa
Iringa.
Sensa
ya Watu na Makazi inafanyika kwa mara ya tano nchini kote ikiongozwa na
kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa Maendeleo: Jiandae kuhesabiwa’ ipo katika
siku
yake ya kwanza na itaendelea kwa siku saba ili kuhakikisha kila
mwananchi
anahesabiwa mara moja tu.