Katibu wa
Chama cha Damokrasia na Maendeleo Mkoani Morogoro, Abel Luanda ametoa
tamko rasmi la kujiuzu nafasi hiyo na kuahidi kutoa taarifa ya chama
atakachohamia mapema wiki ijayo.
Luanda alitoa tamko hilo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa na kutaja sababu tano zilizomsababisha
kuchukua maamuzi hayo aliyoyaita kuwa ni magumu katika siasa.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni kupisha upepo mbaya
wa kisiasa ndani ya Chadema kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa, kukosa
ushirikiano na mwenyekiti wa Chadema mkoa Susan Kiwanga ambaye ni mbunge
wa viti maalumu wa chama hicho mkoani hapa pamoja na dharau iliyojengwa
na viongozi wakuu wa chama hicho kitaifa dhidi ya viongozi wa mkoa.
Sababu nyingine alieleza kuwa ni kupisha agenda ya
siri iliyofichika ndani ya M4C inayolenga kuwaondoa viongozi fulani
ndani ya mkoa na wilaya wanaoonekana kuwa na misimamo ya kupinga kambi
fulani inayojiandaa na uchaguzi mkuu wa chama hapo mwakani.
Vilevile alisema kuwa sababu iliyomfanya ajiuzulu
ni pamoja na viongozi wa ngazi ya chini kuanzia kata, jimbo, wilaya hadi
mkoa kutumiwa kama muhuri huku wakitakiwa watimize wajibu mkubwa wakati
mtetezi wa haki zao hayupo.
“Mimi naondoka lakini nawaachia ujumbe mmoja kuwa Chadema siyo
yenu ninyi viongozi wachache ambao mpo hapa kwa dhamana tu nanyi mtapita
kama waasisi wa chama hichi waliopita, lakini nawaachia chama kikiwa
salama na imara” alisema Luanda.
Aidha alisema kuwa yeye si mgeni kwenye siasa kwani
aliwahi kuwa mwanachama wa NCCR- Mageuzi na baadaye alihamia Chadema na
kupata nafasi ya udiwani mwaka 2005-2010 wa kata ya Kibungo juu ambapo
alisema kuwa katika nafasi hiyo aliweza kukiimarisha Chadema kuanzia
ngazi ya tawi hadi mkoa.
Alisema kuwa kutokana na mema aliyoyafanya kwa Chadema anaamini
kuwa wapo viongozi wengine wa chadema wa ngazi mbalimbali watakaounga
mkono maamuzi yake na kuachia ngazi hivyo aliwataka kutoogopa kukihama
chadema kwani wanaweza kufanya siasa kwenye chama chochote.
Alipotakiwa kueleza kama anania ya kuhamia CCM
Luanda alisema kuwa kwa sasa anaangalia upepo wa kisiasa na muda si
mrefu atatangaza ramsi chama atakachohamia huku akisisitiza kuwa
atahamia chama ambacho kitakuwa na misimamo na chenye kufuata katiba na
miongozo na sio kupigana majungu na fitina.
Chanzo:morogoroyetu blog
